MST-Department of Kiswahili and African Languages

Permanent URI for this collection

Browse

Recent Submissions

Now showing 1 - 20 of 254
  • Item
    Mchango wa Sitiari na Metonimu Katika Uzuaji wa Polisemia Katika Kiswahili
    (Kenyatta University, 2024-04) Masika, Mark Elphas; King'ei, Kitula Osore, Miriam
    Utafiti huu ulilenga kuangazia mchango wa sitiari na metonimu katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili ambapo uliweza kupambanua namna metonimu na sitiari zinavyoweza kuzua maana mpya ya maneno ya Kiswahili. Pia ulitusaidia kufahamu athari ya metonimu na sitiari katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili. Kimsingi polisemi ni leksimu moja yenye maana nyingi ambazo zinahusiana kwa njia moja au nyingine (Chacha na Pendo, 2019). Pia kuna njia zingine za uzuaji wa polisemi kwa mfano ukopaji, mabadiliko katika matumizi ya neno, na ufasiri mpya wa homonimu. Kuna baadhi ya wataalamu ambao wamezungumzia polisemia kama vile Mwendamseke (2016) aliyeandika makala kuhusu uelekeo wa maana za kipolisemia katika msamiati wa Kiswahili. Naye Gaichu (2013) alishughulikia uchunguzi wa sitiari dhanifu katika methali za Kiswahili. Utafiti huu wa sitiari na metonimu ndio usiodhihirika moja kwa moja. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: Kubainisha polisemi ambazo zimeundwa kutokana na sitiari na metonimu katika Kiswahili, kuainisha polisemi katika lugha ya Kiswahili, kudhihirisha mchakato ambao sitiari na metonimu hupitia kuunda polisemi katika Kiswahili. Nadharia ya semantiki tambuzi iliongoza utafiti huu. Nadharia hii ni sehemu ya nadharia ya Isimu Tambuzi ambayo ina misingi katika saikolojia tambuzi (Vyvyan & Greens, 2006). Data husika ilikusanywa maktabani. Maktabani, maneno ambayo ni polisemi na yameundwa kwa sitiari na metonimu kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2018) yalikusanywa. Mbinu ya usampulishaji wa kimaksudi ilitumika katika uteuzi wa sampuli. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo na majedwali ili iweze kueleweka. Kutokana na data ya utafiti huu, imebainika kuwa kuna baadhi ya polisemi zilizojitokeza ndani ya homonimu. Kwa mfano, tata2 na chuo1. Pia, imebainika kuwa data hiyo ilikuwa na polisemi za majina ya wanyama, wadudu na ndege. Hata hivyo, imebainika kuwa sitiari huwa na maeneo mawili ya ufahamu: moja ni ile inayotokana na maumbo tunayoyaona na nyingine ni ile ya kidhahania. Hiyo ya kwanza inaitwa eneo chasili na ya pili eneo lengwa. Kwa mfano, sitiari “Maria ni chui” maumbo tunayoyaona (eneo chasili) ni Maria na chui na maumbo ya kidhahania (eneo lengwa) ni ukali. Kwa upande mwingine, imebainika kuwa metonimu huwa na eneo moja. Kwa mfano, leksimu kiti eneo lake ni uongozi. Tafiti zingine zinaweza kufanywa kuhusu mchango wa mbinu zingine za lugha kama vile tashibihi, lakabu na jazanda yaani; namna ambavyo mbinu hizo zinaweza kuchangia pia katika kuunda polisemia katika Kiswahili.
  • Item
    Uanuwai wa Kimofolojia Katika Tafsiri za Nomino za Pekee Katika Biblia
    (Kenyatta University, 2023-06) Mwangi, Simon Kiarie; Leonard Chacha; Miriam Osore
    Abstract
  • Item
    Mchango Wa Kiswahili Katika Mofofonolojia Ya Nominomkopo Za Kibukusu
    (Kenyatta University, 2023-06) Juma, James Tom; Jacktone Okello Onyango
    Abstract
  • Item
    Changamoto Katika Ujifunzaji Fonolojia Arudhi ya Kiswahili Katika Shule za Upili, Gatuzi la Homabay, Kenya
    (Kenyatta University, 2023-05) ‘Wagabi, Wanga James; Jacktone O. Onyango
    Abstract
  • Item
    Usawiri wa Waathiriwa wa Ghasia za Kisiasa na Kijamii katika Riwaya Teule za Kiswahili
    (Kenyatta University, 2023-11) Mogondo, Erickson Okora; Beth N. Mutugu.
    Abstract
  • Item
    Uchanganuzi wa Makosa ya Kisarufi Katika Insha za Kiswaiiele Miongoni Mwa Wanafunzi wa Shule za Upili Katika Kaunti ya Nakuru Kenya
    (Kenyatta University, 2023-11) KIGIA, JOHN MWAURA; Babusa Hamisi; Miima Florence
    Abstract
  • Item
    Uchanganuzi wa Nyimbo za Jaguar (Charles Njagua Kanyi) na Willy Paul (Wilson Abubakar Radido)
    (Kenyatta University, 2023-06) Ng'ata, John Gituhu; King'ei, Kitula Osore, Miriam; Richard. M. Wafula
  • Item
    Uchanganuzi wa Nyimbo za Jaguar (Charles Njagua Kanyi) na Willy Paul (Wilson Abubakar Radido)
    (Kenyatta University, 2023-06) Ng'ata, John Gituhu; King'ei, Kitula Osore, Miriam; Richard. M. Wafula
  • Item
    Mbinu za Kujllmarisha na Kujidumisha Kilugha kwa Wambeere
    (CHAKAMA, 2015) Kaviti, Fridah M; Ngugi, Pamela
  • Item
    Isimu Ikolojia ya Leksimu za Miti Shamba Katika Lugha ya Kiswahili
    (Kenyatta University, 2023-11) Karoli, Bonareri Nelly; Leonard Mwita Chacha
    This study examined the ecology of herbal lexicon in Swahili language. Ecology is a branch that explores debates that are relevant or inappropriate for the environment. Language and culture are inseparable. Language patterns influence the way humans think about their environment and that leads to actions that are the heart of the ecological challenges they face. In this project, we analysed how herbal lexicons are considered as signs of environmental conservation techniques in the ecosystem. The project aimed to achieve these goals: to identify how the herbal lexicons could be classified in the Swahili language, to examine how the herbal lexicons reflected environmental conservation and to demonstrate the relationship between the herbal lexicons and the Swahili culture. This study was guided by the ecosemiotic theory that helped us understand that what is identified as an impact on ecology often has semiotic factors and differences in interpreting signs or vocabulary. Data was collected by the interview technique from the Swahili speakers found in Mvita. We noted that there are herbal lexicons like mpambamwitu that the Swahili used to show the beauty of their forests by bringing a natural image and a unique look. In addition, we found that the Swahili people interacted with the herbal trees in their day-to-day life such as mwarubaini. This culture was seen as a system of symbols that the Swahili used to communicate and bring meaning to their environment. How we choose our vocabulary while communicating about the environment can change the way the community views their environment. This study suggests that we should recognize the value of the natural environment and incorporate it into our policies and systems. By recognizing that our environment is our biggest ally then we will use it in a sustainable way for future generations. 1
  • Item
    Athari za Ekegusii Katika Matumizi ya Kiimbo cha Kiswahili Miongoni mwa Wanafunzi wa Shule za Upili Kaunti ya Kisii, Kenya
    (Kenyatta University, 2023-11) Nyougo, Christine; Peter Githinji
    Utafiti huu ulichunguza matumizi ya kiimbo cha Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wanaozungumza Ekegusii kama lugha ya kwanza. Shule tatu zilihusishwa katika utafiti huu: Shule ya upili ya Senior Chief Musa Nyandusi, Nyamondo na Nyabisia. Malengo ya utafiti huu yalikuwa: Kutathmini utamkaji na ufasili wa kiimbo cha Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wanaozungumza Ekegusii kama lugha ya kwanza, kuchunguza jinsi viarudhi vya lugha ya Ekegusii vinavyoathiri kiimbo cha Kiswahili. Kutathmini jinsi usuli wa lugha na tajriba ya wanafunzi inavyochangia matumizi bora ya kiimbo katika uzungumzaji wa Kiswahili. Ili kuafiki madhumuni haya, maswali yafuatayo yalitumiwa: Je, wazungumzaji wa Ekegusii hufasili vipi kiimbo cha Kiswahili sanifu? Viarudhi vingine vya Ekegusii huathiri kiimbo cha Kiswahili vipi? Usuli na tajriba ya wanafunzi huchangia vipi katika matumizi bora ya kiimbo cha Kiswahili? Nadharia ya ujifunzaji wa kiimbo cha lugha ya pili iliyoasisiwa na Mennen (2015) ilitumiwa katika kuchunguza matumizi ya kiimbo. Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Maktabani ulihusu kusoma matini, vitabu, tasnifu, majarida na makala mtandaoni kuhusu kiimbo. Nyanjani ulijumuisha matumizi ya hojaji funge na wazi katika kupata tathmini ya wanafunzi ya sampuli ya data waliyopewa na mtafiti. Vilevile, mbinu ya mahojiano ambayo yalirekodiwa ilitumika kwa walimu wanaofunza Kiswahili. Pia, uchunzaji wa kushiriki ulitumiwa. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo, majedwali, michoro na chati. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa lugha ya Ekegusii huathiri matumizi ya kiimbo sahihi cha Kiswahili. Wazungumzaji wa Ekegusii walionyesha athari katika usomaji na ufasili wa kiimbo cha Kiswahili. Ilibainika kuwa viarudhi vingine vya Ekegusii huathiri matumizi ya kiimbo cha Kiswahili. Utafiti ulithibitisha kuwa jinsia huchangia katika matumizi sahihi ya kiimbo ambapo ilidhihirika kuwa jinsia ya kike hutumia kiimbo sahihi katika mazingira rasmi ikilinganishwa na jinsia ya kiume. Tajriba pia huchangia kiimbo sahihi pale ambapo wanafunzi ambao wamekuwa shuleni kwa muda mrefu huzungumza kwa kiimbo bora. Vifaa vya kisasa pia huchangia kuboresha matumizi ya kiimbo sahihi cha Kiswahili. Tunapendekeza walimu wakuze matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji wa kiimbo cha Kiswahili, kuwepo sheria shuleni kuhusu matumizi ya Kiswahili katika mazingira rasmi na ufundishaji wa kiimbo utiliwe maanani kuanzia viwango vya chini vya elimu.
  • Item
    Tathmini ya Kiwango cha Ubadilishaji Msimbo Katika Vituo vya Moduli ya Masafa ya Mulembe na Moduli ya Masafa ya Sulwe
    (2023-11) Mabonga, Ivy; ; Peter Githinji
    Utafiti huu ulijikita katika kutathmini kiwango cha ubadilishaji msimbo katika vituo viwili vya Royal Media Services ambavyo ni vya moduli ya masafa ya Mulembe na Sulwe. Katika kituo cha Sulwe, lahaja ya Kibukusu imechukuwa nafasi ya lugha msingi huku lahaja za Kiluyia haswa Kikabrasi, Kiwanga, Kikhayo na lahaja zingine zikichukuwa nafasi ya lugha msingi katika kituo cha Mulembe . Ijapokuwa lugha hizo zinatumiwa katika mahojiano, matangazo na mambo mengine ya utangazaji wakati mwingine wageni na watangazaji hutumia Kiswahili. Kwa hivyo, utafiti huu uliangazia matumizi ya Kiswahili katika vituo hivyo ili kuweza kuchunguza kiwango chake katika ubadilishaji msimbo kupitia tathmini ya vichocheo vya ubadilishaji msimbo, ubainishaji wa jinsi ubadilishaji msimbo hutokea na uchanganuzi wa athari zinazotokana na ubadilishaji msimbo zinazojidhihirisha katika jamii hiyo. Kupitia malengo hayo, kiwango cha ubadilishaji msimbo kiliweza kutathminiwa kwa kuchunguza matumizi ya Kiswahili ambayo yalituwezesha kupima kiwango cha matumizi yake vituoni humo. Nadharia ya Maki iliyoasisiswa na Myers –Scotton (1993) ndio iliyoongoza utafiti huu. Nadharia hii ilijikita katika dhana za kutia na kutoa maki zilizowasilisha upya au ukawaida. Mkabala huu ulilinganisha lugha kadhaa ili kuangazia sababu zinazopelekea lugha moja kuchaguliwa kwa minajili ya matumizi miongoni mwa nyingine. Dhana ya kutia na kutoa maki hutumika katika nadharia hii kujenga msingi wa kubainisha vichocheo vya kisaikolojia na vya kijamii katika uchanganuzi wa msimbo. Mbali na hayo, nadharia hii inaeleza kuhusu maswala mengine kama vile ustadi au uwezo wa kuwasiliana, ambayo huchanganua maswala ya muktadha na ustadi.Mengine ni Haki na Majukumu ambayo hudhihirisha mazingira ya kutoa au kutia maki katika msimbo. Utafiti huu ulifanyika maktabani mno kwa kusoma tafiti na vitabu vilivyoandikwa kuhusu mada ambavyo vilikuwa nguzo ya utafiti huu. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika vituo teule kupitia usikilizaji wa baadhi ya vipindi na pia kuwahoji na wanahabari wa vituo hivyo. Data iliwasilishwa kwa njia ya kijarabati na kimaelezo, ili kuelezea na kuchanganua kikamilifu semi zenye ubadilishaji msimbo. Utafiti huu utawafaidi watafiti tathmini matumizi ya lugha katika jamii yenye wingi lugha iliyowekewa mipaka au huru. Kupitia ubainishaji wa athari ya Kiswahili kwa Kiluyia na vichocheo vilivyobainishwa, wanaisimu jamii wataweza kupima na kuchanganua mtagusano wa lugha kiidadi na kimaelezo.
  • Item
    Athari za Katama Mkangi kwa John Habwe: Mfano Kutoka kwa Riwaya Teule za Mafuta (1984) na Cheche za Moto (2008)
    (Kenyatta University, 2023-11) Musyoka, Kalingwa Felix; Titus M. Kaui
    Utafiti huu unashughulikia athari za Katama Mkangi kwa John Habwe kwa kujikita katika riwaya teule za Kiswahili za Mafuta (1984) na Cheche za Moto (2008). Utanzu wa riwaya ya Kiswahili umeendelea kupanuka kimaudhui na kifani kutokana na juhudi za watunzi mbalimbali kama vile Katama Mkangi na John Habwe. Japo tafiti za awali zimetafitia suala la mwingiliano matini, tafiti nyingi zimejikita katika kazi za mtunzi mmoja.Utafiti wa kina ulihitajika kuchunguza namna utunzi wa Mafuta (1984) ulivyoathiri John Habwe alipoitunga riwaya yake ya Cheche za Moto (2008). Katama Mkangi aliandika riwaya ya Mafuta katika wakati wa chama kimoja cha kisiasa ambapo uhuru wa kujieleza ulikuwa umebanwa sana. Habwe ameandika kazi yake ya Cheche za Moto katika mazingira yaleyale, miaka ishirini na minne baadaye. Wakati wa utunzi wa Cheche za Moto, uhuru wa kujieleza ulikuwa umepanuliwa. Kwa hivyo, amekwepa mtindo wa kimajazi alioutumia Mkangi na kuyaangazia masuala anayoyaibua Mkangi kwa njia wazi. Utafiti huu uliongozwa na malengo matatu: kwanza, ni kufafanua namna mwangwi wa maudhui ya riwaya ya Mafuta unavyojitokeza katika riwaya ya Cheche za Moto, kubainisha athari za usawiri wa wahusika wa Katama Mkangi kwa John Habwe, na mwisho, kuonyesha athari za kimtindo za Katama Mkangi kwa John Habwe. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya mwingiliano matini iliyoasisiwa na Julia Kristeva (1969). Mihimili mikuu ya nadharia hii iliyoongoza utafiti huu ni pamoja na: hakuna matini ya fasihi yenye sifa za pekee, matini hubainisha sifa mbalimbali za matini tangulizi, na mwisho, matini ya baadaye huweza kufafanua dhana fulani kutoka matini tangulizi kwa njia inayoeleweka. Nadharia hii ya mwingiliano matini ilisaidia pakubwa kuonyesha namna kazi ya awali, Mafuta (1984) ilivyomwathiri John Habwe katika utunzi wa Cheche za Moto (2008), kimaudhui na kifani. Riwaya ziliteuliwa kimakusudi ili kupata sampuli faafu yenye data ya kujaza pengo la utafiti. Data ilikusanywa kupitia kwa usomaji wa maktabani na vilevile kusakura mitandaoni kuhusu vipengele vya mwingiliano matini katika riwaya ya Kiswahili. Data hii imewasilishwa kwa njia ya kimaelezo. Utafiti huu unatarajiwa kutoa mchango katika uhakiki wa utanzu wa riwaya ya Kiswahili, hususan kuhusu kipengele cha kuathiriana baina ya watunzi wa riwaya za Kiswahili.
  • Item
    Uhusika katika vichwa vya habari za siasa kwenye gazeti la taifa leo (2017-2019)
    (Kenyatta University, 2021-12) Mutuku, Fidelis Kioko; Jacktone Onyango; Leonard Chacha
    Utafiti huu umechambua uhusika katika vichwa vya habari za siasa kwenye gazeti la Taifa Leo. Matoleo ya magazeti teule ya Taifa Leo yaliyochapishwa kati ya mwaka wa 2017 na 2019 yameongoza uchambuzi huu. Ili kufanikisha uchambuzi wa mantiki ya mada hii, nadharia ya uhusika inayoafiki malengo ya utafiti huu imetumikizwa. Malengo ya utafiti huu ni pamoja na; kudhihirisha na kuchambua dhana mbalimbali za uhusika katika vichwa vya habari za siasa kwenye gazeti la Taifa Leo, kutofautisha majukumu na maumbo ya uhusika katika vichwa vya habari husika na kubainisha umuhimu wa sarufi uhusika katika taaluma ya isimu. Uhusika ni kategoria ya kisarufi ambayo huonyesha uhusiano wa viambajengo katika tungo. Aidha, uamilifu wa kila kiambajengo katika tungo na athari ya kila kiambajengo kwa viambajengo vingine huonyeshwa. Nyenzo ya data msingi ya utafiti huu ni maktaba. Mbinu ya upekuzi wa yaliyomo ilitumika katika ukusanyaji wa data hii, ambapo machapisho mbalimbali ya gazeti la Taifa Leo (2017-2019) yanayotawaliwa na kigezo cha siasa yalipitiwa na mtafiti kwa umakinifu kabla ya kufanywa data teule. Katika uwasilishi wa data, maelezo yameandamana na michoroti ya kisintaksia pamoja na majedwali. Kijumla, mpangilio wa kazi hii umewasilishwa kwenye sura tano. Sura ya kwanza ni utangulizi wa utafiti ulioshughulikia suala la utafiti, malengo ya utafiti, upeo na mipaka ya utafiti, misingi ya nadharia na mbinu za utafiti. Katika sura ya pili, mtafiti amebaini kuwa, miundo mbalimbali ya vichwa vya habari za siasa zina aina zifuatazo za uhusika; uhusika kiima, mahali, yambwa, tendea, tokeo na ala. Vichwa hivi vya habari huwa na kategoria mbili za uwakilisho, nazo ni; muundo ndani na muundo nje. Kwenye sura ya tatu, mtafiti ameweka wazi tofauti iliyoko kati ya majukumu na maumbo ya uhusika. Mtafiti amebainisha kuwa, majukumu ya uhusika ni dhahania ilhali maumbo yake huonekana. Umuhimu mbalimbali wa sarufi uhusika katika taaluma ya isimu umeelezwa ipasavyo katika sura ya nne. Baadhi ya umuhimu huo ni kurahisisha uelewaji wa sentensi katika lugha, kutambua dhima ya maneno katika tungo na kadhalika. Hatimaye sura ya tano imeangazia matokeo, changamoto na mapendekezo ya utafiti. Mtafiti ameeleza matokeo ya utafiti huu kama ifuatavyo; Kiswahili hakina maumbo dhahiri ya uhusika isipokuwa viwakilishi vya nafsi ya pili na tatu, umoja na wingi. Hata hivyo, vichwa vya habari ambavyo muundo wake hauruhusu uwepo wa viwakilishi hivi, viwakilishi ....
  • Item
    Tathmini ya Kiwango cha Ubadilishaji Msimbo katika Vituo vya Moduli ya Masafa ya Mulembe na Moduli ya Masafa ya Sulwe
    (Kenyatta University, 2023) Mabonga, Ivy; Peter Githinji
    Utafiti huu ulijikita katika kutathmini kiwango cha ubadilishaji msimbo katika vituo viwili vya Royal Media Services ambavyo ni vya moduli ya masafa ya Mulembe na Sulwe. Katika kituo cha Sulwe, lahaja ya Lubukusu imechukuwa nafasi ya lugha msingi huku lahaja za Kiluhya haswa Lukabrasi, Luwanga, Lukhayo na lahaja zingine zikichukuwa nafasi ya lugha msingi katika kituo cha Mulembe. Ijapokuwa lugha hizo zinatumiwa katika mahojiano, matangazo na mambo mengine ya utangazaji wakati mwingine wageni na watangazaji hutumia Kiswahili. Kwa hivyo, utafiti huu uliangazia matumizi ya Kiswahili katika vituo hivyo ili kuweza kutathmini kiwango chake katika ubadilishaji msimbo kupitia tathmini ya vichocheo vya ubadilishaji msimbo, ubainishaji wa jinsi ubadilishaji msimbo hutokea na uchanganuzi wa athari zinazotokana na ubadilishaji msimbo zinazojidhihirisha katika jamii hiyo. Kupitia malengo hayo, kiwango cha ubadilishaji msimbo kiliweza kutathminiwa kwa kuchunguza matumizi ya Kiswahili ambayo yalituwezesha kupima kiwango cha matumizi yake vituoni humo.Nadharia ya Maki iliyoasisiswa na Myers –Scotton (1993) ndio iliyoongoza utafiti huu. Nadharia hii ilijikita katika dhana za kutia na kutoa maki zilizowasilisha upya au ukawaida. Mkabala huu ulilinganisha lugha kadhaa ili kuangazia sababu zinazopelekea lugha moja kuchaguliwa kwa minajili ya matumizi miongoni mwa nyingine. Dhana ya kutia na kutoa maki hutumika katika nadharia hii kujenga msingi wa kubainisha vichocheo vya kisaikolojia na vya kijamii katika kuchanganuzi wa msimbo. Mbali na hayo, nadharia hii inaelezea maswala mengine kama vile ustadi au uwezo wa kuwasiliana, ambayo huchanganua maswala ya muktadha na ustadi.Mengine ni haki na majukumu ambayo hudhihirisha mazingira ya kutoa au kutia maki katika msimbo. Utafiti huu ulifanyika maktabani mno kwa kusoma tafiti na vitabu vilivyoandikwa kuhusu mada ambavyo vilikuwa nguzo ya utafiti huu. Utafiti wa nyanjani ulifanyika katika vituo teule kupitia usikilizaji wa baadhi ya vipindi na mahojiano na wanahabari wa vituo hivyo. Data iliwasilishwa kwa njia ya kijarabati na kimaelezo, ili kuelezea na kuchanganua kikamilifu semi zenye ubadilishaji msimbo. Utafiti huu utawafaidi watafiti tathmini ya matumizi ya lugha katika jamii yenye wingi lugha iliyowekewa mipaka au huru. Kupitia ubainishaji wa athari ya Kiswahili kwa Kiluhya na vichocheo vilivyobainishwa, wanaisimu jamii wataweza kupima na kuchanganua mtagusano wa lugha kiidadi na kimaelezo.
  • Item
    Utata kama Chanzo cha Taharuki Katika Vichwa vya Habari Katika Gazeti la Taifa Leo
    (Kenyatta University, 2023) Njeru, Joyce Wanjiru; leonard chacha mwita
    Utafiti huu ulidhamiria kutathmini utata kama chanzo cha taharuki katika vichwa vya habari katika gazeti la Taifa Leo. Pia, utafiti huu ulilenga kuweka wazi athari ya utata uliopo katika vichwa vya habari kwa wasomaji wa gazeti la Taifa Leo. Gazeti ni njia mwafaka na muhimu ya kuwasilisha ujumbe kama vile masuala nyeti, sera za serikali, masuala ibuka na ujumbe mwingine wowote. Wasomaji ndio wapokezi wa habari hizo. Hivyo, ni muhimu kuchunguza athari ya utata huo kwa wasomaji kwani ndio walengwa. Nia ya wahariri wa gazeti ni kupitisha ujumbe. Vichwa vya habari ni sehemu muhimu ya kuwapa wasomaji msukumo wa kusoma habari zilizopo katika gazeti na hivyo, vichwa vinapaswa kuibua taharuki ili kuvutia wasomaji wasome ujumbe huo. Hivyo basi, utafiti huu ulilenga kuchunguza iwapo vichwa vya habari vyenye utata vinaibua taharuki katika gazeti la Taifa Leo. Taharuki ilichukuliwa kuwa, hamu ya kutaka kujua yanayofafanuliwa katika habari baada ya kusoma kichwa fulani cha habari, yaani msukumo ambao huchochea wasomaji kutaka kujua kinachozungumziwa katika habari inayofuata. Pia, utafiti huu uliweza kuweka bayana maoni ya wasomaji wa gazeti la Taifa Leo kuhusiana na utata katika vichwa vya habari. Nadharia iliyotumiwa katika utafiti huu ni nadharia ya maana kama matumizi iliyoasisiwa na Wittgenstein mwaka wa 1930 ambayo ilituelekeza kuchunguza maana ya maneno katika muktadha wa mutumizi yake. Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Maktabani, mtafiti alisoma vitabu na majarida yaliyo jadili kuhusu utata na kuchambua vichwa vya habari vyenye utata katika gazeti la Taifa Leo ili kubainisha aina mbalimbali za utata. Utata uliobainika katika data iliyokusanywa ni utata wa kileksia, utata wa kimantiki, utata wa kutafakari, utata wa kipragmantiki na utata wa kisarufi. Nyanjani, wasomaji, wahariri na waandishi wa gazeti la Taifa Leo walihojiwa ili kutathmini athari ya utata uliopo katika vichwa vya habari na iwapo utata huo huzua taharuki kwa wasomaji. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa asilimia kubwa ya wasomaji huwa na athari chanya kuhusu utata katika vichwa vya habari na vichwa hivyo huzua taharuki kwa wengi wa wasomaji wa gazeti la Taifa Leo. Hata hivyo, ilibainika kuwa wakati mwingine utata uchanganya na kupotosha ujumbe lengwa na hivyo kutozua taharuki kwa wasomaji. Hivyo, wahariri wanapaswa kuwa makini wanapoteua vichwa vya habari ili vizue taharuki. Utafiti huu utawasaidia waandishi na wahariri wa gazeti kutambua athari na maoni ya wasomaji kuhusiana na vichwa vya habari vyenye utata na mchango wa utata katika kuzua taharuki. Hili litawasaidia kuwasilisha ujumbe ipasavyo wakitilia maanani wasomaji wa gazeti. Pia, utafiti huu utapanua fikra za wasomaji kuhusu utata katika vichwa vya habari kwa kuwa uliweza kuchambua utata kwa kina.
  • Item
    Maendeleo ya Tawasifu ya Kiswahili tangu Karne ya 19 hadi 21
    (Kenyatta University, 2023) Wabomba, Eric W.; Richard Wafula; Pamela M.Ngugi
    Utafiti huu umechanganua tawasifu tatu zilizoandikwa katika karne tatu tofauti ambazo ni: Tawasifu ya Tippu Tip iliyoandikwa karne ya 19 na kuhaririwa na Whiteley (1958), ya Shaaban Robert (1969) ya Maisha yangu na Baada ya miaka Hamsini, ya karne ya 20, na tawasifu ya Ken Walibora (2014) ya Nasikia sauti ya Mama, ambayo iliandikwa katika karne ya 21. Utafiti huu ulikuwa na malengo matatu ambayo ni: Kuchanganua vipengele vya uhalisia na ubunifu katika tawasifu ya Tippu Tip iliyohaririwa na Whiteley (1958); Kuchanganua vipengele vya uhalisia na ubunifu katika tawasifu ya Shaaban Robert (1969); Kuchanganua vipengele vya uhalisia na ubunifu katika tawasifu ya Ken Walibora (2014). Vipengele hivi vilichanganuliwa kwa kuangazia maudhui na mtindo wa uandishi uliotumika katika tawasifu hizi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili ambazo ni: Nadharia ya Uhalisia na nadharia ya Mtindo. Nadharia ya Uhalisia iliasisiwa na Hegel (1975 – 1979), Zola (1969) na Flaubert (1972), miongoni mwa wengine. Kwa mujibu wa nadharia ya Uhalisia, maisha ya jamii yanafaa kuwasilishwa kwa uaminifu na usahihi mkubwa. Mambo yanayoonekana katika jamii ndiyo hutiliwa mkazo. Nadharia ya Mtindo iliasisiwa na Buffon (1930) na kuendelezwa na waasisi wengine wakiwemo Wellek na Warren (1949), Coombes (1963), na Leech (1981). Nadharia hii huchunguza lugha ili kubainisha ubunifu uliomo kwenye lugha hiyo. Nadharia ya Uhalisia ilichaguliwa kuongoza utafiti huu kwa sababu, mwandishi yeyote wa tawasifu anatazamiwa kuelezea ukweli halisi kuhusu maisha yake. Kwa upande mwingine, nadharia ya Kimtindo ilichaguliwa kwa vile ambavyo tunatarajia mtunzi wa kinathari aelezee kiubunifu maisha yake akizingatia mbinu zinazoakisi ukweli, uzushi, chuku na kadhalika. Nadharia ya Uhalisia kwa upande mmoja, ilisaidia katika kuangalia viwango vya uyakinifu katika tawasifu hizi. Kwa upande mwingine, nadharia ya mtindo ilichangia katika kubainisha mtindo na ubunifu uliomo katika tawasifu hizi tatu. Mbinu za utafiti zilizotumiwa katika utafiti huu ni kusoma kwa kina, kueleza na kuchanganua vipengele vya mada. Data zilizotokana na utafiti huu zinabainisha viwango vya uhalisia na ubunifu na hivyo kuchangia pakubwa katika ujuzi wa tawasifu kama kipera cha riwaya. Watafiti wengine wanaopania kuzama katika uwanja wa tawasifu na uandishi wa kinathari kwa ujumla watafaidika kwa data za utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa muhimu katika tafiti nyingine, haswa zile zitakazonuia kushughulikia uhalisia na ubunifu, sio tu katika tawasifu ya Kiswahili, bali katika tagaa la riwaya kwa ujumla.
  • Item
    Ufungamano wa Itikadi na Propaganda Katika Tamthilia za Kithaka wa Mberia: Kifo Kisimani (2001) na Maua Kwenye Jua La Asubuhi (2004)
    (kenyatta university, 2023) Minyade, Sheril Mugaduka; jessee murithi; jessee murithi
    Utafiti huu umeonyesha ufungamano wa itikadi na propaganda katika tamthilia za Kithaka Wa Mberia: Kifo Kisimani (2001) na Maua kwenye Jua la Asubuhi (2004). Baadhi ya sababu ambazo zimechochea kufanywa kwa utafiti huu ni kuwa; suala la itikadi ni la muhimu sana kwa vile ndilo ambalo huongoza matendo ya binadamu. Pia, propaganda ina uhusiano wa karibu sana na kazi za kifasihi ambazo huwa ni chombo cha kiitikadi. Kwa hivyo, malengo ya utafiti yalikuwa kubainisha aina za itikadi katika tamthilia teule, kuonyesha aina za propaganda katika tamthilia teule na kuonyesha uhusiano kati ya itikadi na propaganda. Kwa mujibu wa Marx na Engels (1977), itikadi ni fikra zote za maoni ya wanadamu kuhusu wanayoyasema na wanayoyafikiria kuhusu dini, sheria, siasa, maadili na falsafa. Propaganda hushawishi fikra za mtu kutenda jambo kwa namna fulani. Ni ushawishi unaoratibiwa kwa malengo fiche, (Ellul, 1965). Tamthilia za Kifo Kisimani na Maua kwenye Jua la Asubuhi ziliteuliwa kimaksudi kwa sababu zina data ambayo imetumika katika kutimiza malengo ya utafiti. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Tahakiki Usemi (UTU) iliyoasisiwa na Fairclough (1989). Ni nadharia ambayo hueleza uhusiano uliopo kati ya matukio ya kiusemi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni na jinsi yanavyoathiriwa na itikadi.Nadharia teule inaangazia jinsi usemi huo huathiri matukio katika jamii. Utafiti huu ni wa kimaelezo kwa sababu uchanganuzi wa data umetekelezwa na kuwasilishwa katika maelezo ya kina. Kutokana na maelezo ya kina, itikadi ya dini, ukombozi, utawala, utamaduni, umwinyi na ubepari imebainishwa kutoka katika tamthilia teule. Data ilikusanywa kutokana na muktadha wa mazungumzo ya wahusika, usemi na matumizi yao ya lugha. Mtafiti ameonyesha aina za propaganda kama vile propaganda ya kisiasa na kijamii, wazi, siri na propaganda ya kati. Pia, utafiti umethibitisha kuwa itikadi na propaganda ni dhana mbili tofauti lakini zina uhusiano wa karibu. Diskozi zote zinaongozwa na itikadi ambapo maudhui, usemi, matumizi ya lugha na muktadha wa mazungumzo huashiria itikadi ya mhusika. Propaganda na itikadi ni masuala muhimu katika kazi za kifasihi. Hata hivyo, imebainika kuwa ili propaganda iweze kufaulu, inajiegemeza katika itikadi fulani. Pia, hakuna itikadi ambayo inaweza kufaulu bila kuwashawishi watu. Ushawishi huu ndio propaganda, na hivyo kufanya dhana hizi kuwa na uhusiano wa karibu sana. Tafiti zaidi zinaweza kufanywa katika kitengo cha itikadi ili kuchunguza wahusika wanaharakati katika tamthilia hizi. Uanaharakati unaendana moja kwa moja na itikadi ambayo huhalalisha seti za matendo zinazojitokeza katika vitendo. Utafiti huu unawawezesha wasomi na wahakiki wa kazi za kifasihi kutumia dhana ya itikadi na propaganda kama dhana mbili tofauti ambazo zina ufungamano.
  • Item
    Uchanganuzi wa Watoto Katili Katika Fasihi ya Watoto
    (2023) Nyariki, Nyariki Enock; King'ei, Kitula Osore, Miriam; Pamela M. Ngugi
    This study aimed at assessing cruel children characters in selected literature books in the youth category. It investigated and analysed the types of cruelty of these children, the reasons that contribute to their being cruel, the effects of this cruelty on other characters and how it can be managed. The following novels which target the youth audience were examined: Siku Njema by Ken Walibora (1996),Tumaini by Clara Momanyi (2006), and Lulu ya Maisha by John Habwe (2013). The study showed that although a child is usually viewed as a victim of cruelity, some children are perpetrators of cruelty and therefore the community needs to come up with ways of controlling their actions. The study found that children commit physical, verbal and emotional types of cruelty. The study was guided by the social learning theory by Bandura (1977) whose proponents include Baltes and Reese (1984) and the realism theory whose proponents include Gustav (1850), Rene Wellek (1961)and Lazaro Carreter (1970) among others. Social learning theory assisted the research in explaining how children learn by observing role models within their environment. The theory of realism assisted the research in showing how cruelity in the community is reflected by writers of literary work. The study was conducted through desktop research. Primary data was obtained by reading the novels mentioned above, dividing the data thematically and analyzing it according to the research objectives. The study compared and cross-validated the research findings with those in journals, news papers, theses, books and other online publications on the subject matter. The research findings were presented in descriptive form. Some of the strategies to address cruelty among children that the study found included reducing potential causes of cruelty in children in families, at school and in the society.The research findings will benefit authors, researchers, editors, publishers and other stakeholders of Literature in highlighting cruelity in a broader percpective of the child not only as a victim of violent situations but also as one capable of acting violently towards other members of the community. Besides, the findings could help those dealing with children issues to device best ways of curbing violent acts in children.
  • Item
    Athari za Sheng’ kwa Kiswahili Sanifu: Uchunguzi wa Kamusi ya Sheng’.
    (Kenyatta University, 2023) Muyumba, Jotham; David Kihara
    Utafiti huu ulidhamiria kutathmini athari za kamusi ya Sheng’ – English Dictionary kwa Kiswahili sanifu. Kamusi ya Sheng’ –English Dictionary (2003) iliteuliwa kama msingi wa uchunguzi huu kwa sababu ndio kamusi ya kwanza ya Sheng’ kuwahi kuchapishwa. Licha ya kamusi hii kuchapishwa katika lugha ya Kiingereza ina leksimu za Sheng’ ambazo yafaa kuchunguzwa namna zinavyoathiri Kiswahili sanifu kwa wakati wa sasa. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha maneno yaliyomo katika Sheng’- English Dictionary na katika Kiswahili sanifu. Kadhalika, utafiti huu ulinuia kueleza muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na jinsi yanavyotofautiana na Kiswahili sanifu. Mwisho, utafiti huu ulidhamiria kueleza sababu za utofauti wa muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na kueleza athari zake kwa Kiswahili sanifu. Nadharia ya utafiti ilikuwa Nadharia ya Fonolojia Boreshi ambayo inapatikana katika mtazamo mpana wa Nadharia Boreshi iliyoasisiwa na Alan Prince na Paul Smolensky (1991). Hii ni nadharia inayochunguza hatua za ukuaji wa msamiati kutoka hali ghafi hadi ukubalifu wake kupitia kwa vizuizi tofauti. Mahali pa utafiti palikuwa maktabani na mtandaoni. Mbinu ya uchunguzi ikawa kupitia kusikiliza wazungumzaji wa Sheng’ na kusoma makala mbalimbali kuhusu mada hii. Data ilikusanywa kupitia kwa kuchunguza maneno na vidahizo vya maneno kutoka kamusi ya Sheng’ – English Dictionary (2003). Iliaminika kuwa kamusi hii ingetoa sampuli ya maneno mahsusi ya Sheng’ ambayo muundo wake huathiri matumizi katika Kiswahili sanifu kwenye jamii ya kisasa. Uchanganuzi wa maelezo ulitegemea mtazamo wa Fonolojia Boreshi katika nadharia ya fonolojia inayoangazia sarufi zalishi. Katika mtazamo huu, uambishaji wa maneno uliangaziwa na jinsi uundaji huo hutawaliwa na vizuizi mbalimbali na sheria za fonolojia. Kadhalika nadharia ya Fonolojia Boreshi ilitumika kueleza michakato ya namna wazungumzaji wa Sheng’ hubuni leksimu mbalimbali katika mawasiliano. Uwasilishaji wa data ulikuwa kupitia kwa maelezo ya kina, michoro na jedwali. Matokeo ya utafiti huu ni kuwa: maneno yanayopatikana katika Sheng’ – English Dictionary na Kiswahili sanifu yalibainishwa. Pia, muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na namna yanavyotofautiana na Kiswahili sanifu ulielezwa. Kadhalika, sababu zinazochangia utofauti wa muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na Kiswahili sanifu zilielezwa. Uchunguzi huu ulidhamiria kuchangia usomi wa Kiswahili kwa kuweka wazi athari za Sheng’ katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili kimsamiati. Kadhalika, utafiti huu utawasaidia wanafunzi kuweka mipaka bayana kati ya msimbo wa Sheng’ na lugha ya Kiswahili sanifu.