MST-Department of Kiswahili and African Languages
Permanent URI for this collection
Browse
Recent Submissions
Item Majazi na Stiari katika Riwaya ya Dunia Yao na Nyuso za Mwanamke(Kenyatta University, 2024-12) Mathuku, JosephUtafiti huu ulichunguza matumizi ya majazi na stiari katika riwaya mbili teule za Said Ahmed Mohamed nazo ni Dunia Yao (2006) na Nyuso za Mwanamke (2010). Utafiti huu ulilenga kubaini majazi na stiari katika kazi teule, nafasi ya majazi na stiari katika kuwasawiri wahusika na kuonyesha jinsi mtunzi ametumia tamathali hizi kuibua maudhui. Utafiti huu ulikuwa wa kimaelezo na wa maktabani. Uteuzi wa sampuli ulikuwa wa kimakusudi ukilenga riwaya za Said Ahmed Mohamed nazo ni Dunia Yao (2006) na Nyuso za Mwanamke (2010). Ukusanyaji wa data ulihusisha usomaji wa kina wa riwaya teule ili kupata data inayokusudiwa. Hizi ni riwaya ambazo zimesheheni matumizi ya majazi na stiari. Data ilichanganuliwa kwa kuongozwa na malengo ya utafiti pamoja na mihimili ya nadharia ya Mtindo na ile ya Matumizi ya Stiari. Nadharia ya Mtindo inashikilia kuwa kazi za kifasihi haziwezi kuibuliwa bila matumizi ya lugha nayo nadharia ya Matumizi ya Stiari hushikilia kuwa ili kuelewa dhana moja ya kistiari yafaa tuilinganishe na nyingine iliyo na sifa zile zile zinazorejelewa. Uwasilishaji wa data hiyo ulikuwa wa kimaelezo. Riwaya ya Dunia Yao (2006) na ile ya Nyuso za Mwanamke (2010) tulizozitafitia ziliandikwa mwanzo mwanzo wa Karne ya 21 na zilidhihirisha mkondo mpya wa kutunga kazi za kifasihi (ule wa usasa baadaye). Riwaya hizi zilisheheni matumizi mapya na ya kipekee ya majazi na stiari ambapo uwasilishaji wa uhalisia na usawiri wa wahusika sasa haufanywi kwa kufuata mkondo wa hurafa kama hapo awali bali unahusisha matumizi mapya ya majazi na stiari ambapo hadithi, wahusika, matukio na mandhari huweza kufasiriwa au kusomwa ili ziweze kuleta zaidi ya kiwango kimoja cha maana. Utafiti huu utawafaa wahakiki wa riwaya ya Kiswahili, wasomi na watunzi wa kazi za kifasihi kuona namna waandishi wa tungo za kifasihi wa Karne hii ya 21 wanavyotumia tamathali za usemi kwa njia ya kipekee kuwasilisha uhalisia.Item Uchanganuzi Linganishi wa Matini ya Hotuba za Kisiasa Kuhusu Ufisadi Kuanzia Mwaka 2015 Hadi 2020(Kenyatta University, 2025-06) Mworeh, Felix Shimenga; King'ei, Kitula Osore, MiriamHotuba ni chombo muhimu kinachotumiwa na wanasiasa kuwasilisha sera zao, itikadi na hata kukemea maovu yanayotendeka katika jamii. Nchini Kenya, suala la ufisadi ni mojawapo ya maovu yanayotekelezwa na baadhi ya viongozi na wananchi. Kwa sababu hii, wanasiasa wengi huliangazia suala hili katika hotuba zao kwa umma kama mojawapo ya mikakati ya kuupiga vita ufisadi. Wao hutumia lugha kwa njia ya kipekee wanapoangazia suala hili hususan vita dhidi yake. Hii basi ndiyo sababu utafiti huu ulilenga kuchanganua na kulinganisha matini ya hotuba za kisiasa zinazoangazia suala la ufisadi nchini Kenya. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Usemi Hakiki (UUH) iliyoasisiwa na Fairclough katika kuchanganua hotuba sita za viongozi wawili wa kisiasa wa nchi ya Kenya kuhusu ufisadi ili kuchanganua na kulinganisha namna matini ya hotuba za kisiasa yanavyoshughulikia suala la ufisadi, kubainisha athari za hotuba hizi kwa wananchi na kisha kubaini mielekeo ya wananchi kuhusu hotuba hizi. Usampulishaji wa kimakusudi ulitumiwa kuwachagua wasailiwa na pia viongozi wa kisiasa ambao matini za hotuba zao zilichanganuliwa na kulinganishwa. Wanasiasa teule ni wale ambao wameliangazia suala hili la ufisadi kwa kina, hivyo basi hotuba zao ni faafu katika utafiti huu. Ili kupata matini za hotuba za kisiasa ambazo zilitumiwa kama data katika utafiti huu, mtafiti alikusanya video kutoka mtandao wa “YouTube”. Data nyingine pia ilikusanywa nyanjani kupitia hojaji funge ya likati na hojaji wazi ili kubaini athari na mielekeo ya wananchi wa Kenya kuhusu hotuba za kisiasa zinazoangazia suala la ufisadi. Mtafiti alizisikiliza na kuzinukuu hotuba teule kisha kuchanganua na kulinganisha matini zake. Aidha, data ilichanganuliwa na kulinganishwa kwa kutumia majedwali, takwimu na maelezo na kisha matokeo yake kuwasilishwa vilevile kwa kutumia maelezo, majedwali na takwimu. Matokeo ya utafiti huu yatawapa wananchi ama matumaini kuwa hotuba za kisiasa zinatekeleza dhima kuu katika vita dhidi ya ufisadi au ni gumzo tupu. Utafiti huu pia utachangia katika taaluma ya uchanganuzi matini ya hotuba za kisiasa zinazolenga maudhui teule kwa kutumia nadharia ya Uchanganuzi Usemi Hakiki.Item Kanuni za Lugha Zinavyoathiri Somo la Kiswahili Katika Shule za Upili: Mfano za Kaunti ya Busia(Kenyatta University, 2025-04) Osodo, Elizabeth Auma; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulishughulikia mielekeo ya wanafunzi na walimu wa shule za upili katika Kaunti ya Busia kuhusu kanuni za lugha shuleni na namna kanuni hizi zinavyoathiri somo la Kiswahili. Utafiti huu ulichunguza na kuhakiki kanuni za lugha katika shule za upili. Aidha ulibaini mielekeo ya wanafunzi na walimu kuhusu kanuni za lugha shuleni na athari yake kwa somo la Kiswahili. Malengo matatu yalioongoza utafiti huu ni: Kueleza kanuni za lugha shuleni, kuchunguza mielekeo ya wanafunzi na walimu kuhusu kanuni za lugha shuleni na kufafanua athari za kanuni za lugha shuleni kwa somo la Kiswahili katika shule zilizo Kaunti ya Busia.Utafiti huu ulitumia nadharia mbili katika uchanganuzi wa data. Kwanza, nadharia ya Saikolojia ya jamii ya Vitendo Vilivyofikiriwa ya Ajzen na Fishbein (1980). Nadharia hii inasema kuwa, binadamu huwa na mtazamo kubalifu kuhusu jambo ambalo litamnufaisha na kuwa na mwelekeo hasi kwa jambo ambalo halina manufaa kwake. Nadharia hii ilitumika kubainisha mielekeo ya walimu na wanafunzi kuhusu kanuni za lugha za shule. Nadharia hii haingeweza kuhakiki kanuni za lugha za shule na athari yake kwa somo la Kiswahili kwa kukosa vigezo vya kuchanganua data hii. Kwa hivyo, nadharia ya pili ambayo ni ya Kijumuia na Kibinadamu ilioasisiwa na Richards na Rodgers (1995) ilitumika. Nadharia hii inasema kuwa, mazingira yenye usalama na utu kwa mwanafunzi humwathiri anapojifunza lugha ya pili. Ili kufanikisha malengo ya utafiti, wanafunzi na walimu kutoka shule za upili saba zenye viwango vya Kitaifa, Zaidi ya Kaunti na Kaunti ziliteuliwa. Walimu na wanafunzi walijaza hojaji likati na wanafunzi kushiriki katika mjadala elekezi wa makundi. Utafiti huu ulihusisha wanafunzi 560 na walimu saba wa somo la Kiswahili ambao pia ni wakuu wa idara ya Kiswahili. Mtafiti pia alifanya mahojiano na walimu wakuu kwa kila shule kuhusu kanuni za lugha zilizoteuliwa. Utafiti uliteua shule tatu za wasichana za bweni, tatu za wavulana za bweni na shule moja ya mseto ya kutwa. Utafiti huu ulifanywa nyanjani na maktabani. Vifaa tofauti vilitumiwa nyanjani, hojaji likati ilitumika ili kubainisha mielekeo ya walimu na wanafunzi kuhusu kanuni za lugha za shule. Mjadala elekezi wa makundi ulitumika kubainisha sababu ya mielekeo chanya au hasi na manufaa ya kanuni za lugha za shule kwa wanafunzi. Mbinu ya uchunzaji ilitumika kwa kutazama mabango yaliyo shuleni na kuchunguza namna mijadala kwa lugha ya Kiswahili ilivyoendeshwa. Utafiti wa maktabani ulifanywa kwa kusoma kazi za waandishi mbalimbali zinazohusu sera ya lugha kwa jumla, kanuni za lugha shuleni pamoja na mielekeo yao. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kuainisha mada tofauti tofauti. Njia ya maelezo ilitumika kuwasilisha data kwa kiasi kikubwa. Picha, majedwali na michoro pia ilitumika. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa, shule tofauti zina kanuni za lugha tofauti na utekelezaji wake pia ni tofauti. Kanuni hizi ni kama lugha ya mawasiliano katika mazingira ya shule, siku za Kiswahili, mabango na maandishi katika mazingira ya shule, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mijadala, shughuli za idara ya Kiswahili kama makongamano, usomaji wa vitabu na magazeti pamoja na vyama vya Kiswahili. Ilibainika kuwa, wanafunzi na walimu wana mielekeo chanya kwa kanuni za lugha za shule ambazo zinaimarisha matokeo ya mtihani katika somo la Kiswahili. Utafiti pia ulibaini kuwa, utekelezaji wa kanuni za lugha za shule unahitaji mchango na ushirikiano wa wizara ya elimu, uongozi wa shule, walimu na wanafunzi wote ili athari yake iwe chanya kwa somo la Kiswahili.Item Itikadi Kama Chanzo cha Migogoro katika Msimu Wa Vipepeo K.W Wamitila (2006) na Mhanga Nafsi Yangu S.A Mohamed (2013).(Kenyatta University, 2025-04) Moses, Grace Mwende; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulishughulikia itikadi kama chanzo cha migogoro katika riwaya ya Msimu wa Vipepeo (2006) yake K.W Wamitila na Mhanga Nafsi Yangu (2013) yake S.A Mohamed. Utafiti huu ulinuia kuonyesha itikadi kama chanzo cha migogoro miongoni mwa wahusika katika riwaya teule. Tafiti tofauti zimefanywa na wataalamu kuhusiana na suala la migogoro katika riwaya ya Kiswahili. Hata hivyo, kadri ya ufahamu wa mtafiti haupo utafiti ambao umeangazia itikadi kama chanzo cha migogoro. Aidha, riwaya teule hazijachambuliwa kwa kuangazia mtazamo huu. Utafiti huu ulinuia kuchanganua itikadi kama chanzo cha migogoro katika riwaya teule, kutathmini athari za migogoro hii katika uwasilishaji wa maudhui na ploti katika riwaya na kujadili suluhu za migogoro hiyo kwa kuangazia riwaya teule. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Hejemonia iliyoasisiwa na mwanafalsafa Antonio Gramsci (1985). Mihimili ya nadharia hii ilikuwa ni, Hejemonia hutegemea makubaliano yaliyopo kati ya watawala na wanaotawaliwa, asasi za kijamii hutumiwa na tabaka tawala kuwapumbaza raia na Hejemonia huendelezwa kupitia kwa tamaduni za jamii husika. Mihimili hii ilimwezesha mtafiti kuichanganua data kwa ukamilifu. Mbinu ya kimaelezo ndiyo iliyotumiwa katika uchanganuzi wa data. Matokeo ya utafiti huu yameafikiana na yaliyotarajiwa katika utafiti huu kwa kudhibitisha kuwa itikadi ndizo chanzo cha baadhi ya migogoro iliyopo katika riwaya teule. Ni wazi kuwa, migogoro ambayo chanzo chake ni itikadi huibua maudhui tofauti na humsaidia mwandishi kuijenga ploti katika kazi yake. Mwisho, baadhi ya migogoro katika riwaya inaweza kusuluhishwa kwa kutumia mbinu tofauti ambazo ziliangaziwa. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa wasomi, watafiti na waandishi wa riwaya ya kiswahili kwa kukuza maarifa yao kuhusu suala la migogoro na itikadi za wahusika katika riwaya.Item Maudhui katika Nyimbo Zilizopendwa za Kiswahili: Mtazamo Linganishi wa Daudi Kabaka Na Kikundi cha Maroon Commandos(Kenyatta University, 2025-02) Malelu, Onesmus KiokoThe research intended to investigate themes in popular Swahili songs: A comperative approach of Daudi Kabaka and Maroon Commndos group. The songs were sang between the year 1960 and 1990. The research was guided by realism theory. The researcher went through recorded songs stored in round discs. Selected literary materials were also read for the purposes of getting data. The collected data was recorded and analysed guided by the research questions and objectives. The report was presented in five chapters. Chapter one includes the study topic, research questions, objectives of the study, justifications for the study, scope of the study, literature review and theoretical framework. The second chapter analyses themes in Daudi Kabaka and Maroon Commandos group songs. Chapter three examines how language use has aided in making the themes come out clearly. The fourth chapter examines the comparisons found between the works of the two artists. The fifth chapter includes summery, conclusion and recommendations for further research. This research will benefit other literary scholars and current artists to make their work better.Item Upokezi wa Taswira za Matangazo ya Biashara katika Runinga: Kata Ndogo za Nyali na Likoni Kaunti ya Mombasa, Kenya(Kenyatta University, 2025-06) Omuhonja, Elizabeth Nipher; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulichunguza upokezi wa taswira za matangazo ya biashara katika runinga. Matangazo kumi ya biashara yanayotangazwa kwa lugha ya Kiswahili yalichunguzwa pamoja na yale ambayo yanachanganya Kiswahili na lugha nyingine. Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha taswira zinazotumika kwenye matangazo yanayohusu bidhaa za nyumbani katika runinga, kuchanganua taswira zinazotumika kwenye matangazo yanayohusu huduma za mawasiliano katika runinga na kutathmini fasiri za watazamaji kuhusu taswira mbalimbali zilizoteuliwa kwa kuzingatia umri, jinsia na elimu. Sababu ya kufanya utafiti huu ni kuwa swala la kuonyesha namna mbinu ya taswira inavyotumika katika matangazo ya biashara kwa madhumuni ya kuathiri upokezi wa bidhaa zinazotangazwa halijachunguzwa kwa kina. Kazi hii iliongozwa na nadharia mbili; nadharia ya semiotiki iliyoasisiwa na Barthes (1984) inayohusu uhakiki wa ishara na nadharia ya ya upokezi iliyoasisiwa na Iser (1974) inayosisitiza nguvu za mpokeaji au msomaji katika kufasiri kazi anayoipokea na hutilia maanani dhima yake kwa kazi hiyo. Uchunguzi ulifanyika maktabani na nyanjani. Maktabani usomaji wa vitabu, tasnifu, makala na majarida yanayohusu mada ulifanyika kwa kina. Nyanjani data kuhusu fasiri mbalimbali za taswira ilikusanywa kwa kutumia hojaji katika maeneo ya Nyali na Likoni ili kuzitathmini. Matokeo ya utafiti yametolewa kwa njia ya kimaelezo na majedwali. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa watangazaji wa matangazo ya biashara hutumia taswira kwa wingi katika matangazo hayo ili kupitisha ujumbe kwa hadhira. Taswira zinazotumika haswa za ishara huhitaji umakinifu wa hali ya juu kutoka kwa hadhira ili waweze kuzifasiri vyema. Taswira za ishara zilipata fasiri mbalimbali kutoka kwa hadhira kwa kuzingatia vigezo vya, umri, jinsia na kiwango cha elimu. Matokeo ya utafiti huu yamewasilishwa katika sura tano. Utafiti huu umetoa mchango kwa wasomi na watafiti kwa kuonyesha namna mbinu ya taswira inavyotumika katika matangazo ya biashara kwa lengo la kuathiri upokezi wake.Item Uchanganuzi wa Kiisimu katika Mashairi Huru ya Kithaka wa Mberia na ya Kezilahabia(Kenyatta University, 2025-06) Wafula, Pouline Nangila; King'ei, Kitula Osore, MiriamLengo kuu la utafiti huu ni kuonyesha jinsi ushairi unavyoweza kuchanganuliwa kiisimu. Tasnifu hii inahusu uhakiki wa kiisimu wa ushairi wa Kiswahili katika mashairi huru ya Kithaka wa Mberia na ya Kezilahabi kwa mtazamo wa nadharia ya Fonolojia Mizani. Utafiti huu umejikita katika diwani teule za watunzi waliotajwa ambazo ni Doa, Msimu wa Tisa, Mvumo wa Helikopta, Kichomi na Karibu Ndani. Uteuzi wa diwani hizi ulifanywa kimakusudi kwa kuwa zina aina data iliyodhamiriwa kuchanganuliwa kiisimu ambayo ilitosheleza mahitaji ya utafiti huu. Mashairi sitini yalihakikiwa kutoka katika diwani teule. Vipengele vya kiisimu vilivyochanganuliwa ni: Aina za sentensi, kipengele cha nafsi na uakifishaji. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Fonolojia Mizani iliyoasisiwa na Liberman (1975) ambayo ina madai kuwa mkazo katika lugha uko katika mfumo wa mfuatano wiani wa kimsonge ambao hupanga silabi, maneno na virai katika sentensi. Tasnifu hii ina sura nne: Sura ya kwanza imeangazia utangulizi unaojumulisha vipengele vifuatavyo: mada, suala la utafiti, maswala ya utafiti, malengo ya utafiti, umuhimu wa utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka ya utafiti, yaliyoandikwa kuhusu mada, misingi ya nadharia, mihimili ya nadharia na mbinu za utafiti. Sura ya pili imeshughulikia vipengele vya kiismu vilivyobainishwa na jinsi vinavyotumika katika kuendeleza kazi ya mashairi huru teule ya Kithaka wa Mberia. Sura ya tatu imebainisha vipengele vya kiisimu na kuonyesha jinsi vilivyotumika katika kuendeleza mashairi huru ya Kezilahabi. Sura ya nne imeshughulikia umuhimu wa vipengele vya kiisimu kisha sura ya tano imeshughulikia muhtasari wa utafiti, matokeo ya utafiti, changamoto za utafiti na mapendekezo ya taifi zaidi. Data iliyotumika katika utafiti huu ilikusanywa kutoka maktabani. Maktabani ndiko usomaji ulifanywaa wa diwani za mashairi teule, tasnifu na vitabu vingine vinavyohusiana na mada ya utafiti na nadharia ya utafiti huu. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kutumia mbinu ya uhakiki matini kwa kuongozwa na pengo la utafiti, maswali na malengo ya utafiti na kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia ya Fonolojia Mizani. Kwa kufanya hivi, utafiti uligundua kwamba mbinu za kiisimu zinaweza kutumiwa katika uhakiki wa mashairi huru ya Kiswahili.Item Usawiri wa Mandhari Katika Diwani ya Doa(Kenyatta University, 2025-06) Gitonga, Doris Gakii; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulishughulikia usawiri wa mandhari katika katika Diwani ya Doa na jinsi mandhari hayo yamechangia katika uwasilishaji wa ujumbe wa mwandishi. Utafiti huu ulilenga kubainisha jinsi mtunzi alivyotumia aina tofauti za mandhari katika kukamilisha ujumbe wake. Utafiti huu umebainisha wazi mandhari mbalimbali katika diwani ya Doa (2018). Aidha, utafiti hu umedhihihirisha namna mandhari hayo yalivyosawiriwa kwa kuweka wazi umuhimu wake katika kukamilisha ujumbe wa mtunzi. Utafiti huu ulichunguza aina za mandhari katika diwani ya Doa (2018). Nadharia ya Naratolojia ndiyo iliyoongoza utafiti huu. Naratolojia iliyoasisiwa na Genette (1972) na baadaye kuendelezwa na De Jong (2012). Nadharia ya Naratolojia huchunguza sifa za muundo wa usimulizi kwa kugawa vipengele ambavyo huhusiana na simulizi kisha kuzingatia uhusiano na uamilifu baina ya vipengele hivyo. Data iliyotumiwa katika uchunguzi huu ilitoka maktabani na mtandaoni. Kwa maktaba, mtafiti alisoma yale yanayohusiana na mada lengwa yakiwemo tasnifu, majarida na vitabu vinginevyo hasa vinavyo husiana na nadharia husika. Mtandaoni mtafiti alisoma baadhi ya tafiti zinazohusiana na mada teule na yanayohusu utanzu wa ushairi. Sampuli kusudio ni nakala ya diwani ya Doa (2018) ambayo ilikuwa muhimu sana katika utafiti huu. Yaliyotokea katika utafiti huu yametolewa kwa maelezo ya kinathari na utoaji wa mifano. Matokeo ya utafiti huu yamepangwa katika sura tano. Matokeo ya utafiti huu yanatarajiwa kuchangia pakubwa katika fasihi ya Kiswahili hasa utanzu wa ushairi kwa kuonyesha aina za mandhari na nafasi yake katika ukuzaji wa maudhui.Item Athari ya Tamthilia ya Mashetani (1971) juu ya Tamthilia ya Mashetani Wamerudi (2016)(Kenyatta University, 2025-05) Nyanchama, Filister EuniceUtafiti huu ulilenga kuchunguza athari ya tamthilia ya Mashetani (1971) juu ya tamthilia ya Mashetani Wamerudi (2016). Kristeva (1966) anafafanua kuwa hakuna matini yoyote ya kifasihi inaweza kuangaliwa kivyake au kujitegemea. Hivyo basi, ilikuwepo haja kuangazia athari ya dhamira, maudhui, wahusika na mtindo katika tamthilia hizi teule. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Mwingilianomatini ilioasisiwa na Kristeva (1966). Mwingilianomatini ni kutegemeana na kuathiriana kwa tanzu au matini (Kuloba, 2015). Hivyo basi, mwingilianomatini ni wakati ambapo sifa za matini moja huweza kujitokeza katika matini nyingine. Mtafiti aliongozwa na malengo yafuatayo: Kwanza, kubainisha athari ya kimaudhui katika tamthilia ya Mashetani na tamthilia ya Mashetani Wamerudi. Pili, kuchunguza athari ya usawiri wa kiwahusika katika tamthilia ya Mashetani na Mashetani Wamerudi. Tatu, kuchanganua athari ya kimtindo katika tamthilia ya Mashetani na tamthilia ya Mashetani Wamerudi. Mbinu ya utafiti iliyotumika ni ya kimaelezo ambapo mtafiti alibainisha matukio au data mbalimbali katika tamthilia ya Mashetani na Mashetani Wamerudi. Data iliyokusanywa iliwasilishwa kwa maelezo na kwa kutoa mifano ya maudhui, usawiri wa wahusika na mtindo kwenye tamthilia zilizoteuliwa. Mtafiti aliteua sampuli kimakusudi ili kufanikisha malengo ya utafiti. Utafiti ulikuwa wa maktabani ambapo mtafiti alisoma tamthilia husika, tasnifu, majarida na vitabu ambavyo vinahusiana na mada.Item Harakati Za Ushairi wa Kiswahili Katika Ujenzi wa Jamii Yenye Mabadiliko: Mfano wa Diwani Ya Karne Mpya(Kenyatta University, 2025-05) Gaceri, Martha; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulichunguza harakati za ushairi wa Kiswahili katika ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Mashairi yaliyorejelewa ni yaliyo katika Diwani ya Karne Mpya (2007). Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha miktadha iliyoibua harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko, kueleza harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko katika diwani teule, pamoja na kuonyesha umuhimu wa harakati hizo katika jamii. Utafiti huu uliongozwa na baadhi ya mihimili ya nadharia ya Uhistoria Mpya. Nadharia ya Uhistoria Mpya ina misingi yake katika mawazo ya Raymond Williams (1977) na Michel Foulcault (1972, 1977, 1997). Nadharia hii huangalia uhusiano uliopo kati ya historia na fasihi. Hivyo, kazi ya fasihi haiwezi kutengwa na historia inayohusika nayo. Utafiti huu ulichukua muundo wa kimaelezo. Utafiti ulifanywa maktabani na mitandaoni. Sampuli ya utafiti huu iliteuliwa kimakusudi na data ikakusanywa kwa kusoma kwa kina mashairi teule na kunukuu sehemu ambazo zina data iliyokidhi mahitaji ya utafiti husika. Mtafiti pia alisoma vitabu, majarida, tasnifu na machapisho mbalimbali yaliyohusiana na mada. Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia iliyoongoza utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo ya kinathari na utoaji mifano. Utafiti huu ulibaini kuwa harakati mbalilmbali za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko, zimeibuliwa na miktadha mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Isitoshe, harakati hizi zina mnachango muhimu katika jamii ya sasa. Inatarajiwa utafiti huu utachangia katika uhakiki wa fasihi kinadharia. Aidha, utaifaa jamii hasa katika kuelewa harakati za kujenga jamii yenye mabadiliko na manufaa yake. Tasnifu hii imegawika katika sura tano. Sura ya kwanza imeshughulikia utagulizi, usuli wa mada, suala la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka, yaliyoandikwa kuhusu mada nadharia iliyoongoza utafiti huu pamoja na mbinu za utafiti. Sura ya pili imeshughulikia miktadha iliyoibua harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya tatu imeshughulikia harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya nne imeshughulikia umuhimu wa ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya tano imeshughulikia hitimisho, matokeo ya utafiti, changamoto za utafiti pamoja na mapendekezo ya utafiti.Item Mtindo kwenye Nyimbo za Jadi Katika Jamii Ya Wakisii Na Waswahili wa Nchini Kenya(Kenyatta University, 2025-06) Oroko, Kerubo Judith; King'ei, Kitula Osore, MiriamMtindo ni uti wa mgongo katika tungo za kisanaa, iwe hadithi, tamthilia, ushairi na hata nyimbo. Utafiti huu umejikita katika kuhakiki mtindo kwenye nyimbo za jadi za jamii ya Wakisii na jamii ya Waswahili wa nchini Kenya. Watafiti mbalimbali wametafiti swala la mtindo katika nyimbo kama vile: Iyaya na wenzake (2021) walitafiti mtindo na lugha ya uwasilishaji katika nyimbo za nyiso za jamii ya Watachoni ambazo ni wenyeji wa Kenya. Muriuki (2013) alitafiti mtindo katika nyimbo za kazi katika jamii ya Warabai. Utafiti huu unatofautiana na tafiti za hapo awali hasa kwa msingi wa malengo na mambo mengine. Utafiti huu umefanikiwa katika: kubainisha jinsi ambavyo watunzi wametumia mbinu za mtindo katika kusawiri historian a tamaduni za jamii ya Wakisii na Waswahili wa nchini Kenya. Hali kadhalika, utafiti huu umehakiki mbinu za mtindo kwenye nyimbo za jadi za jamii ya Wakisii na Waswahili. Mwisho kabisa, utafiti huu umefanikiwa kuchunguza jinsi ambavyo mbinu za mtindo zilivyotumiwa kufanikisha uwasilishaji wa maudhui katika jamii teule. Nadharia ya mtindo ambayo iliasisiwa na Coombes ndiyo iliongoza utafiti huu. Coombes (1953) anasema kuwa mtindo huchunguza lugha na kanuni zinazoongoza lugha yenyewe ili kubainisha mbinu za kimtindo zilizotumiwa, sababu ya mbinu hizo kutumiwa na athari ya mbinu hizo katika kazi husika. Katika nadharia hii lazima mhakiki wa kazi yoyote ile ya fasihi achunguze vipengele hivyo na aelewe utendekazi wake. Waitifaki wengine ni kama Leech na Short (1981) ambapo wanasema kuwa nadharia hii ina lengo la kuelezea uhusiano uliopo baina ya lugha na majukumu ya kisanaa. Ambapo swali kuu ni mbona mwandishi akaamua kujieleza kwa njia fulani? Nyimbo za jadi za jamii ya Wakisii na Waswahili zilizotumiwa katika utafiti ziliteuliwa kwa kutumia mbinu ya maksudi ambapo nyimbo zenye ukwasi wa mtindo ndizo zilizingatiwa. Utafiti hulifanywa makatabni na nyanjani. Maktabani ulihusisha kusoma vitabu, tasnifu, matini na majaida kuhusu mtindo. Nyanjani ulijumuhisha kuwahoji watu kumi wakongwe kutoka kila jamii na kila jinsia ikiwakilishwa na watu watano watano. Hali kadhalika, hadhira ambayo ilishiriki katika uimbaji isailiwa ambapo watu wawili wawili kutoka kila sherehe walishirikishwa na mwisho kabisa watu wanne kutoka kila jamii ambao waliongozwa katika uimbaji wa nyimbo hizo walishirikishwa katika utafiti. Wawili wawili kutoka kwa kila jinsia. Mbali na hayo, mbinu ya kusikiliza na kurekodi nyimbo hio za jadi ilitumiwa baada ya hapo uchambuzi ukaanza. Data ilichanganuliwa kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia, maswali na malengo ya utafiti. Kazi hii imepangwa katika sura tano. Utafiti huu uliweza kubainisha kuwa mbinu za mtindo zina nafasi kubwa katika kuendeleza nyimbo za jadi. Utafiti huu utakuwa na mchango mkubwa katika uwanaja wa fasihi simulizi kwa utawasadia wataalamu wa fasihi nawanafunzi wa fasihi kuchanganua na kuelewa mtindo katika nyimbo za jadi za jamii husika na pia katika kuhakiki mtindo katika tanzu zingine za fasihi simulizi.Item Matumizi ya Nyenzo za Kusikiliza na Kuona Katika Ufunzaji na Ujifunzaji wa Matamshi Katika Shule za Upill, Kaunti ya Kiambu, Kenya(Kenyatta University, 2022-10) Osore, Joy Lodenyi; King'ei, Kitula Osore, MiriamAbstractItem Uwasilishaji wa Maudhui ya Utamaduni Katika Riwaya Teule za Kiswahili(Kenyatta University, 2023-06) Kinyua Gatakaa Caroline; King'ei, Kitula Osore, MiriamAbstractItem Tathmini ya Viwango vya Maarifa ya Fasihi Katika Shule za Msingi, Kaunti ya Nyeri(Kenyatta University, 2022-04) Muriuki, Elizabeth Wangari; King'ei, Kitula Osore, MiriamAbstractItem Utata wa Kubainisha Homonimu na Polisemi Katika Kamusi Ya Kiswahili Sanifu na Kamusi ya Karne ya 21(Kenyatta University, 2019-02) Makenge, Juma Abdul; King'ei, Kitula Osore, MiriamAbstractItem Historia na Bunilizi katika Kaburi bila Msalabana Wimbo Mpya(Kenyatta University, 2023-03) Ng'ang'a, Hannah Njoki; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulichunguza uhusiano uliopo kati ya historia na bunilizi katika riwaya za Kaburi Bila Msalaba (Karcithi, 1969) na Wimbo Mpya (Mbatiah, 2004). Riwaya hizi zina mchango thabiti kwa bunilizi na historia. Hoja hizi thabiti hazijafanyiwa utafiti wa kina. Utafiti huu ulitumia vigezo vya matukio, usawiri wa wahusika na mitindo katika viwango mbalimbali ili kufikia malengo yake. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo; Kwanza, kuchambua maudhui ya kihistoria na kibunilizi katika riwaya za Kaburi Bila Msalaba na Wimbo Mpya. Pili, kuchunguza usawiri wa wahusika wa kihistoria na wa kibunilizi katika riwaya za Kaburi Bila Msalaba na Wimbo Mpya. Tatu, kubainisha jinsi vipengele vya kibunilizi vilivyotumika katika riwaya za Kaburi Bila Msalaba na Wimbo Mpya. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Uhalisia wa Kihistoria. Kwa kuzingatia mihimili ya nadharia hii, riwaya teule zilihakikiwa ili kupata matokeo yaliyotosheleza mabhitaji ya utafiti. Data ilirckodiwa na kuchanganuliwa kulingana na malengo ya utafiti, maswali ya utafiti na mihimili ya nadharia husika. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maclezo. Mbinu za utafiti zilijumlisha; Muundo wa utafiti, mahali pa utafiti, uteuzi wa sampuli, ukusanyaji wa data, uchanganuzi wa data na uwasilishaji wa matokeo. Kutokana na utafiti huu mahsusi, tulipata kuwa riwaya teule zina viwango mbalimbali vya kihistoria na kibunilizi. Hivyo basi ilibainika kuwa bunilizi na historia vinakuwa vigezo muhimu vya kuendeleza fasihi kwa mujibu wa utafiti huu.Item Tathmini ya Usimulizi Katika Mahubiri ya Kiswahili kwa Watoto: Muktadha Wa Kanisa la Kiadventista Katika Kaunti ya Nakuru, Kenya(Kenyatta University, 2023-06) Masika, Rogers Mulwa; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulinuia kuchunguza usimulizi katika mahubiri ya Kiswahili kwa watoto katika kanisa la Kiadventista. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kuchunguza dhamira na maudhui ya masimulizi katika mahubiri kwa watoto, kuchunguza mbinu zilizotumika kuwasilisha masimulizi katika mahubiri kwa watoto na kuchunguza jinsi wahusika walivyosawiriwa katika masimulizi kwa watoto. Nadharia ya naratolojia iliyoasisiwa na Todorov mwaka wa 1969 pamoja na nadharia ya semiotiki iliyoasisiwa na Pierce (1977) ilitumika kuongoza utafiti huu. Kwa mujibu wa Todorov, nadharia ya naratolojia hubaini sifa za masimulizi na zinavyojitokeza katika miktadha mahsusi. Nadharia ya semiotiki inahusu ufasiri wa maana kutokana na ishara. Data zilikusanywa nyanjani kwa kutumia mbinu ya kuchunza au ushuhudiaji. Mtafiti alihudhuria ibada katika makanisa teule ya Kiadventista na kurekodi mahubiri hayo na kisha kuyasikiliza na kuyanakili kwa maandishi. Hatimaye, data zilichanganuliwa kwa kuongozwa na nadharia ya naratolojia na semiotiki. Matokeo ya utafiti huu yalibainisha kuwa hadithi nyingi za watoto zilihusu maadili na kwa hivyo wasimulizi walikusudia kuwafundisha watoto kuzingatia maadili mema katika Jjamii. Aidha, matokeo ya utafiti huu yalionyesha kuwa matumizi ya masimulizi huboresha usikivu wa watoto. Kwa hivyo, utafiti huu una manufaa kwa walimu na wahubiri wa watoto hasa katika kuteua ujumbe ufaao na unaowajenga watoto kimaadili na pia kutumia mbinu ya uwasilishaji ambayo itawafanya watoto kuchangamkia ujumbe.Item Ubora Wa Tafsiri Katika Kamusi Tafsiri Za Mtandaoni(Kenyatta University, 2024-06) Lukungu, Winnie O.; King'ei, Kitula Osore, MiriamKiswahili ni lugha inayozidi kukita mizizi kidijitali kupitia mbinu anuai ikiwemo programu za kamusi na vitabu vingine kama Bibilia vilivyoswahilishwa na kuhifadhiwa mtandaoni. Utafiti huu ulinuia kudihirisha ubora wa tafsiri ya maneno yaliyotolewa katika kamusi-tafsiri za mtandaoni. Kwa kuwa enzi hii kuna watumizi wengi wa mtandao kwa malengo anuai, kamusi za mtandaoni zina dhima kuu na hivyo kuwepo na tafsiri potovu kunaweza kuwaathiri watumiaji wengi. Utafiti ulichukua muundo wa kutathmini tafsiri ya maneno kwenye kamusi zilizoteuliwa za mtandaoni kuanzia alfabeti A – M na kutoa mapendekezo ya tafsiri bora zaidi, kwa msaada wa wataalamu wa lugha kama vile waandishi wa kamusi kama walivyolengwa na mtafiti. Mtafiti alishirikiana moja kwa moja na wataalamu hawa kama vile waandishi wa vitabu mbalimbali na wanaotumia kamusi hizi katika kuandaa tasnifu yake kupitia kwa mahojiano, hojaji pamoja na mawasiliano ya kila mara kupitia simuni ili kuhakikisha kuwa malengo yake yametimia. Utafiti huu ulilenga tafsiri ya Kiingereza-Kiswahili na wala sio lugha zingine. Mihimili ya Nadharia ya Isimu Kongoo ilitumika katika kupendekeza kongoo matini bora inayotumika kama tafsiri kwa kamusi za mtandao. Mbali na nadharia hii, nadharia ya Ulinganifu wa Kimuundo ambayo ni mojawapo ya miavuli ya nadharia ya Tafsiri ilitumika katika kuasisi tafsiri bora kwa maneno. Utafiti ulikuwa wa kimaelezo, na usampulishaji wa kimakusudi ulitumika katika kuwateua wahojiwa pamoja na kuteua data kutoka kwenye kamusi za mtandao. Data ilichanganuliwa kwa mwongozo wa mihimili ya nadharia pamoja na malengo ya utafiti. Baada ya kuchanganua data, matokeo yaliwasilishwa kwa kutumia maelezo na michoro ya jadwali kisha kutolewa maelezo yake. Matokeo ya utafiti yananuia kuboresha tafsiri ya kamusi kwenye mtandao ili kuwafaidi wategemezi, waunfaji na watumiaji wa kamusi hizi katika shughuli zao anuai. Baadhi ya watakaoweza kufaidi kwa kamusi yenye tafsiri bora ni pamoja na wasomi, watafsiri, walimu, pamoja na wageni wanaotumia kamusi hizi ili kujifundishia lugha ya Kiswahili.Item Makosa Ya Kiisimu Ya Wanafunzi Wanaojifunza Kiswahili Kama Lugha Ya Pili: Uchunguzi Kuhusiana Na Lahaja Ya Kigichugu(Kenyatta University, 2024-10) Njagi, Nancy Wanja; King'ei, Kitula Osore, MiriamBinadamu wanahitaji lugha ili kuwasiliana na mojawapo ya lugha maarufu ulimwenguni ni Kiswahili. Kiswahili kimetafitiwa na wataalamu wengi ili kutafuta suluhisho la baadhi ya changamoto zinazokumba lugha hii na kuiboresha. Mojawapo ya changamoto na suala ambalo halijatafitiwa na utafiti huu ulikusudia kuchunguza ni makosa ya kiisimu ya wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya pili: Uchunguzi kuhusiana na lahaja ya Kigichugu.Wataalamu ambao wamechunguza masuala ya Kigichugu wameshughulikia masuala mengine tofauti na hili kama vile Kamau (1996) aliyelinganisha michakato ya kifonolojia ya lahaja hii na ya Kindia, Ruri (2011) anayelinganisha vitamkwa vya konsonanti za Kindia na Kigichugu. Naye Gituru (2019) anaangazia unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ, Iribe (2012) anachunguza mbinu tofauti za kifonolojia zinazotumika katika kutohoa maneno ya Kiswahili yanapoingia katika Kigichugu na Ndung’u (2022), aliyefanya utafiti kati ya wanajamii wanaozungumza lahaja ya Kindia na wale wanaozungumza Kigichugu kuhusu mitazamo ya lugha na utambulisho wa kijamii. Utafiti huu ulitumikiza kanuni na mihimili ya nadharia ya Sintaksia Finyizi ili kuweka wazi makosa ya kisintaksia na kisemantiki yanayofanywa na wanagenzi wa Kigichugu wanapojifunza Kiswahili kama L2. Uchunguzi huu uliendelezwa nyanjani na maktabani. Nyanjani ulitekelezwa katika shule za sekondari za kutwa katika kaunti ndogo ya Gichugu. Katika utafiti huu tulipaswa kuteua shule, na wanafunzi wa kufanyia utafiti. Katika uchaguzi wa shule za kutwa za kufanyia utafiti tulitumia mbinu ya sampuli kimaksudi. Katika uteuzi wa wanafunzi tulitumia usampulishaji wa kinasibu pale ambapo tulipatia wanafunzi nambari kinasibu na kuteua waliopata nambari moja hadi sita. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia hojaji, insha na masimulizi. Data ya utafiti iliwasilishwa kupitia majedwali na maelezo. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa wengi wa wanafunzi katika shule za upili za kutwa katika eneo la Gichugu hujifunza Kigichugu kama lugha yao ya kwanza. Isitoshe, wengi huanza kutumia Kiswahili wanapojiunga na shule. Licha ya hilo, makosa ya kisintaksia na kisemantiki yaliyotokana na lahaja ya Kigichugu yalijitokeza katika utafiti huu. Makosa haya yalichanganuliwa kwa kutumia nadharia ya Sintaksia Finyizi na kudhihirisha ukiukaji wa kanuni za nadharia hii. Aidha utafiti huu ulibainisha vyanzo vya makosa haya ambavyo vinaegemea kwa kiasi kikubwa kwa L1.Vyanzo hivi ni: uhamishaji wa mifumo ya kiisimu, tafsiri sisisi na ujumlishaji mno. Ili kupunguza makosa haya, mikakati mbalimbali ilibainishwa; ufundishaji kwa mwelekeo wa uchanganuzi linganuzi,walimu kutangamana na wanafunzi, wanafunzi kukosoana na kutahadharisha wanafunzi dhidi ya tafsiri za moja kwa moja kutoka L1.Item Nafasi na Mahali katika Hadithi Fupi Teule za Diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine(Kenyatta University, 2024-11) Njoroge, Florence Wahu; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulichunguza kipengele cha nafasi na mahali katika hadithi fupi ya Kiswahili kwa kurejelea diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine (2007) iliyoharirirwa na Mwenda Mbatia. Vipengele tofauti vya fasihi kama vile, wahusika na uhusika, mandhari, mtindo na matumizi ya lugha vimetafitiwa na watafiti mbalimbali. Hata hivyo, kadri ya ufahamu wa mtafiti, utafiti kuhusu nafasi na mahali kama kipengele cha fasihi haujafanywa kwa kina katika fasihi ya Kiswahili. Vilevile, diwani teule haijachambuliwa kwa kutumia mtazamo wa nafasi na mahali. Utafiti huu ulinuia kuchunguza: Vipengele vya nafasi na mahali kama vinavyojitokeza katika diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine, kuonyesha namna kipengele cha nafasi na mahali kilivyowasilishwa katika hadithi teule, na kuonyesha umuhimu wa nafasi na mahali katika kujenga maudhui na wahusika katika hadithi fupi teule za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Utafiti uliongozwa na nadharia ya naratolojia mkondo wa De Jong (2012) wa nafasi katika usimulizi. Mihimili ya nadharia iliyotumika ni; nafasi ya hadithi, nafasi ya msimulizi, fremu na vielezo. Utafiti ulifanywa maktabani na mtandaoni ili kupata data ya kuufaa utafiti wetu. Mtafiti aliisoma diwani teule, tasnifu na makala mengine muhimu. Uteuze wa sampuli ulifanywa kimakusudi ambapo mtafiti aliteua hadithi sita za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Data ilikusanywa, kuchanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo. Matokeo ya utafiti wetu yaliafiki matarajio yetu kwa kuthibitisha kuwa nafasi na mahali ni kipengele cha kimsingi katika ujenzi wa hadithi. Utafiti ulibainisha vipengele tofauti vya nafasi na mahali ambavyo vinapatikana katika hadithi teule za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Isitoshe, mtafiti alionyesha mbinu mbalimbali zilizotumika kuwasilisha nafasi na mahali katika hadithi teule na hatimaye akaonyesha dhima ya nafasi na mahali katika ujenzi wa maudhui na wahusika wa hadithi teule katika diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa waandishi wa fasihi ya Kiswahili hususan wa hadithi fupi, wasomi na watafiti wa baadaye wa fasihi ya Kiswahili.