Mchango wa Sitiari na Metonimu Katika Uzuaji wa Polisemia Katika Kiswahili

Loading...
Thumbnail Image
Date
2024-04
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuangazia mchango wa sitiari na metonimu katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili ambapo uliweza kupambanua namna metonimu na sitiari zinavyoweza kuzua maana mpya ya maneno ya Kiswahili. Pia ulitusaidia kufahamu athari ya metonimu na sitiari katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili. Kimsingi polisemi ni leksimu moja yenye maana nyingi ambazo zinahusiana kwa njia moja au nyingine (Chacha na Pendo, 2019). Pia kuna njia zingine za uzuaji wa polisemi kwa mfano ukopaji, mabadiliko katika matumizi ya neno, na ufasiri mpya wa homonimu. Kuna baadhi ya wataalamu ambao wamezungumzia polisemia kama vile Mwendamseke (2016) aliyeandika makala kuhusu uelekeo wa maana za kipolisemia katika msamiati wa Kiswahili. Naye Gaichu (2013) alishughulikia uchunguzi wa sitiari dhanifu katika methali za Kiswahili. Utafiti huu wa sitiari na metonimu ndio usiodhihirika moja kwa moja. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: Kubainisha polisemi ambazo zimeundwa kutokana na sitiari na metonimu katika Kiswahili, kuainisha polisemi katika lugha ya Kiswahili, kudhihirisha mchakato ambao sitiari na metonimu hupitia kuunda polisemi katika Kiswahili. Nadharia ya semantiki tambuzi iliongoza utafiti huu. Nadharia hii ni sehemu ya nadharia ya Isimu Tambuzi ambayo ina misingi katika saikolojia tambuzi (Vyvyan & Greens, 2006). Data husika ilikusanywa maktabani. Maktabani, maneno ambayo ni polisemi na yameundwa kwa sitiari na metonimu kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2018) yalikusanywa. Mbinu ya usampulishaji wa kimaksudi ilitumika katika uteuzi wa sampuli. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo na majedwali ili iweze kueleweka. Kutokana na data ya utafiti huu, imebainika kuwa kuna baadhi ya polisemi zilizojitokeza ndani ya homonimu. Kwa mfano, tata2 na chuo1. Pia, imebainika kuwa data hiyo ilikuwa na polisemi za majina ya wanyama, wadudu na ndege. Hata hivyo, imebainika kuwa sitiari huwa na maeneo mawili ya ufahamu: moja ni ile inayotokana na maumbo tunayoyaona na nyingine ni ile ya kidhahania. Hiyo ya kwanza inaitwa eneo chasili na ya pili eneo lengwa. Kwa mfano, sitiari “Maria ni chui” maumbo tunayoyaona (eneo chasili) ni Maria na chui na maumbo ya kidhahania (eneo lengwa) ni ukali. Kwa upande mwingine, imebainika kuwa metonimu huwa na eneo moja. Kwa mfano, leksimu kiti eneo lake ni uongozi. Tafiti zingine zinaweza kufanywa kuhusu mchango wa mbinu zingine za lugha kama vile tashibihi, lakabu na jazanda yaani; namna ambavyo mbinu hizo zinaweza kuchangia pia katika kuunda polisemia katika Kiswahili.
Description
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu Cha Kenyatta, Aprili 2024. Supervisor Leonard Mwita Chacha
Keywords
Citation