Athari za Katama Mkangi kwa John Habwe: Mfano Kutoka kwa Riwaya Teule za Mafuta (1984) na Cheche za Moto (2008)

Loading...
Thumbnail Image
Date
2023-11
Authors
Musyoka, Kalingwa Felix
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu unashughulikia athari za Katama Mkangi kwa John Habwe kwa kujikita katika riwaya teule za Kiswahili za Mafuta (1984) na Cheche za Moto (2008). Utanzu wa riwaya ya Kiswahili umeendelea kupanuka kimaudhui na kifani kutokana na juhudi za watunzi mbalimbali kama vile Katama Mkangi na John Habwe. Japo tafiti za awali zimetafitia suala la mwingiliano matini, tafiti nyingi zimejikita katika kazi za mtunzi mmoja.Utafiti wa kina ulihitajika kuchunguza namna utunzi wa Mafuta (1984) ulivyoathiri John Habwe alipoitunga riwaya yake ya Cheche za Moto (2008). Katama Mkangi aliandika riwaya ya Mafuta katika wakati wa chama kimoja cha kisiasa ambapo uhuru wa kujieleza ulikuwa umebanwa sana. Habwe ameandika kazi yake ya Cheche za Moto katika mazingira yaleyale, miaka ishirini na minne baadaye. Wakati wa utunzi wa Cheche za Moto, uhuru wa kujieleza ulikuwa umepanuliwa. Kwa hivyo, amekwepa mtindo wa kimajazi alioutumia Mkangi na kuyaangazia masuala anayoyaibua Mkangi kwa njia wazi. Utafiti huu uliongozwa na malengo matatu: kwanza, ni kufafanua namna mwangwi wa maudhui ya riwaya ya Mafuta unavyojitokeza katika riwaya ya Cheche za Moto, kubainisha athari za usawiri wa wahusika wa Katama Mkangi kwa John Habwe, na mwisho, kuonyesha athari za kimtindo za Katama Mkangi kwa John Habwe. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya mwingiliano matini iliyoasisiwa na Julia Kristeva (1969). Mihimili mikuu ya nadharia hii iliyoongoza utafiti huu ni pamoja na: hakuna matini ya fasihi yenye sifa za pekee, matini hubainisha sifa mbalimbali za matini tangulizi, na mwisho, matini ya baadaye huweza kufafanua dhana fulani kutoka matini tangulizi kwa njia inayoeleweka. Nadharia hii ya mwingiliano matini ilisaidia pakubwa kuonyesha namna kazi ya awali, Mafuta (1984) ilivyomwathiri John Habwe katika utunzi wa Cheche za Moto (2008), kimaudhui na kifani. Riwaya ziliteuliwa kimakusudi ili kupata sampuli faafu yenye data ya kujaza pengo la utafiti. Data ilikusanywa kupitia kwa usomaji wa maktabani na vilevile kusakura mitandaoni kuhusu vipengele vya mwingiliano matini katika riwaya ya Kiswahili. Data hii imewasilishwa kwa njia ya kimaelezo. Utafiti huu unatarajiwa kutoa mchango katika uhakiki wa utanzu wa riwaya ya Kiswahili, hususan kuhusu kipengele cha kuathiriana baina ya watunzi wa riwaya za Kiswahili.
Description
Tasnifu Hii Inawasilishwa kwa Minajili ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Novemba 2023
Keywords
Athari za Katama Mkangi kwa John Habwe, Mfano Kutoka kwa Riwaya Teule za Mafuta (1984), Cheche za Moto (2008)
Citation