Athari za Sheng’ kwa Kiswahili Sanifu: Uchunguzi wa Kamusi ya Sheng’.

Loading...
Thumbnail Image
Date
2023
Authors
Muyumba, Jotham
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulidhamiria kutathmini athari za kamusi ya Sheng’ – English Dictionary kwa Kiswahili sanifu. Kamusi ya Sheng’ –English Dictionary (2003) iliteuliwa kama msingi wa uchunguzi huu kwa sababu ndio kamusi ya kwanza ya Sheng’ kuwahi kuchapishwa. Licha ya kamusi hii kuchapishwa katika lugha ya Kiingereza ina leksimu za Sheng’ ambazo yafaa kuchunguzwa namna zinavyoathiri Kiswahili sanifu kwa wakati wa sasa. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kubainisha maneno yaliyomo katika Sheng’- English Dictionary na katika Kiswahili sanifu. Kadhalika, utafiti huu ulinuia kueleza muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na jinsi yanavyotofautiana na Kiswahili sanifu. Mwisho, utafiti huu ulidhamiria kueleza sababu za utofauti wa muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na kueleza athari zake kwa Kiswahili sanifu. Nadharia ya utafiti ilikuwa Nadharia ya Fonolojia Boreshi ambayo inapatikana katika mtazamo mpana wa Nadharia Boreshi iliyoasisiwa na Alan Prince na Paul Smolensky (1991). Hii ni nadharia inayochunguza hatua za ukuaji wa msamiati kutoka hali ghafi hadi ukubalifu wake kupitia kwa vizuizi tofauti. Mahali pa utafiti palikuwa maktabani na mtandaoni. Mbinu ya uchunguzi ikawa kupitia kusikiliza wazungumzaji wa Sheng’ na kusoma makala mbalimbali kuhusu mada hii. Data ilikusanywa kupitia kwa kuchunguza maneno na vidahizo vya maneno kutoka kamusi ya Sheng’ – English Dictionary (2003). Iliaminika kuwa kamusi hii ingetoa sampuli ya maneno mahsusi ya Sheng’ ambayo muundo wake huathiri matumizi katika Kiswahili sanifu kwenye jamii ya kisasa. Uchanganuzi wa maelezo ulitegemea mtazamo wa Fonolojia Boreshi katika nadharia ya fonolojia inayoangazia sarufi zalishi. Katika mtazamo huu, uambishaji wa maneno uliangaziwa na jinsi uundaji huo hutawaliwa na vizuizi mbalimbali na sheria za fonolojia. Kadhalika nadharia ya Fonolojia Boreshi ilitumika kueleza michakato ya namna wazungumzaji wa Sheng’ hubuni leksimu mbalimbali katika mawasiliano. Uwasilishaji wa data ulikuwa kupitia kwa maelezo ya kina, michoro na jedwali. Matokeo ya utafiti huu ni kuwa: maneno yanayopatikana katika Sheng’ – English Dictionary na Kiswahili sanifu yalibainishwa. Pia, muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na namna yanavyotofautiana na Kiswahili sanifu ulielezwa. Kadhalika, sababu zinazochangia utofauti wa muundo wa kifonolojia wa maneno ya Sheng’ na Kiswahili sanifu zilielezwa. Uchunguzi huu ulidhamiria kuchangia usomi wa Kiswahili kwa kuweka wazi athari za Sheng’ katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili kimsamiati. Kadhalika, utafiti huu utawasaidia wanafunzi kuweka mipaka bayana kati ya msimbo wa Sheng’ na lugha ya Kiswahili sanifu.
Description
Tasnifu hii Inawasilishwa Katika Idara ya Kiswahili kwa Madhumuni ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Kenyatta
Keywords
Sheng’, Kiswahili Sanifu, Kamusi ya Sheng’.
Citation