Maendeleo ya Tawasifu ya Kiswahili tangu Karne ya 19 hadi 21
Loading...
Date
2023
Authors
Wabomba, Eric W.
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umechanganua tawasifu tatu zilizoandikwa katika karne tatu tofauti ambazo ni:
Tawasifu ya Tippu Tip iliyoandikwa karne ya 19 na kuhaririwa na Whiteley (1958), ya
Shaaban Robert (1969) ya Maisha yangu na Baada ya miaka Hamsini, ya karne ya 20, na
tawasifu ya Ken Walibora (2014) ya Nasikia sauti ya Mama, ambayo iliandikwa katika karne
ya 21. Utafiti huu ulikuwa na malengo matatu ambayo ni: Kuchanganua vipengele vya uhalisia
na ubunifu katika tawasifu ya Tippu Tip iliyohaririwa na Whiteley (1958); Kuchanganua
vipengele vya uhalisia na ubunifu katika tawasifu ya Shaaban Robert (1969); Kuchanganua
vipengele vya uhalisia na ubunifu katika tawasifu ya Ken Walibora (2014). Vipengele hivi
vilichanganuliwa kwa kuangazia maudhui na mtindo wa uandishi uliotumika katika tawasifu
hizi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili ambazo ni: Nadharia ya Uhalisia na nadharia ya
Mtindo. Nadharia ya Uhalisia iliasisiwa na Hegel (1975 – 1979), Zola (1969) na Flaubert
(1972), miongoni mwa wengine. Kwa mujibu wa nadharia ya Uhalisia, maisha ya jamii
yanafaa kuwasilishwa kwa uaminifu na usahihi mkubwa. Mambo yanayoonekana katika jamii
ndiyo hutiliwa mkazo. Nadharia ya Mtindo iliasisiwa na Buffon (1930) na kuendelezwa na
waasisi wengine wakiwemo Wellek na Warren (1949), Coombes (1963), na Leech (1981).
Nadharia hii huchunguza lugha ili kubainisha ubunifu uliomo kwenye lugha hiyo. Nadharia ya
Uhalisia ilichaguliwa kuongoza utafiti huu kwa sababu, mwandishi yeyote wa tawasifu
anatazamiwa kuelezea ukweli halisi kuhusu maisha yake. Kwa upande mwingine, nadharia ya
Kimtindo ilichaguliwa kwa vile ambavyo tunatarajia mtunzi wa kinathari aelezee kiubunifu
maisha yake akizingatia mbinu zinazoakisi ukweli, uzushi, chuku na kadhalika. Nadharia ya
Uhalisia kwa upande mmoja, ilisaidia katika kuangalia viwango vya uyakinifu katika tawasifu
hizi. Kwa upande mwingine, nadharia ya mtindo ilichangia katika kubainisha mtindo na
ubunifu uliomo katika tawasifu hizi tatu. Mbinu za utafiti zilizotumiwa katika utafiti huu ni
kusoma kwa kina, kueleza na kuchanganua vipengele vya mada. Data zilizotokana na utafiti
huu zinabainisha viwango vya uhalisia na ubunifu na hivyo kuchangia pakubwa katika ujuzi
wa tawasifu kama kipera cha riwaya. Watafiti wengine wanaopania kuzama katika uwanja wa
tawasifu na uandishi wa kinathari kwa ujumla watafaidika kwa data za utafiti huu. Matokeo ya
utafiti huu yatakuwa muhimu katika tafiti nyingine, haswa zile zitakazonuia kushughulikia
uhalisia na ubunifu, sio tu katika tawasifu ya Kiswahili, bali katika tagaa la riwaya kwa ujumla.
Description
Tasnifu hii Imetolewa kwa Madhumuni ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, June, 2023
Keywords
Maendeleo ya Tawasifu, Kiswahili, Kiswahili tangu Karne ya 19 hadi 21