Nafasi na Mahali katika Hadithi Fupi Teule za Diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine
Loading...
Date
2024-11
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza kipengele cha nafasi na mahali katika hadithi fupi ya Kiswahili kwa kurejelea diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine (2007) iliyoharirirwa na Mwenda Mbatia. Vipengele tofauti vya fasihi kama vile, wahusika na uhusika, mandhari, mtindo na matumizi ya lugha vimetafitiwa na watafiti mbalimbali. Hata hivyo, kadri ya ufahamu wa mtafiti, utafiti kuhusu nafasi na mahali kama kipengele cha fasihi haujafanywa kwa kina katika fasihi ya Kiswahili. Vilevile, diwani teule haijachambuliwa kwa kutumia mtazamo wa nafasi na mahali. Utafiti huu ulinuia kuchunguza: Vipengele vya nafasi na mahali kama vinavyojitokeza katika diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine, kuonyesha namna kipengele cha nafasi na mahali kilivyowasilishwa katika hadithi teule, na kuonyesha umuhimu wa nafasi na mahali katika kujenga maudhui na wahusika katika hadithi fupi teule za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Utafiti uliongozwa na nadharia ya naratolojia mkondo wa De Jong (2012) wa nafasi katika usimulizi. Mihimili ya nadharia iliyotumika ni; nafasi ya hadithi, nafasi ya msimulizi, fremu na vielezo. Utafiti ulifanywa maktabani na mtandaoni ili kupata data ya kuufaa utafiti wetu. Mtafiti aliisoma diwani teule, tasnifu na makala mengine muhimu. Uteuze wa sampuli ulifanywa kimakusudi ambapo mtafiti aliteua hadithi sita za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Data ilikusanywa, kuchanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo. Matokeo ya utafiti wetu yaliafiki matarajio yetu kwa kuthibitisha kuwa nafasi na mahali ni kipengele cha kimsingi katika ujenzi wa hadithi. Utafiti ulibainisha vipengele tofauti vya nafasi na mahali ambavyo vinapatikana katika hadithi teule za diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Isitoshe, mtafiti alionyesha mbinu mbalimbali zilizotumika kuwasilisha nafasi na mahali katika hadithi teule na hatimaye akaonyesha dhima ya nafasi na mahali katika ujenzi wa maudhui na wahusika wa hadithi teule katika diwani ya Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine. Matokeo ya utafiti huu yatakuwa ya manufaa kwa waandishi wa fasihi ya Kiswahili hususan wa hadithi fupi, wasomi na watafiti wa baadaye wa fasihi ya Kiswahili.
Description
Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Kenyatta
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Novemba 2024.
Msimamizi
Jesse Murithi