Usawiri wa Hadhi ya Mwanamke katika Methali za Igikuria na Maroa

Loading...
Thumbnail Image
Date
2024-11
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umechunguza na kuchanganua usawiri wa hadhi ya mwanamke katika methali za Igikuria. Suala la mwanamke katika ulimwengu wa sasa ni la kimsingi mno. Makundi ya wasomi, wanadini, wanasiasa na wanaoshughulikia haki za binadamu wamezama katika kuchunguza upya nafasi ya mwanamke katika jamii za ulimwenguni. Hili linatokana na madai mengi na hisia kuwa mwanamke ana hali duni katika jamii nyingi duniani. Tafiti za awali zilizofanywa kuhusu vipera vya fasihi simulizi kama vile; nyimbo na methali zilidhihirisha namna tofauti mwanamke anavyodunishwa katika jamii za Kiafrika kutokana na mifumo tawala inayompendelea mwana mume. Mifumo hii imejificha katika mila na desturi potovu za jamii mbalimbali. Japo hatupingi kauli za tafiti za awali, ni wazi kuwa, wanawake ni nguzo muhimu katika jamii nyingi duniani na wana mchango wao katika uendelezaji wa asasi tofauti za jamii. Kwa vile lugha huumbwa na utamaduni wa jamii, hutumika pia kama chombo cha kuusafirisha utamaduni huo. Methali kama mbinu ya lugha husheheni falsafa ya jamii inayoitumia lugha hiyo. Kutokana na ukweli huo, mtafiti amechunguza na kuchanganua usawiri wa hadhi ya mwanamke katika methali za Igikuria. Mtafiti amechunguza na kufafanua baadhi ya methali zinazomwinua na kumdunisha mwanamke ili kutimiza malengo ya utafiti. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Ufeministi katika maelezo na uchanganuzi wa data. Uwasilishaji wa data umefanywa kwa njia ya maelezo ambayo yametolewa mifano mwafaka ili kueleweka zaidi. Tasnifu hii ina sura tano kuu; sura ya kwanza ni utangulizi, usuli wa mada, suala la utafiti, malengo na maswali ya utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka ya utafiti, yaliyoandikwa kuhusu mada, misingi ya nadharia na mbinu za utafiti. Sura ya pili imechunguza methali za Igikuria zinazomwinua mwanamke kwa kuzingatia baadhi ya mihimili ya Ufeministi. Sura ya tatu imechunguza baadhi ya methali za Igikuria zinazomdunisha mwanamke, miktadha yake na kuzilinganisha na mihimili ya nadharia iliyoongoza utafiti huu kwa jumla. Dhima ya methali za Igikuria imeangaziwa na kufafanuliwa katika sura ya nne ambapo mtafiti ameeleza utendaji wake. Sura ya tano ni hitimisho la utafiti huu ambapo mtafiti ameeleza matokeo ya utafiti, msimamo wake na mapendekezo kwa wasomi, watafiti na wapangaji sera ya elimu.
Description
Tasnifu Imewasilishwa katika Idara ya Kiswahili, Shule ya Sheria, Sanaa na Sayansi za Kijamii ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa Ajili ya Kutimiza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili, Novemba 2024. Msimamizi Catherine Nduko
Keywords
Citation