RP-Department of Kiswahili and African Languages
Permanent URI for this collection
Browse
Browsing RP-Department of Kiswahili and African Languages by Author "Githinji, Peter"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Athari Ya Viarudhi Vya Ekegusii Kwa Kiimbo Cha Kiswahili Miongoni mwa Wanafunzi wa Shule za Upili(East African Journal of Swahili Studies, 2023-11-10) Nyougo, Christine; Githinji, PeterMakala hii inadhamiria kuonyesha athari ya viarudhi vya Ekegusii kwa matumizi ya kiimbo cha Kiswahili sanifu. Wasailiwa wetu ni wanafunzi wa shule tatu za upili zinazopatikana katika eneo la Kisii. Tulijikita katika nadharia ya Mennen (2015) ya ujifunzaji wa kiimbo katika lugha ya pili. Nadharia hii huchunguza matatizo ambayo wajifunzaji wa lugha ya kwanza hupata wakati wa kujifunza kiimbo cha lugha ya pili. Tumejikita kwa mantiki kuwa mtagusano baina ya lugha moja na nyingine huweza kuibua kufanana au kutofautiana kimatumizi katika uenezaji wa viimbo tofauti. Tumetumia mihimili minne katika uchanganuzi wa data tuliyopata nyanjani. Mhimili wa kimfumo unashughulikia vipengele vya kiarudhi katika lugha husika na usambazaji wake, mhimili wa utekelezaji unashughulikia utaratibu wa namna ambavyo vipengele mbalimbali vya kifonolojia vinavyotekeleza majukumu yavyo katika lugha husika. Mhimili wa ujirudiaji unaangazia kiwango cha matumizi ya vipengele hivi vya fonolojia ambapo lugha hutofautiana katika kiwango cha matumizi ya vipengele vyake na mhimili wa kisemantiki unaoshughuklika maana inayopatikana kutokana na matumizi ya viarudhi husiaka. Usampulishaji wa kimaksudi ulitumiwa katika kuteua wanafunzi wa vidato tofauti katika shule tatu teule na walimu wanaofunza Kiswahili katika shule hizo. Data yetu ilitokana na hojaji, mahojiano usomaji wa sentensi pamoja na kifungu ambacho kilikuwa na aina nne za viimbo ambapo wasailiwa walizisoma kwa sauti. Data ya ziada ilitokana na usomaji wa sentensi nane za Ekegusii zenye kiimbo cha taarifa, swali, amri na mshangao ambazo zilisomwa na walimu wanaozungumza Ekegusii kama lugha ya kwanza katika shule hizo tatu. Uchanganuzi wa data ulifanywa kupitia ufasili wa data ya hojaji, mahojiano na uchunzaji wa kushiriki. Matokeo tuliyopata yalibainisha kuwa uhawilisho wa viarudhi hivi kwa kiwango kikubwa huathiri matumizi sahihi ya kiimbo cha Kiswahili ambapo wasailiwa wa lugha ya kwanza hurudufu baadhi ya vipengele vya lugha hiyo katika kiimbo cha lugha ya pili. Matokeo haya pia yalidhihirisha kuwa maumbo ya silabi katika Ekegusii, shadda, toni na wakaa huathiri matumizi ya kiimbo cha Kiswahili sanifu.Item Ukiukaji wa Kanuni Bia za Greenberg katika Miundo ya Tungo Zenye Vihusishi Katika Lugha ya Kiswahili(EANSO, 2023-11) Ongwae, Jemimah Kwamboka; Githinji, PeterMakala haya yalidhamiria kubaini ukiukaji wa baadhi ya kanuni bia za Greenberg katika miundo ya tungo zenye vihusishi vya Kiswahili. Katika utafiti wake, Greenberg (1963), alipendekeza kanuni bia 45 na kutafiti lugha 30 ili kuchunguza mpangilio wa vipashio vya kiisimu katika makundi mbalimbali ya lugha. Lugha ya Kiswahili ilikuwepo mojawapo ya sampuli alizoteua. Hata hivyo, katika kuzingatia uwekaji vihusishi, inaonekana kukiuka baadhi ya kanuni hizo. Kwa hivyo, mkabala wa Greenberg (1963) ulitumika. Kanuni bia za Greenberg hasa zile zinazozungumzia vihusishi pekee zilitumika kuchanganua miundo na mazingira ya kiisimu yanayosababisha ukiukaji wa baadhi ya kanuni za Greenberg katika uwekaji wa vihusishi vya Kiswahili. Data iliyotumika ilikuwa ni tungo zenye vihusishi. Mbinu ya usampulishaji wa kimakusudi ilitumika kuteua vihusishi hivi na vilikusanywa kwa kusoma vitabu vya sarufi na makala kutoka kwenye majarida na makala ya mtandaoni. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia mkabala wa kanuni bia za Greenberg kupitia ufafanuzi wa data kwa njia ya maelezo na unukuzi wa kanuni bia za Greenberg. Ilijidhihirisha kuwa baadhi ya kanuni bia za Greenberg zina ukiushi katika lugha ya Kiswahili. Ukiushi hasa ulitokea kwa sababu sifa A haikumiliki sifa B kwa kuzingatia sheria ya uchanganuzi iliyopeanwa. Haya yalibainika hasa kwa kuwa lugha ya Kiswahili inamiliki aina mbili za vihusishi; vihusishi vya kabla ya nomino na vihusishi vya baada ya nomino katika umbo lake la nje. Hata hivyo, baadhi ya kanuni bia zingine zilionyesha utiifu. Aidha baadhi ya kanuni hizi zina utata ambao unaleta changamoto katika juhudi za kutoa kauli jumlishi. Makala haya yatachangia katika kongoo ya utaratibu wa vipashio katika sentensi, taipolojia ya lugha na sintaksia ya Kiswahili.