Dini kama chombo cha kuwadhulumu waumini: mifano kutoka fasihi katika kiswahili
Loading...
Date
2011-05
Authors
Ng'etich, Kiprugut Daniel
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia dini kama chombo cha kuwadhulumu waumini katika
fasihi andishi ya Kiswahili. Vitabu vilivyoteuliwa na kutumiwa katika utafiti ni :
Nitaolewa Nikipenda (1982), Masaibu ya Ndugu Jero (1974), Nguvu ya Sala
(1999) na Paradiso (2005). Katika sura ya kwanza ya utafiti tumetanguliza utafiti
huku tukijadili mambo yafuatayo kwa kina: utangulizi, swala la utafiti, maswali
ya utafiti, madhumuni ya utafiti, sababu ya kuchagua mada, misingi ya nadharia,
yaliyoandikwa kuhusu mada, mbinu za utafiti, upeo na mipaka ya utafiti na mbinu
za utafiti. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya udenguzi na nadharia ya
maadili.
Sura ya pili imeweka wazi namna ambavyo dini inadenguliwa kuwa chombo cha
dhuluma katika tamthilia ya Nitaolewa Nikipenda na Masaibu ya Ndugu Jero.
Katika sura ya tatu tumeeleza jinsi dini inadenguliwa kuwa chombo cha udhalimu
katika riwaya ya Paradiso na Nguvu ya Sala.
Katika sura ya nne tumefafanua aina za dhuluma za kidini na visababishi vyake.
Sura ya tano nayo imejadili athari za dhuluma na jinsi waandishi wa fasihi
wametumia mbinu za kisanaa kuunga au kupinga udhalimu wa kidini.
Tumehitimisha utafiti wetu na kutoa mapendekezo kwa tafiti zijazo katika sura ya
sita.
Data za utafiti zimekusanywa, kuchanganuliwa na kuwasilishwa kwa kuzingatia
malengo ya utafiti na nadharia teule. Uwasilishaji wa data umefanywa kwa njia ya
kimaelezo. Utafiti huu ulimulika kwa undani udhalimu wa kidini. Tulionyesha
kuwa dini ni asasi muhimu sana katika jamii. Asasi hii muhimu inaweza
kutumiwa kukuza maadili na umoja wa kijamii. Hata hivyo, baadhi ya waumini
wametumia nafasi hii kuwadhulumu wenzao. Tulionyesha kuwa ni rahisi kutumia
dini kama chombo cha udhalimu kwa sababu aghalabu binadamu hukwepa
kupinga chochote kinachohusiana na Mungu au miungu. Nadharia ya udenguzi
ilitusaidia kufafanua unafiki wa viongozi wa kidini na nadharia ya maadili ilitufaa
katika kujadili dhima ya dini miongoni mwa wanajamii.
Description
Tasnifu hii imewasillshwa katika idara ya kiswahill na lugha za kiafrika ili kutosheleza baadhi ya mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta.