Dhima ya lugha teule katika kuwasilisha taswira ya mtoto katika jamii ya abagusii tasnifu
Loading...
Date
2018
Authors
Ombaye, Robert Omuga
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza dhima ya lugha teule katika kuwasilisha taswira ya mtoto katika
jamii ya Abagusii. Malengo ya utafiti huu yalikuwa kutambua lugha iliyowasilisha taswira ya
mtoto na kubainisha dhima na athari zake katika jamii ya Abagusii. Nadharia ya Ethnografia
ya Mawasiliano iliyoasisiwa na Hymes (1964) ilitumika katika utafiti huu. Nadharia hiyo
ilifaa kwa sababu iliangazia jinsi mawasiliano yalivyochanganuliwa kwa kuzingatia
vipengele vya: mada, umbo la ujumbe, muktadha, wahusika, sababu za mawasiliano, kanuni
za ufafanuzi wa ujumbe, njia za mawasiliano na utendaji. Data ya kimsingi ilipatikana kutoka
eneo bunge la Nyaribari Chache, Ugatuzi Mdogo wa Kisii ya Kati, Kaunti ya Kisii. Aidha,
data nyingine ilikusanywa maktabani kwa kusoma vitabu, kumbukumbu, ripoti, tasnifu,
makala na majalida kuhusu mada ya utafiti. Nyanjani mtafiti alitumia sampuli iliyoteuliwa
kwa kutumia mbinu ya kimakusudi kuwahoji watu sabini na wawili. Mbinu ya makusudi
ilitumiwa kupata watafitiwa walioimudu vyema lugha ya Ekegusii kuhojiwa ili kupata
matokeo faafu. Mtafiti aliwahoji watu wawili (2) kutoka kila kikundi; watoto, vijana, watu
wazima, naibu wa machifu, machifu na wataalamu wa haki za watoto kutoka wodi sita (6) za
eneo bunge la Nyaribari Chache. Vifaa vilivyotumiwa kuwahoji ni hojaji wazi na maswali ya
mahojiano ya ana kwa ana na wahojiwa. Data iliyokusanywa ilirekodiwa na kuchanganuliwa
kwa kuzingatia maswali, malengo na nadharia ya utafiti. Matokeo ya utafiti huu
yaliwasilishwa kwa kutumia maelezo na yalibainisha kuwa, lugha hasi na chanya ilitumika
katika kuwasilisha taswira mbalimbali za watoto katika jamii ya Abagusii. Matokeo ya utafiti
huu vilevile yalibainisha kuwa dhima za lugha hiyo ni: kuelimisha, kukuza maadili, kuonya,
kurekebisha tabia, kuwasiliana, kutia motisha, kusifu, kufariji, kulinganisha, kushauri na
kukemea. Aidha, matokeo ya utafiti huu yalibainisha kuwa lugha hiyo ilizua athari kadhaa
kwa mtoto ambazo ni: kuhama kutoka nyumbani kwao, kutelekezwa, kubaguliwa, kukata
tamaa, kuchanganyikiwa akili, kuwa na tabia nzuri au mbaya, kupendwa, kukubalika na
kufurahi. Utafiti huu ulikuwa wa manufaa katika jamii ya Abagusii kwa vile uliwawezesha
kuelewa kuhusu lugha iliyowasilisha taswira ya mtoto. Ufahamu wa lugha hiyo ni muhimu
kwa vile ulichangia katika kuamua maisha ya mtoto siku za usoni. Aidha, ufahamu huo
ulichangia pakubwa katika utoaji wa mielekeo, maoni na matendo ya watu wazima kwa
watoto katika jamii ya Abagusii.
Description
Tasnifu hii imetolewa ili kutosheleza baadhi ya mahitaji ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Cha Kenyatta