Dhuluma za Kitabaka katika Riwaya za Mkamandume na Shetani Msalabani
Loading...
Date
2021
Authors
Kausi, Barasa George
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umebainisha namna masuala ya dhuluma za kitabaka yanavyojitokeza katika riwaya za Mkamandume (2004) na Shetani Msalabani (1982). Waandishi wa riwaya hizi; Said A. Mohamed na Ngugi wa Thiong’o mtawalia wametuchorea picha halisi ya namna dhuluma za kitabaka zimekithiri katika jamii wanamoishi. Katika riwaya teule, wahusika wanyonge kutoka tabaka la chini wamedhulumiwa na wahusika wa tabaka la juu kwa misingi ya kiuchumi. Hali hii imechangia utengano uliopo baina ya wahusika maskini na matajiri katika riwaya za utafiti. Malengo ya utafiti yalikuwa ni kuonyesha jinsi dhuluma za kitabaka zinavyobainika katika riwaya teule, kubainisha athari zake kwa wahusika na kuchunguza mbinu wanazotumia wanyonge kujikomboa na kujiimarisha kimaisha. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Uhakiki wa ki-Marx ambayo iliasisiwa na Karl Marx na Engles (1959). Nadharia hii inaeleza kuwa historia ya maisha ya binadamu inaweza kuelezeka katika misingi yakinifu ya kiuchumi ambayo huchunguza njia kuu za uzalishaji na usambazaji mali. Tabaka la juu lenye watu wachache huwa na uwezo mwingi kiuchumi kuliko tabaka la chini lenye watu wengi wasiomiliki mali. Pia huonyesha namna jamii huimarika kutokana na migogoro ya kitabaka baina ya watu wa tabaka la chini dhidi ya wale wa tabaka la juu. Utafiti huu uligundua kwamba riwaya za Mkamandume na Shetani Msalabani zimeonyesha kwa undani namna tabaka nyonyaji linavyowanyonya wachochole wa tabaka la chini. Riwaya hizi zimebainisha suala la kiuchumi kama chanzo cha dhuluma zinazowakumba wahusika wanyonge. Aidha, dhuluma hizi zimesababisha athari chungu nzima katika tabaka la walalahoi. Vilevile, utafiti huu umebainisha kuwa wanyonge katika riwaya teule wanaungana na kujikomboa kiuchumi, kisiasa na kielimu. Mbinu walizotumia kupigania ukombozi ni: maandamano, migomo kazini, kuelimika kimasomo, uandishi wa vitabu vya fasihi na kuanzisha biashara ili kujikimu kimaisha. Utafiti huu utawazindua wahusika wanyonge kujikomboa dhidi ya dhuluma za kitabaka katika jamii.
Description
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Novemba, 2021
Keywords
Dhuluma, Kitabaka, Riwaya, Mkamandume, Shetani Msalabani