Uhalisiajabu katika riwaya ya babu alipofufuka (2001) ya S.A mohamed na bina-adamu! (2002) yA K.W Wamitila
Loading...
Date
2004-08
Authors
Magaju, Jacinta Kagendo
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia swala la uhalisiajabu katika riwaya teule za fasihi ya Kiswahili.
Riwaya zilizohakikiwa ni Babu Alipofufuka (2001) ya S.A. Mohamed na Bina-Adamu!
(2002) ya K.W. Wamitila. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni kitengo kimoja cha mwelekeo
wa usasaleo. Hii ni nadharia ya uhalisiajabu. Katika nadharia ya uhalisiajabu, matukio
yanasawiriwa kiajabuajabu, ni ya kuogofya na kutisha. Matukio haya huashiria hali halisi ya
maisha katika jamii. Uhalisiajabu ni mtindo wa riwaya wa hivi majuzi unaopiku njia za
kimapokeo za uandishi wa fasihi ya Kiswahili na usawiri wa jamii. Kimapokeo, riwaya
inapaswakujengeka katika misingi ya uhalisia.
Tasnifu hii ina jumla ya sura tano. Sura ya kwanza ni utangulizi wa utafiti. Hapa ndipo
tumeshughulikia mada ya utafiti, malengo ya utafiti, sababu za kuchagua mada na
yaliyoandikwa kuhusu hii mada. Aidha, tumejadili upeo wa utafiti huu na misingi ya
nadharia iliyouongoza. Mwisho, mbinu za utafiti zimeelezwa.
Sura ya pili imejadili maisha ya waandishi S.A. Mohamed na K.W. Wamitila. Tumeonyesha
vipindi mbalimbali vya uandishi wao. Uchunguzi huu umedhamiria kuonyesha mitindo
waliyoitumia tangu waanze kuandika na pia kuonyesha ni kwenye kipindi gani cha uandishi
waliingilia uandishi wa kihalisiajabu na kwa nini walifanya hivyo.
Sura ya tatu na nne zinachunguza jinsi riwaya za Babu Alipofufuka na Bina-Adamu!
zimetumia uhalisiajabu katika kuwasilisha ujumbe. Tumeonyesha mihimili ya nadharia ya
uhalisiajabu waliyoitumia. Mihimili hii ni pamoja na matukio ya kiajabuajabu, ndoto na
uhalisia, uduara wa wakati, visaasili, uvunjwaji wa mipaka ya mahali na upekee wa mtindo
wa riwaya ya kihalisiajabu. ,;~
Sura ya tano imehusika na kulinganisha na kulinganua riwaya zote mbili kwa mujibu wa
mada husika. Aidha, matokeo ya utafiti, matatizo yaliyokabiliwa katika utafiti na
mapendekezo yametolewa katika sura hii.
Kutokana na utafiti huu, imebainika wazi kwamba Mohamed na Wamitila wanatumia
uhalisiajabukimakusudi. Mihimili mikuu ya uhalisiajabu imo katika kazi zao. La maana zaidi
ni kwamba wanatumia uhalisiajabu kama mkakati unaowawezesha kujadili maswala
yanayousibu ujirani wetu. S.A. Mohamed anatumia mkakati huu kumulika rnatatizo ya
kiuchumi na ya kijamii yanayowakabili Waafrika kutokana na utawala finyu wa viongozi
wao. K.W. Wamitila anatumia mtindo huo huo kuupiga vita utandaradhi na ubepari wa
kimataifa. Pamoja na kuonyesha matatizo yanayoyakabiliwa na Waafrika, Mohamed na
Wamitila wana imani kwamba matatizo ya Waafrika yanaweza kutatuliwa si kwa kutafuta
tiba huko nje katika mataifa ya Kimagharibi, bali kwa kuyatafuta humuhumu barani Afrika
kihalisiajabu.
Description
Tasnifu hii imetolewa iIi kutosheleza baadhi ya mahitaji ya Shahada
ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Agosti 2004
Keywords
Mohamed, S.A., Babu alipofufuka, Wamitila, K.W., Bina-adamu, History and criticism