Makosa Ya Kiisimu Ya Wanafunzi Wanaojifunza Kiswahili Kama Lugha Ya Pili: Uchunguzi Kuhusiana Na Lahaja Ya Kigichugu
Loading...
Date
2024-10
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Binadamu wanahitaji lugha ili kuwasiliana na mojawapo ya lugha maarufu ulimwenguni ni Kiswahili. Kiswahili kimetafitiwa na wataalamu wengi ili kutafuta suluhisho la baadhi ya changamoto zinazokumba lugha hii na kuiboresha. Mojawapo ya changamoto na suala ambalo halijatafitiwa na utafiti huu ulikusudia kuchunguza ni makosa ya kiisimu ya wanafunzi wanaojifunza Kiswahili kama lugha ya pili: Uchunguzi kuhusiana na lahaja ya Kigichugu.Wataalamu ambao wamechunguza masuala ya Kigichugu wameshughulikia masuala mengine tofauti na hili kama vile Kamau (1996) aliyelinganisha michakato ya kifonolojia ya lahaja hii na ya Kindia, Ruri (2011) anayelinganisha vitamkwa vya konsonanti za Kindia na Kigichugu. Naye Gituru (2019) anaangazia unyambulishaji wa vitenzi katika Kigĩchũgũ, Iribe (2012) anachunguza mbinu tofauti za kifonolojia zinazotumika katika kutohoa maneno ya Kiswahili yanapoingia katika Kigichugu na Ndung’u (2022), aliyefanya utafiti kati ya wanajamii wanaozungumza lahaja ya Kindia na wale wanaozungumza Kigichugu kuhusu mitazamo ya lugha na utambulisho wa kijamii. Utafiti huu ulitumikiza kanuni na mihimili ya nadharia ya Sintaksia Finyizi ili kuweka wazi makosa ya kisintaksia na kisemantiki yanayofanywa na wanagenzi wa Kigichugu wanapojifunza Kiswahili kama L2. Uchunguzi huu uliendelezwa nyanjani na maktabani. Nyanjani ulitekelezwa katika shule za sekondari za kutwa katika kaunti ndogo ya Gichugu. Katika utafiti huu tulipaswa kuteua shule, na wanafunzi wa kufanyia utafiti. Katika uchaguzi wa shule za kutwa za kufanyia utafiti tulitumia mbinu ya sampuli kimaksudi. Katika uteuzi wa wanafunzi tulitumia usampulishaji wa kinasibu pale ambapo tulipatia wanafunzi nambari kinasibu na kuteua waliopata nambari moja hadi sita. Data ya utafiti huu ilikusanywa kwa kutumia hojaji, insha na masimulizi. Data ya utafiti iliwasilishwa kupitia majedwali na maelezo. Matokeo ya utafiti huu yalidhihirisha kuwa wengi wa wanafunzi katika shule za upili za kutwa katika eneo la Gichugu hujifunza Kigichugu kama lugha yao ya kwanza. Isitoshe, wengi huanza kutumia Kiswahili wanapojiunga na shule. Licha ya hilo, makosa ya kisintaksia na kisemantiki yaliyotokana na lahaja ya Kigichugu yalijitokeza katika utafiti huu. Makosa haya yalichanganuliwa kwa kutumia nadharia ya Sintaksia Finyizi na kudhihirisha ukiukaji wa kanuni za nadharia hii. Aidha utafiti huu ulibainisha vyanzo vya makosa haya ambavyo vinaegemea kwa kiasi kikubwa kwa L1.Vyanzo hivi ni: uhamishaji wa mifumo ya kiisimu, tafsiri sisisi na ujumlishaji mno. Ili kupunguza makosa haya, mikakati mbalimbali ilibainishwa; ufundishaji kwa mwelekeo wa uchanganuzi linganuzi,walimu kutangamana na wanafunzi, wanafunzi kukosoana na kutahadharisha wanafunzi dhidi ya tafsiri za moja kwa moja kutoka L1.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa Ili Kutimiza Baadhi Ya Mahitaji Ya Shahada Ya Uzamili Ya Kiswahili Katika Chuo Kikuu Cha Kenyatta, Oktoba 2024.
Msimamizi:
1.David Kihara