Athari za Ekegusii Katika Matumizi ya Kiimbo cha Kiswahili Miongoni mwa Wanafunzi wa Shule za Upili Kaunti ya Kisii, Kenya
Loading...
Date
2023-11
Authors
Nyougo, Christine
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza matumizi ya kiimbo cha Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wanaozungumza Ekegusii kama lugha ya kwanza. Shule tatu zilihusishwa katika utafiti huu: Shule ya upili ya Senior Chief Musa Nyandusi, Nyamondo na Nyabisia. Malengo ya utafiti huu yalikuwa: Kutathmini utamkaji na ufasili wa kiimbo cha Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wanaozungumza Ekegusii kama lugha ya kwanza, kuchunguza jinsi viarudhi vya lugha ya Ekegusii vinavyoathiri kiimbo cha Kiswahili. Kutathmini jinsi usuli wa lugha na tajriba ya wanafunzi inavyochangia matumizi bora ya kiimbo katika uzungumzaji wa Kiswahili. Ili kuafiki madhumuni haya, maswali yafuatayo yalitumiwa: Je, wazungumzaji wa Ekegusii hufasili vipi kiimbo cha Kiswahili sanifu? Viarudhi vingine vya Ekegusii huathiri kiimbo cha Kiswahili vipi? Usuli na tajriba ya wanafunzi huchangia vipi katika matumizi bora ya kiimbo cha Kiswahili? Nadharia ya ujifunzaji wa kiimbo cha lugha ya pili iliyoasisiwa na Mennen (2015) ilitumiwa katika kuchunguza matumizi ya kiimbo. Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Maktabani ulihusu kusoma matini, vitabu, tasnifu, majarida na makala mtandaoni kuhusu kiimbo. Nyanjani ulijumuisha matumizi ya hojaji funge na wazi katika kupata tathmini ya wanafunzi ya sampuli ya data waliyopewa na mtafiti. Vilevile, mbinu ya mahojiano ambayo yalirekodiwa ilitumika kwa walimu wanaofunza Kiswahili. Pia, uchunzaji wa kushiriki ulitumiwa. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya maelezo, majedwali, michoro na chati. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa lugha ya Ekegusii huathiri matumizi ya kiimbo sahihi cha Kiswahili. Wazungumzaji wa Ekegusii walionyesha athari katika usomaji na ufasili wa kiimbo cha Kiswahili. Ilibainika kuwa viarudhi vingine vya Ekegusii huathiri matumizi ya kiimbo cha Kiswahili. Utafiti ulithibitisha kuwa jinsia huchangia katika matumizi sahihi ya kiimbo ambapo ilidhihirika kuwa jinsia ya kike hutumia kiimbo sahihi katika mazingira rasmi ikilinganishwa na jinsia ya kiume. Tajriba pia huchangia kiimbo sahihi pale ambapo wanafunzi ambao wamekuwa shuleni kwa muda mrefu huzungumza kwa kiimbo bora. Vifaa vya kisasa pia huchangia kuboresha matumizi ya kiimbo sahihi cha Kiswahili. Tunapendekeza walimu wakuze matumizi ya vifaa vya kisasa katika ufundishaji wa kiimbo cha Kiswahili, kuwepo sheria shuleni kuhusu matumizi ya Kiswahili katika mazingira rasmi na ufundishaji wa kiimbo utiliwe maanani kuanzia viwango vya chini vya elimu.
Description
Idara ya Kiswahili na Lugha za Kiafrika Chuo Kikuu cha Kenyatta Tasnifu Hii Imewasilishwa kwa Ajili ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Idara ya Kiswahili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Novemba, 2023
Keywords
Athari, Ekegusii, Matumizi, Kiimbo, Kiswahili, Miongoni, Wanafunzi, Shule, Upili, Kaunti ya Kisii, Kenya