Tathmini ya mpango wa kisintaksia wa ngeli za nomino za Kiswahili: ufunzaji shule za Nairobi
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia tathmini ya mpangilio wa kisintaksia wa ngeli za nomino za Kiswahili. Utafiti huu ulilenga kuonyesha matatizo yaliyopo katika mipangilio ya zamani ya kufunzia ngeli, kueleza mpangilio wa kisintaksia na kuchunguza iwapo mpangilio huu umeweza kutatua matatizo yanayojitokeza katika mipangilio ya kimofolojia na kisemantiki. Mada hii ilichaguliwa kwa sababu ya mabadiliko ya mitalaa ya mitalaa ya kufunza mada ya ngeli katika shule nchini Kenya. Mabadiliko haya yalitokea kwa sababu ya utata ambao ulikuwepo katika mipangilio ya wali ya ngeli. Hivyo utafiti huu ulinuia kudhibitisha iwapo utata na matatizo yaliyodaiwa kuwepo katika mipangilio ya kimofolojia na kisemantiki yameondolewa na mpangilio huu wa kisintaksia. Aidha, imeziba pengo la kuonyesha kama bado kuna matatizo yanayokumba somo la ngeli shuleni. Kadhalika, kulikuwa na haja ya kuchunguza chanzo cha matatizo ya wanafunzi katika sarufi hasa maendelezo ya sentensi sahihi. Ili kufanikisha malengo ya utafiti, insha na sentensi walizotunga wanafunzi kutoka katika baadhi ya shule za Nairobi, zimehakikiwa ili kuona utenda kazi wa mpangilio wa sintaksia. Maoni ya walimu kupitia hojaji yaliweza kuonyesha mpangilio wanaopendelea zaidi na matatizo yanayowakumba katika ufunzaji wa ngeli. Matokeo ya kazi za wanafunzi zimeonyesha kuwa wanafunzi bado wana matatizo katika kuendeleza sentensi sahihi kisarufi kutokana na kukanganywa kwao na mambo kama vile vitambulishi vya ngeli na kutoelewa maana ya nomino