Motifu za Yatima Katika Hadithi Teule za Watoto
Abstract
Utafiti huu umechanganua motifu za yatima katika fasihi andishi ya watoto ukitumia
hadithi teule za watoto. Utafiti unalenga kubainisha hali zinazochangia watoto kuwa
yatima katika hadithi teule za fasihi ya watoto. Pia, utafiti umewezesha kuelewa
changamoto zinazowakumba watoto yatima katika jamii. Vilevile utafiti umenuia
kuonyesha jinsi mtoto yatima anavyojiopoa kutokana na changamoto zinazomkumba.
Nadharia changamano ya vikale iliyoasisiwa na Northrop Frye (1950-1954) na Nadharia
ya Uhalisia iliyoasisiwa na Georg Hegel na kuendelezwa na Lukacs (1972) na Larkin
(1977) imetumika katika utafiti huu. Mihimili yake imetumika kama dira ya kuongoza
utafiti huu katika kuyaafiki malengo yake. Utafiti unakusudia kuhusisha vitabu teule
vilivyoandikwa na waandishi tofauti tofauti. Vitabu ambavyo vimerejelewa ni pamoja na:
Mama wa Kambo (Kisovi, 2005), Yatima (Wamitila, 2006) na Mateso ya Johari (Ng’ang’a,
2006). Vitabu hivi vimeteuliwa kwa kutumia mbinu kusudio. Pia, vimeshughulikia
mhusika yatima kama kikale na mbinu ya kuwasilisha ujumbe katika fasihi ya watoto.
Utafiti umejikita maktabani ambamo vitabu, majarida, magazeti, machapisho na tasnifu
mbalimbali zimesomwa ili kuupa msingi utafiti. Data iliyopatikana imechanganuliwa na
matokeo yakawasilishwa kwa njia ya maelezo na mifano kutolewa kwa kuzingatia malengo
ya utafiti. Muhtasari umefanywa baadaye na kutolewa kimaelezo. Utafiti huu umebaini
kuwa yatima hupitia maisha yaliyo na matatizo mengi na ya aina mbalimbali. Hata hivyo,
utafiti huu pia umebaini kuwa watoto yatima huweza kujiopoa kutokana na matatizo haya
kupitia kwa juhudi zao za kibinafsi kama vile kuiombea hali yao, kukumbana na matatizo
haya kwa ujasiri wao na hata kufanya bidii ili kujiopoa na hali hizi ngumu wanazokumbana
nazo. Kwenye ngazi ya kijamii, watoto yatima huweza kuopolewa na jamaa na hata
marafiki. Hali hizi za maisha pamoja na njia wanazotumia kujiopoa yatima hawa
zinaambatana na hali ya maisha kwa mtazamo wa nadharia zilizoongoza utafiti huu.
Kutokana na haya yote, utafiti huu umependekeza utafiti zaidi juu ya masuala ya maisha
ya watoto yatima kwa kuzingatia aina nyingine za fasihi kama vile ushairi, tamthilia na
hata hadithi fupi. Pia, imependekezwa kuwa utafiti zaidi uweze kufanywa kule nyanjani
kando na huu uliozingatia utafiti wa maktabani.