Nafasi ya mshikamano katika kukuza maudhui katika insha za wanafunzi wa kidato cha nne katika Kaunti ya Murang’a
Abstract
Utafiti huu ulitekelezwa kwa madhumuni ya kuchunguza nafasi ya mshikamano
katika kukuza maudhui katika insha za wanafunzi wa shule za upili. Mtafiti
alichunguza matatizo yanayohusiana na mshikamano pekee katika insha za
wanafunzi wa shule za viwango mbalimbali; wilaya, kaunti na taifa. Wanafunzi
lengwa ni wa kidato cha nne wa kaunti ya Murang’a. Kusudi la kuchunguza
matatizo yanayohusiana na mshikamano lilikuwa kubainisha chanzo cha matatizo
hayo kwa madhumuni ya kupendekeza mbinu mwafaka zinazoweza kutumiwa na
walimu pamoja na wanafunzi ili kuimarisha ufunzaji na uandishi wa insha.
Nadharia zilizoongoza utafiti huu ni nadharia za Sarufi Zalishi na Sarufi Amilifu
Mfumo. Nadharia ya Sarufi Zalishi ilisaidia katika kutathmini ung’amuzi na
matumizi ya vipengele vya mshikamano katika insha za wanafunzi. Nadharia ya
Sarufi Amilifu Mfumo ilisaidia katika kudondoa na kuchanganua maudhui. Utafiti
ulifanyiwa nyanjani pamoja na maktabani. Uteuzi wa sampuli kimakusudi
ulitumiwa na shule sita zikachaguliwa. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa
kuainisha mada tofauti tofauti kulingana na malengo ya utafiti kisha kuwekwa
kwenye majedwali na vielelezo. Uchanganuzi ulitumia mihimili ya umilisi na
utendaji ya Sarufi Zalishi na ya maana tambuzi, maana husishi na maana
matinishi ya nadharia ya SAM. Mahitimisho yalionyesha kuwa matatizo ya
mshikamano huathiri ubora wa insha za wanafunzi. Utafiti huu unanuia kuwafaidi
wanafunzi, walimu watafiti na watahini.