Uchanganuzi wa methali za kiswahili: mtazamo wa kiudenguzi
Loading...
Date
2015
Authors
Murithi, Moses Murega
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umezichanganua methali za Kiswahili kwa mtazamo wa kiudenguzi. Utafiti
huu umefanywa ikizingatiwa kuwa maana za matini hujiahirisha kwa ambavyo hakuna
matini iliyo na maana moja. Sababu kuu ya kuchagua mada hii ilikuwa kubainisha kuwa
baadhi ya methali za Kiswahili zina dhima hasi kwa jamii kinyume na dhana ya kijumla
kuwa methali zote zina dhima chanya ambayo ndiyo tu imekuwa ikiangaziwa. Kwa
misingi hii, malengo ya utafiti huu yamekuwa kutambua miktadha ya matumizi ya
methali za Kiswahili zenye dhima hasi, kuziainisha methali za Kiswahili zenye dhima
hasi kutegemea uhasi wake na kutambua manufaa ya methali za Kiswahili zenye dhima
hasi kwa jamii. Utafiti huu umeongozwa na nadharia ya Udenguzi. Nadharia ya Udenguzi
iliufaa utafiti huu kwa kuwa inawiana na lengo kuu la utafiti ambalo ni kuonyesha kuwa
baadhi ya methali za Kiswahili zina maana hasi; maana hii inaweza kupatikana tu kwa
kuzidengua. Data zilizotumika katika utafiti zilikusanywa maktabani ambapo kupitia
usomaji methali za Kiswahili zinazopatikana katika kamusi mbalimbali za methali
zilihakikiwa kwa makini na kubainisha dhima iliyomo; yaani uchanya au uhasi wake.
Baada ya data (methali zenye dhima hasi) kukusanywa ziliainishwa kulingana na ujumbe
uliomo kisha zilichanganuliwa kutegemea ujumbe husika na hususan kuzingatia dhima ya
methali husika. Matokeo ya utafiti yamebainisha kuwa methali zenye dhima hasi kama
kuchochea vita, kudharau wanyonge, kuvunja moyo, kudhihaki ulemavu na zenye
ubaguzi wa kikabila, kiuana na kiumri zipo. Matokeo ya utafiti yamewasilishwa kwa
kuzingatia malengo ya utafiti na nadharia teule. Utafiti huu umegawika katika sura tano
ambazo ni utangulizi uliochukua sura ya kwanza huku muktadha wa matumizi ya methali
zenye dhima hasi ikichukua sura ya pili. Sura ya tatu inahusisha uchanganuzi wa methali
za Kiswahili zenye dhima hasi kwa misingi ya nadharia ya Udenguzi. Aidha, sura ya nne
imejikita katika uchunguzi wa manufaa ya methali zenye dhima hasi zilizochanganuliwa
katika sura ya tatu kwa jamii huku sura ya tano ikibeba hitimisho na mapendekezo kwa
utafiti zaidi.
Description
Tasnifu hii imewasilishwa katika idara ya kiswahili ili kutosheleza sehemu ya mahitaji ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, 2015