Maigizo kama mbinu ya maudhui katika riwaya mbili za Ken Walibora
Loading...
Date
2008-04
Authors
Ochenja, Rajab
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia maigizo kama mbinu ya maudhui katika riwaya
mbili za Ken Walibora. Riwaya zilizoshughulikwa ni Ndoto ya Amerika,
(2001) na Kufa Kuzikana, (2003). Utafiti huu uliongozwa na nadharia mseto
za uhalisia na uigizaji. Nadharia hizi zilifaa katika utafiti huu hasa
ikizingatiwa ya kwamba riwaya zilizotafitiwa zimesheheni matukio mengi
ambayo yanaakisi mambo yanayotokea katika maisha ya kawaida.
Kutokana na utafiti huu, imebainika kuwa riwaya za Walibora zilizotafitiwa
zina sifa za kitamthilia. Mwandishi ametumia mbinu mahsusi za maigizo
ambazo zimezifanya riwaya hizi kubainika kama tamthilia.
Kwanza, mwandishi amewashirikisha wahusika wake zaidi katika kutenda na
kusema, kuliko kusema pekee. Vitendo vyao vimeandamana na mazungumzo.
Haya yanaonekana kupitia wahusika kama Isaya, Madoa na 'Rock Mwamba'
au Zablon Okutoyi katika Ndoto ya Amerika (2001); na Akida, Tim na Tamari
katika Kufa Kuzikana (2003).
Utafiti pia umebainisha kuwa katika kuzifanya riwaya zake zibainike kama
tamthilia, Walibora amewafanya wahusika wake wote kuwa binadamu halisi
wanaowasiliana moja kwa moja. Jambo hili limeyapa masimulizi yake uhai na
uhalisi zaidi kiasi cha kuonekana kama maigizo.
Katika matukio mengi, mwandishi amewafanya wahusika wake wawasiliane
wakitumia wakati uliopo, jambo ambalo linatoa taswira ya uigizaji. Kupitia
utafiti, imebainika pia kuwa riwaya za Walibora zilizotafitiwa zimebeba
wahusika wa kila umri na jinsia; hili ni jambo la kawaida katika maisha halisi
kwa sababu linaakisi hali inayopatikana katika maisha ya kila siku; na maisha
ni maigizo.
Utafiti pia umebainisha kuwa mwandishi ametumia mabadiliko ya mandhari
katika riwaya zilizohakikiwa ili kujenga taswira ya uigizaji. Mandhari
yamebadilishwa ili kuafiki mada iliyohusishwa katika mazungurnzo baina ya
wahusika. Kupitia riwaya hizi, kuna mandhari ya shule, ofisi, mahakama,
sokoni na hata kituo cha polisi. Hili ni sawa na jukwaa ambalo hupatikana
katika maigizo. Kubadilika kwa mandhari kila mara kunaweza
kukamithilishwa na mabadiliko yanayotokea jukwaani katika michezo ya
kuigiza ili kuashiria kumalizika kwa onyesho moja na kuanza kwa onyesho
lingine.
Utafiti umebainisha vile vile kuwa maudhui yanayoshughulikiwa katika kazi
za Walibora yamechangia pakubwa kuzifanya zikaonekana kama maigizo.
Maudhui ya uhalifu, ukabila, ubinafsi na ukatili yamewasilishwa kwa hadhira
kupitia maigizo ya moja kwa moja ya wahusika mbalimbali.
Utafiti huu utakuwa na mchango ufuatao; kwanza, umetuonyesha kuwa inafaa
tuwe na mtazamo tofauti na vigezo vingine vya kuzihakiki riwaya badala ya
kuselelea katika mitazamo ya kijadi iliyokuwa ikichukulia riwaya kama
utanzu mahsusi unaojitosheleza. Kupitia utafiti hull, imebainika kuwa riwaya
za WaIibora zilizotafitiwa zina pia sifa za kitamthilia.
Mchango mwmgme ni kuwa, baada ya utafiti, imebainika kuwa riwaya
yoyote inaweza pia ikawa na sifa za kitamthilia kama ilivyobainika katika
riwaya za Walibora zilizotafitiwa.
Utafiti huu pia ni miongoni mwa kazi chache ambazo zimewahi kuhakiki
baadhi ya kazi za Walibora kwa mtazamo tofauti. Kazi hizo zimehakikiwa
kama zinazobeba sifa mseto za tanzu mbaIimbali na kutofautiana na mitazamo
ya awali iliyochukulia tanzu tofauti za fasihi andishi kama zinazojitosheleza.
Kwa hivyo, utafiti huu utawapatia wasomi wengine wa kazi za fasihi ya
Kiswahili barabara tofauti za kufuata wakiwa katika safari ya kusaka mengi
zaidi katika taaluma hii.
Description
Tasnifu hii imetolewa ill kutosheleza baadhi ya mahitaji ya Shahada ya Uzamili ya Chuo Kikuu cha Kenyatta