Vichekesho vya Machang'i na Kihenjo: mtazamo wa sanaa ya ubwege

Loading...
Thumbnail Image
Date
2011-11-03
Authors
Njue, P. Mwaniki
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia Sanaa ya Ubwege inavyodhihirika katika sanaa za Kiafrika. Hasa, utafiti huu umehusu kuwepo kwa Sanaa ya Kibwege katika futuhi ya kitashtiti ya papo kwa hapo. Katika kutekeleza lengo hilo, mtafiti ameteua vichekesho vya Kikikuyu vya machale `Machang'i' na `Kihenjo'. Vichekesho hivyo ni `Mundurume ni Mugambo' (2001) cha `Machang' i' na `Kiama Kia Ng'ombe ' (2006) cha `Kihenjo'. Utafiti huu uliongozwa na nadharia mseto. Nadharia zenyewe ni ile ya Nadharia ya Same ya Ubwege na Uchanganuzi Usemi Kihakiki. Nadharia hizi ziliafiki hasa ikizingatiwa kuwa utafiti huu umeshughulikia jinsi lugha inavyotumika katika masuala ya kifasihi. Baadhi ya mihimili tu ya nadharia husika ndiyo iliyotumika kuchanganulia vichekesho teule. Mihimili mahsusi tu ya Nadharia ya Uchanganuzi Usemi Kihakild ilitumiwa katika azma ya kubainisha vipengele anuwai vya mnaa za kibwege. Tasnifu hii imegawanywa katika faslu tano. Faslu ya kwanza imeshughulikia mada ya utafiti, malengo ya utafiti na sababu za kuchagua mada husika. Vile vile, imegusia upeo, udurusu wa maandishi yanayohusu mada ya utafiti, misingi wa nadharia pamoja na mbinu. Faslu ya pili imetalii historia, usuli na kazi za machale teule `Machang'i' na `Kihenjo'. Maisha yao kabla na katika uigizaji wao yameshughulikiwa yakihusishwa na mada ya utafiti. Aidha, sura hii imetoa muhtasari wa kazi zao zilizotolewa katika kanda hadi kuanza kwa utafiti huu. Maelezo jumla na uchunguzi kwa kina wa kichekesho `Mundurume Ni Mugambo ' (2001) cha Machang'i upo katika sura ya tatu. Pia, sura hii ilishirikisha tathmini ya sanaa ya kibwege katika maudhui ya maisha ya kijamii yaliyosheheniwa kichekeshoni. Sura ya nne imehakiki vipera anuwai vya sanaa ya kibwege kupitia maudhui ya kisiasa katika kichekesho `Kiama Kia Ng'ombe' (2006) cha `Kihenjo'. Faslu ya tano ni hitimisho linalotoa muhtasari wa tasnifu nzima na matokeo ya utafiti. Vile vile, matatizo na mapendekezo ya tafiti za baadaye yametolewa katika sura hii. Utafiti huu umebainisha ithibati tosha za kuwepo kwa ubwege kupitia vipera mbalimbali vya Sanaa ya Ubwege. Mathalani, sura za Maigizo ya Ubwege kama vile muundo-bwege, mbinu na lugha-bwege, uhusika bwege, hali-kinzani, unyume na ubatili wa maisha zimejidhihiri. Utafiti umechangia kubainisha kuwa ipo tofauti baina ya sanaa ya ubwege uliojidhihiri katika vichekesho husika na ule ulioasisiwa kule Uropa. Wasanii hawa wa Kiafiika wanasheneza maudhui mazito katika mzaha na ubwege wa vichekesho vyao. Ubwege na kuburudisha kwenyewe kunatumiwa tu kama njia ya kuwasilishia maudhui nyeti na ibuka katika jamii. Hatimaye, utafiti huu utawezesha kazi za machale hawa kukia mpaka finyu wa kikabila. Utafiti huu ndio wa kwanza kiakademia kufanyiwa machale hawa wa fituhi mujarabu kwa lugha ya Kikikuyu. Kutafsiriwa na kunukuliwa kimaandishi kwa Kiswahili, kunaziwezesha kushughulikiwa kiakademia na wasomi katika kiwango cha kimataifa. Hata kuigizwa, sasa kunawezekana na wasaii wasiokifahamu Kikikuyu, iwe ni katika Afrika Mashariki au kwingineko ulimwenguni
Description
Keywords
Citation