Tathmini ya Ufunzaji Matamshi ya Kiswahili Katika Shule za Upili Kaunti ya Murang’a Kenya

Loading...
Thumbnail Image
Date
2021
Authors
Gatuthu, Muiga Harrison
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Mahitaji ya silabasi mpya ya Kiswahili (2006) kwa shule za upili hupendekeza ufunzaji wa mada za sauti na matamshi. Suala la matamshi ya lugha, linahusika na matawi ya fonetiki na fonolojia. Matawi ya fonetiki na fonolojia ya lugha yoyote ile hujenga msingi wa matawi mengine ya lugha husika. Watahiniwa wa K.C.S.E. wamekuwa wakiripoti matokeo mabaya katika karatasi ya lugha 102/2 mwaka baada ya mwaka. Mojawapo ya vipengele vinavyotahiniwa katika karatasi hii ni mada za sauti na matamshi bora. Aidha, ilikisiwa kuwa mojawapo ya sababu za wanafunzi wengi kutojieleza vizuri kwa lugha sanifu ya Kiswahili ni kukosa msingi bora wa fonetiki na fonolojia. Hivyo basi kulikuwa na haja kubwa ya kutathmini kwa undani hali halisi ya ufunzaji wa matamshi katika shule za upili nchini Kenya. Malengo ya utafiti yalikuwa kutathmini yanayofunzwa katika shule za upili kuhusu sauti na matamshi ya Kiswahili, kubainisha mbinu za ufunzaji sauti na matamshi katika shule za upili na kuchunguza changamoto katika ufunzaji wa mada za matamshi ya Kiswahili katika shule za upili. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya fonolojia zalishi iliyoasisiwa na Chomsky na Halle (1968). Nadharia hii imebainisha sauti za lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia kipengele cha uwilisifa. Vile vile, nadharia ya utabia iliyoasisiwa na Skinner (1957) ilitumika kushughulikia suala la ufundishaji wa matamshi ya Kiswahili. Utafiti wa maktabani na wa nyanjani ulizalisha data kuhusu mbinu na changamoto za ufunzaji sauti na matamshi katika shule za upili. Uteuzi wa sampuli ulikuwa wa kimaksudi ambapo shule kumi na nne; mbilimbili katika kila kaunti ndogo zilizoko katika kaunti ya Murang’a ziliteuliwa. Wanafunzi sita na walimu wawili wawili kwa kila shule waliteuliwa kuunda sampuli ya watafitiwa 112. Mbinu za hojaji, na mazoezi kwa wanafunzi zilitumiwa kukusanya data. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kimaelezo, kwa njia ya majedwali na michoro duara. Uchanganuzi wa kitakwimu ulifanyika kwa kutumia mbinu ya tarakilishi ya uchanganuzi tarakimu sayansi za kijamii. Utafiti huu uligundua kuwa, ufunzaji matamshi ya Kiswahili umetiliwa uzito zaidi katika vidato vya chini (kidato cha kwanza na kidato cha pili) na kupuuzwa katika vidato vya juu (kidato cha tatu na kidato cha nne). Aidha, uzoefu wa kutosha wa mada za matamshi ya Kiswahili haukubainika katika silabasi ya Kiswahili kutoka kidato kimoja hadi kingine. Utafiti huu vile vile ulibaini changamoto mbalimbali katika ufunzaji na ujifunzaji wa matamshi ya Kiswahili kama vile, mielekeo hasi ya walimu na wanafunzi kuhusu mada za matamshi ya Kiswahili, wanafunzi kuathiriwa na lugha zao za kwanza, ukosefu wa vifaa muhimu vya kufunzia matamshi kama vinasa sauti na athari za lugha ya sheng’ kwa wanafunzi. Utafiti huu ulihitimisha kwa kupendekeza marekebisho ya silabasi ya Kiswahili katika mada za matamshi ya Kiswahili ili kuwe na mwendelezo wa yanayofunzwa kuhusu matamshi ya Kiswahili kutoka kidato kimoja hadi kingine. Utafiti huu utawafaa wakuzaji mitaala kwani watabaini changamoto zinazokumba ufunzaji wa sauti na matamshi ya Kiswahili na kufanya marekebisho yanayohitajika. Aidha walimu na wanafunzi, wahadhiri pamoja na vyombo vya utangazaji vitafaidika kwa njia za kuandaa wanafunzi na walimu wa lugha kuhusu mbinu mwafaka za ufunzaji sauti na matamshi ya Kiswahili.
Description
Tasnifu hii Imetolewa kwa Madhumuni ya Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Mei, 2021
Keywords
Tathmini, Ufunzaji Matamshi, Kiswahili, Shule za Upili, Kaunti ya Murang’a, Kenya
Citation