Mwananchi wa kawaida kama mdhulumu wa maslahi yake katika tamthilia za Kilio Cha Haki, Amezidi na Mstahiki Meya.

Loading...
Thumbnail Image
Date
2018-03
Authors
Omoga, Ronic Gaddafi
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichanganua kazi za Al- Amin Mazrui, Timothy Arege na Said Ahmed Mohamed ambazo ni tamthilia za Kilio cha Haki (1981), Mstahiki Meya (2009) na Amezidi (1995) mtawalia. Kazi hizi zililenga kumsawiri mwananchi wa kawaida kama chanzo cha dhuluma dhidi yake. Kwa kutumia sifa mbalimbali za wahusika, kazi hizi zinaangazia maisha ya wananchi katika nchi zinazoendelea hasa katika kipindi cha ukoloni na baada ya ukoloni. Utafiti huu unapania kuonyesha kuwa shida wanazokumbana nazo wananchi katika mataifa yanayoendelea zinatokana na wananchi wenyewe. Kwa hivyo, utafiti umebainisha baadhi ya matendo wanayoshiriki wananchi ambayo yanawafanya wajidhulumu. Nadharia ambazo ziliongoza utafiti huu ni nadharia ya uhalisia wa kijamaa ya Friedrich Hegel na nadharia ya udenguzi ya Jacques Derrida . Nadharia ya udenguzi imeasaidia katika kubainisha jinsi maoni ya waandishi wengi kuhusu chanzo cha dhuluma kwa mwananchi si ya hakika. Waandishi wengi wanahusisha kuteseka kwa mwananchi na umaskini, uongozi mbaya, mila zilizopitwa na wakati miongoni mwa sababu nyingine. Utafiti unalenga kuonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa, ni mwananchi aliye chanzo cha dhuluma anazokumbana nazo. Nadharia ya uhalisia wa kijamaa imemwezesha mtafiti kuhakiki na kuchambua hali na maisha halisi ambamo wananchi wa kawaida hujidhulumu. Utafiti huu ulifanywa maktabani na tamthilia teule zilichaguliwa kwa njia makusudi ikilenga tamthilia za Mstahiki Meya, Kilio cha Haki na Amezidi. Matokeo ya utafiti yamewasilishwa kwa maelezo kwa kufuata utaratibu huu: sura ya kwanza ya utafiti imetanguliza mada, maswali yanayoongoza utafiti, malengo ya utafiti, upeo na mipaka, yaliyoandikwa kuhusu mada, sababu za kuchagua mada na misingi ya nadharia. Sura ya pili ilihusu chanzo cha dhuluma kwa mwananchi wa kawaida. Sura ya tatu ilishughulikia athari zinazotokana na dhuluma kwa mwananchi kwa kuangazia tamthilia teule. Sura ya nne ilishughulikia mikakati ya mwananchi katika kuzuia dhuluma nayo sura ya tano ilishughulikia matokeo ya utafiti pamoja na mapendekezo ya mtafiti. Inatarajiwa kuwa utafiti huu umekuwa wa manufaa katika kuonyesha nafasi aliyonayo mwananchi katika kujikomboa au kujidhulumu. Aidha, utafiti huu utakuwa wa muhimu kwa wananchi kufahamu nafasi zao katika kubainisha uongozi bora.
Description
Tasnifu hii imetolewa ili kutosheleza baadhi ya mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Machi, 2018
Keywords
Citation