Usawiri wa Mandhari katika Embe Tamu (Njogu, 2003), Siku ya Wajinga (Momanyi, 2005) na Njiapanda (Amana, 2008) an Examination of Settings in Embe Tamu (Njogu, 2003), Siku ya Wajinga (Momanyi, 2005) and Njiapanda (Amana, 2008)

Loading...
Thumbnail Image
Date
2022
Authors
Mbithi, Mutisya Cosmas
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza usawiri wa mandhari katika fasihi andishi ya watoto. Mandhari yaweza kuwa mahali, wakati au muda ambao matendo ya kifasihi hufanyika. Malengo yalikuwa; kubainisha aina za mandhari yanayosawiriwa kuwasilisha maudhui katika miktadha ya fasihi andishi ya watoto katika riwaya hizi; Embe Tamu (Njogu, 2003), Siku ya Wajinga (Momanyi, 2005) na Njiapanda (Amana, 2008). Vilevile, ulichunguza jinsi mandhari yalichangia sifa za wahusika na mwisho kufafanua matumizi ya lugha katika kusawiri mandhari. Nadharia changamano zilitumika katika utafiti huu. Kwanza, nadharia ya finominolojia iliyoasisiwa na Husserl (1900 - 1901) na kuendelezwa baadaye na Heidegger, Sartre, Merleau (2012), Dordrecht na Boston (1997) na Smith na Thomasson (2005) miongoni mwa wengine. Nadharia hii huchunguza miundo ya uzoefu au ufahamu wa mandhari na jinsi watu wanavyoona vitu au kuvihisi katika mandhari na maana vitu vilivyo nayo kulingana na uzoefu wa mtu na ufahamu wake kuvihusu. Nadharia hii ilitumika kuchunguza aina ya mandhari kwa kuzingatia dhana tofauti katika mandhari na kuyahusisha na miktadha husika ya fasihi andishi ya watoto. Aidha, nadharia ya kimtindo iliyoasisiwa na Leech (1969) ilitumika. Nadharia ya kimtindo hushikilia kuwa lugha hufanikisha kazi ya sanaa katika uzuaji na ubunifu wa kifasihi kwani lugha husaidia kutoa ujumbe wa msanii au mtunzi kwa wasomaji au wasikilizaji. Nadharia hii ilitumika kutathmini matumizi ya lugha katika kusawiri mandhari katika fasihi andishi ya watoto. Ngara (1982), anaonyesha kwamba sehemu mbalimbali kama vile maudhui, mandhari na hata wahusika haviwezi kuwasilishwa bila kutumia lugha. Naye Wamitila (2003), anasema kuwa mtindo humwezesha mwandishi kuwasilisha ujumbe wake na kuonyesha sifa mahususi za mwandishi zilizojitokeza. Mihimili ya nadharia ya finominolojia na kimtindo ilitumika ili kuongoza utafiti na kutimiza malengo ya utafiti. Ukusanyaji data ulikuwa wa maktabani; kusoma vitabu na tasnifu mbalimbali zenye data iliyomnufaisha mtafiti katika kazi yake. Utafiti ulitumia vitabu ambavyo viliteuliwa kimaksudi vilivyolenga watoto ambao ni wa darasa la tano hadi nane kwa kuwa waliyafahamu mandhari halisi na yaliyowapendeza. Data iliyopatikana ilichanganuliwa na matokeo kuwasilishwa kupitia maandishi ya kinathari na maelezo kutolewa. Waandishi wa fasihi watanufaika na mchango wa kazi hii kwani utawaongoza kusawiri mandhari ambayo yatawavutia watoto na kuwasaidia kukua pamoja na kuwapasha ujumbe. Isitoshe, utafiti huu utawafaidi wakuza mitaala kwani wataweza kuteua vitabu ambavyo vitawafaa watoto na mwisho, utafaidi jamii kwa jumla kwani unaweka wazi mandhari ambayo yatawafaa watoto na hivyo kuendeleza jamii toka kizazi kimoja hadi kingine.
Description
Tasnifu hii Imewasilishwa ili Kutimiza Baadhi ya Mahitaji ya Kutuzwa Shahada ya Uzamili katika Idara ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Kenyatta, 2021
Keywords
Usawiri wa Mandhari, Embe Tamu (Njogu, 2003), Siku ya Wajinga (Momanyi, 2005), Njiapanda (Amana, 2008), Examination of Settings
Citation