Tathmini ya Maigizo ya Wahusika Walemavu Katika Kipindi cha Sultana Kwenye Runinga ya Citizen Nchini Kenya
Loading...
Date
2025-09
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Kipindi cha Sultana kilipeperushwa kwenye runinga ya Citizen nchini Kenya kuanzia
Machi, 2022 hadi Julai, 2023. Kipindi hicho kilihusisha wahusika mbalimbali wakiwemo
walemavu. Tafiti za awali zimechunguza usawiri wa wahusika walemavu katika njia hasi.
Utafiti huu ulilenga kuziba pengo hilo kwa kuchunguza usawiri wa wahusika walemavu
kwenye vipindi vya televisheni kwa njia chanya. Hivyo basi, utafiti huu ulilenga
kuchunguza maigizo ya wahusika walemavu kwenye kipindi hicho. Suala la utafiti
lilikuwa kutathmini maigizo ya wahusika walemavu katika kipindi cha Sultana katika
runinga ya Citizen nchini Kenya. Malengo ya utafiti huu yalikuwa; kujadili maudhui
yanayowasilishwa na wahusika walemavu katika kipindi cha Sultana kwenye runinga ya
Citizen, pili, kubainisha sifa za wahusika walemavu katika kipindi cha Sultana kwenye
runinga ya Citizen na kufafanua mbinu za maigizo zinazotumika na wahusika walemavu
katika kipindi cha Sultana kwenye runinga ya Citizen. Utafiti huu uliongozwa na nadharia
ya Maigizo (Turner, 1969) inayosisitiza umuhimu wa kudhihirisha mitagusano ya
wanajamii kwenye maisha yao halisi kupitia matendo yao kwenye jukwaa. Aidha,
nadharia hii inaonyesha manufaa ya hadhira katika kuchunguza vitendo vya waigizaji
kwenye jukwaa. Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Maktabani mtafiti
alidurusu vitabu, majarida, tasnifu na miswada mbalimbali kuhusu uigizaji, mbinu za
utafiti na nadharia ya Maigizo. Utafiti wa nyanjani ulihusu ukusanyaji wa data kwa
kuhusisha mahojiano na kurekodi. Vifaa vya utafiti vilivyotumiwa ni simu ya rununu,
tarakilishi na mwongozo wa mahojiano. Jumuiya ya utafiti ilikua waigizaji walemavu wa
viungo na wa tabia wa kipindi cha Sultana cha runinga ya Citizen. Sampuli ya utafiti
iliteuliwa kimaksudi ili mtafiti aweze kupata data ya malengo ya utafiti. Data ilikusanywa
kwa kutazama, kusikiliza na kunukuu majibu ya maswali kutoka kipindi kiteule. Data
ilichanganuliwa kwa njia ya maelezo kwa kuzingatia nadharia ya Maigizo, maswali na
malengo ya utafiti. Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kimaelezo. Utafiti ulibaini kuwa
wahusika walemavu wa viungo na wa tabia wanawasilisha maudhui mbalimbali.
Wahusika walemavu wanawasilisha maudhui ya bidii, mapenzi, ujasiri na unyanyapaa
ilhali wale wa tabia wanawasilisha maudhui ya ukatili, mauaji, tamaa na utabaka. Utafiti
pia umeonyesha kuwa wahusika walemavu wana sifa mbalimbali wanazotumia
kuwasilisha maudhui. Wahusika walemavu wa viungo wanadhihirisha kuwa na
ukakamavu, hasira, ubinafsi, upweke, uvumilivu na hekima ilhali wale wa tabia
wanadhihirisha kuwa na taasubi ya kiume, ukatili, udanganyifu, tamaa, ukaidi na
uchochezi. Aidha, mbinu mbalimbali zilitumiwa na wahusika walemavu. Mbinu hizi ni
pamoja na kufananisha, ishara za mwili, mazungumzo na hisia na mielekeo ya wahusika.
Utafiti huu utasaidia kuongeza data muhimu katika taaluma ya fasihi. Pia, utawafaa
watafiti watakaotumia nadharia ya Maigizo kwa kurejelea mihimili yake ambayo mtafiti
amejadili kwa kina.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa Katika Shule ya Sheria, Sanaa na Sayansi za Kijamii Ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha
Kenyatta. Septemba, 2025
Msimamizi
Richard Makhanu Wafula