Kanuni za Lugha Zinavyoathiri Somo la Kiswahili Katika Shule za Upili: Mfano za Kaunti ya Busia
Loading...
Date
2025-04
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulishughulikia mielekeo ya wanafunzi na walimu wa shule za upili katika Kaunti ya Busia kuhusu kanuni za lugha shuleni na namna kanuni hizi zinavyoathiri somo la Kiswahili. Utafiti huu ulichunguza na kuhakiki kanuni za lugha katika shule za upili. Aidha ulibaini mielekeo ya wanafunzi na walimu kuhusu kanuni za lugha shuleni na athari yake kwa somo la Kiswahili. Malengo matatu yalioongoza utafiti huu ni: Kueleza kanuni za lugha shuleni, kuchunguza mielekeo ya wanafunzi na walimu kuhusu kanuni za lugha shuleni na kufafanua athari za kanuni za lugha shuleni kwa somo la Kiswahili katika shule zilizo Kaunti ya Busia.Utafiti huu ulitumia nadharia mbili katika uchanganuzi wa data. Kwanza, nadharia ya Saikolojia ya jamii ya Vitendo Vilivyofikiriwa ya Ajzen na Fishbein (1980). Nadharia hii inasema kuwa, binadamu huwa na mtazamo kubalifu kuhusu jambo ambalo litamnufaisha na kuwa na mwelekeo hasi kwa jambo ambalo halina manufaa kwake. Nadharia hii ilitumika kubainisha mielekeo ya walimu na wanafunzi kuhusu kanuni za lugha za shule. Nadharia hii haingeweza kuhakiki kanuni za lugha za shule na athari yake kwa somo la Kiswahili kwa kukosa vigezo vya kuchanganua data hii. Kwa hivyo, nadharia ya pili ambayo ni ya Kijumuia na Kibinadamu ilioasisiwa na Richards na Rodgers (1995) ilitumika. Nadharia hii inasema kuwa, mazingira yenye usalama na utu kwa mwanafunzi humwathiri anapojifunza lugha ya pili. Ili kufanikisha malengo ya utafiti, wanafunzi na walimu kutoka shule za upili saba zenye viwango vya Kitaifa, Zaidi ya Kaunti na Kaunti ziliteuliwa. Walimu na wanafunzi walijaza hojaji likati na wanafunzi kushiriki katika mjadala elekezi wa makundi. Utafiti huu ulihusisha wanafunzi 560 na walimu saba wa somo la Kiswahili ambao pia ni wakuu wa idara ya Kiswahili. Mtafiti pia alifanya mahojiano na walimu wakuu kwa kila shule kuhusu kanuni za lugha zilizoteuliwa. Utafiti uliteua shule tatu za wasichana za bweni, tatu za wavulana za bweni na shule moja ya mseto ya kutwa. Utafiti huu ulifanywa nyanjani na maktabani. Vifaa tofauti vilitumiwa nyanjani, hojaji likati ilitumika ili kubainisha mielekeo ya walimu na wanafunzi kuhusu kanuni za lugha za shule. Mjadala elekezi wa makundi ulitumika kubainisha sababu ya mielekeo chanya au hasi na manufaa ya kanuni za lugha za shule kwa wanafunzi. Mbinu ya uchunzaji ilitumika kwa kutazama mabango yaliyo shuleni na kuchunguza namna mijadala kwa lugha ya Kiswahili ilivyoendeshwa. Utafiti wa maktabani ulifanywa kwa kusoma kazi za waandishi mbalimbali zinazohusu sera ya lugha kwa jumla, kanuni za lugha shuleni pamoja na mielekeo yao. Uchanganuzi wa data ulifanywa kwa kuainisha mada tofauti tofauti. Njia ya maelezo ilitumika kuwasilisha data kwa kiasi kikubwa. Picha, majedwali na michoro pia ilitumika. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa, shule tofauti zina kanuni za lugha tofauti na utekelezaji wake pia ni tofauti. Kanuni hizi ni kama lugha ya mawasiliano katika mazingira ya shule, siku za Kiswahili, mabango na maandishi katika mazingira ya shule, matumizi ya lugha ya Kiswahili katika mijadala, shughuli za idara ya Kiswahili kama makongamano, usomaji wa vitabu na magazeti pamoja na vyama vya Kiswahili. Ilibainika kuwa, wanafunzi na walimu wana mielekeo chanya kwa kanuni za lugha za shule ambazo zinaimarisha matokeo ya mtihani katika somo la Kiswahili. Utafiti pia ulibaini kuwa, utekelezaji wa kanuni za lugha za shule unahitaji mchango na ushirikiano wa wizara ya elimu, uongozi wa shule, walimu na wanafunzi wote ili athari yake iwe chanya kwa somo la Kiswahili.
Description
Tasnifu Hii Imetolewa ili Kutimiza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Aprili, 2025
Supervisor:
1.Pamela Muhadia Y. Ngugi