Harakati Za Ushairi wa Kiswahili Katika Ujenzi wa Jamii Yenye Mabadiliko: Mfano wa Diwani Ya Karne Mpya

Loading...
Thumbnail Image
Date
2025-05
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza harakati za ushairi wa Kiswahili katika ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Mashairi yaliyorejelewa ni yaliyo katika Diwani ya Karne Mpya (2007). Malengo ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha miktadha iliyoibua harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko, kueleza harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko katika diwani teule, pamoja na kuonyesha umuhimu wa harakati hizo katika jamii. Utafiti huu uliongozwa na baadhi ya mihimili ya nadharia ya Uhistoria Mpya. Nadharia ya Uhistoria Mpya ina misingi yake katika mawazo ya Raymond Williams (1977) na Michel Foulcault (1972, 1977, 1997). Nadharia hii huangalia uhusiano uliopo kati ya historia na fasihi. Hivyo, kazi ya fasihi haiwezi kutengwa na historia inayohusika nayo. Utafiti huu ulichukua muundo wa kimaelezo. Utafiti ulifanywa maktabani na mitandaoni. Sampuli ya utafiti huu iliteuliwa kimakusudi na data ikakusanywa kwa kusoma kwa kina mashairi teule na kunukuu sehemu ambazo zina data iliyokidhi mahitaji ya utafiti husika. Mtafiti pia alisoma vitabu, majarida, tasnifu na machapisho mbalimbali yaliyohusiana na mada. Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia malengo ya utafiti kwa kuongozwa na mihimili ya nadharia iliyoongoza utafiti huu. Matokeo ya utafiti huu yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo ya kinathari na utoaji mifano. Utafiti huu ulibaini kuwa harakati mbalilmbali za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko, zimeibuliwa na miktadha mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Isitoshe, harakati hizi zina mnachango muhimu katika jamii ya sasa. Inatarajiwa utafiti huu utachangia katika uhakiki wa fasihi kinadharia. Aidha, utaifaa jamii hasa katika kuelewa harakati za kujenga jamii yenye mabadiliko na manufaa yake. Tasnifu hii imegawika katika sura tano. Sura ya kwanza imeshughulikia utagulizi, usuli wa mada, suala la utafiti, malengo ya utafiti, maswali ya utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka, yaliyoandikwa kuhusu mada nadharia iliyoongoza utafiti huu pamoja na mbinu za utafiti. Sura ya pili imeshughulikia miktadha iliyoibua harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya tatu imeshughulikia harakati za ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya nne imeshughulikia umuhimu wa ujenzi wa jamii yenye mabadiliko. Sura ya tano imeshughulikia hitimisho, matokeo ya utafiti, changamoto za utafiti pamoja na mapendekezo ya utafiti.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Mei, 2025 Supervisor 1.Edwin Masinde
Keywords
Citation