Uchawi na Mazingaombwe katika Riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi
Loading...
Date
2022
Authors
Maggati, Charles Nyanduru
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza na kulinganisha matumizi ya uchawi na mazingaombwe kati ya vipindi viwili tofauti: kipindi cha riwaya za Kiswahili kabla ya uandishi wa usasabaadaye na kipindi cha usasabaadaye kwa kutumia riwaya za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi kwa kuzihusisha na mazingira asilia ya watunzi hao. Lengo la kuhusisha mazingira asilia yaliyowalea na kuwakuza watunzi hao lilikuwa ni kutaka kubaini mchango wa mazingira asilia ya mtunzi katika matumizi ya mbinu ya uchawi na mazigaombwe katika riwaya teule. Riwaya za Adili na Nduguze (1952), Kusadikika (1951) na Kufikirika (1946) za Shaaban Robert ziliteuliwa kimaksudi kuwakilisha kipindi cha uandishi wa riwaya za Kiswahili kabla ya usasabaadaye (uandishi unaotumia nduni za fasihi simulizi katika fasihi andishi). Riwaya za Nagona (1990) na Mzingile (1991) za Euphrase Kezilahabi ziliteuliwa kuwakilisha kipindi cha uandishi cha usasabaadaye (kipindi cha utandawazi). Madhumuni ya utafiti huu yalikuwa ni kubainisha uchawi na mazingaombwe katika mazingira asilia ya watunzi wa riwaya teule. Kuchunguza athari ya mazingira asilia ya watunzi katika matumizi ya mbinu ya uchawi na mazingaombwe katika riwaya teule, na kulinganisha matumizi ya mbinu ya uchawi na mazingaombwe kati ya watunzi Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi. Uchambuzi wa data katika utafiti huu uliongozwa na nadharia mbili: Nadharia ya uhalisiamazingaombwe iliyoasisiwa na Franz Roh mwaka 1925 na nadharia ya kiwewe cha kuathiriwa iliyoasisiwa mwaka 1973 na Harold Bloom. Uhalisiamazingaombwe ulitumika kubainisha matumizi ya uchawi na mazingaombwe katika riwaya teule na kuchunguza uhalisia wake katika mazingira asilia ya watunzi wa riwaya husika. Hii ni kwa sababu matumizi hayo hayawezi kufumbuliwa kwa kutegemea mbinu za kisayansi na nadharia za kihalisia. Nadharia ya kiwewe cha kuathiriwa ilitumika kulinganisha na kulinganua matumizi ya uchawi na mazingaombwe kati ya waandishi hao wawili katika riwaya teule. Utafiti umefanyika katika maktaba na nyanjani. Katika maktaba, riwaya teule zilisomwa na data za uchawi na mazingaombwe zilibainishwa na kulinganishwa. Nyanjani utafiti ulifanyika kwa njia za mahojiano, madodoso na ushuhudiaji. Utafiti ulihusisha matumizi ya uchawi na mazingaombwe kutoka mazingira asilia ya watunzi husika na kutoka riwaya teule. Hii ni kwa sababu hakuna utafiti wa kina uliokwishalinganisha matumizi ya uchawi na mazingaombwe kati ya kipindi kabla na kipindi cha usasabaadaye katika fasihi ya Kiswahili uliohusisha matumizi ya uchawi na mazingaombwe kutoka mazingira asilia ya watunzi na kazi zao za fasihi. Data zilizokusanywa na kuchambuliwa kwa kuongozwa na mkabala wa kitaamuli ni pamoja na: matumizi ya wahusika wa kichawi na wa kimazingaombwe, matukio ya ajabuajabu, uvunjivu wa kaida za uhalisia, na visasili na istiara. Matokeo yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo na ufafanuzi kwa maandishi. Ilitarajiwa kuwa kazi hii itawasaidia wasomaji, waandishi na wahakiki wa kazi za fasihi, kubaini mchango wa mazingira asilia ya mtunzi katika kuelezea na kukuza kazi za fasihi. Kutambua kuwa uchawi na mazingaombwe ni mtindo mwafaka wa kifasihi unaoweza kutumiwa kuelezea matukio halisi yanayomkabili binadamu katika mazingira yake kwa namna isiyo ya kawaida kwa kufumbata ujumbe katika matukio ya ajabu yanayojenga taharuki ili kumteka msomaji, huku ukifaulisha kueleza masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kidini na ya kitamaduni kwa namna inayokwepa kudhibitiwa na tabaka tawala.
Description
Tasnifu Imewasilishwa ili Kutosheleza Mahitaji ya Shahada ya Uzamifu katika Idara ya Kiswahili Chuo Kikuu cha Kenyatta, Mei, 2022
Keywords
Uchawi, Mazingaombwe, Riwaya, Shaaban Robert, Euphrase Kezilahabi