Ulinganishaji wa Ujifunzaji Stadi za Kiswahili kwa Wanafunzi wenye Ulemavu wa Macho katika Shule Jumuishi katika Kaunti za Nakuru na Kisumu, Kenya.

Loading...
Thumbnail Image
Date
2022
Authors
Muguche, Abunga Lilian
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Mawasiliano bora hutegemea uelewa wa stadi za lugha katika lugha husika. Ujifunzaji wa stadi za lugha ni kipengele muhimu katika lugha yoyote na huhusisha kusikiliza, kusoma, kuandika na kuzungumza kwa kiwango kikubwa ili kupata maana iliyokusudiwa katika muktadha husika. Utafiti huu ulilenga kubainisha tofauti za changamoto zinazowakumba wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika shule jumuishi za Menengai na Joel Omino katika ujifunzaji wa lugha ya Kiswahili. Vilevile, kulinganisha tofauti za usuli wa mazingira ya ujifunzaji kati ya shule jumuishi ya Menengai na Joel Omino na kuchambua athari za tofauti za kimazingira kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika ujifunzaji wa stadi za lugha ya Kiswahili. Kazi hii iliongozwa na Nadharia ya Usomi Tendaji ya Bruner (1966). Kulingana na nadharia hii, mchakato wa ujifunzaji huwa bora zaidi wanafunzi wakishirikishwa kwani wao hujenga maana pamoja na hivyo, kuimarishana kiujuzi. Utafiti huu ulifanywa maktabani na nyanjani. Shule jumuishi za msingi zilizotafitiwa ni Menengai na Joel Omino. Sampuli iliteuliwa kwa kutumia mbinu ya kimaksudi. Data ilikusanywa kwa kuhoji wanafunzi wote wenye ulemavu wa macho na baadhi ya walimu wa Kiswahili ilhali hojaji zilijazwa na wanafunzi wote wenye ulemavu wa macho na baadhi ya wanafunzi wasio na ulemavu wa macho. Mbinu ya uchunzaji ilitumika pia kuchunguza uhusiano wa mwalimu anapofunza na kuongoza kila shughuli darasani huku mwanafunzi akifuata maagizo na kujifunza. Data iliyokusanywa ilirekodiwa na kuchanganuliwa kwa kuzingatia maswali, malengo na nadharia ya utafiti. Matokeo ya utafiti yalibaini kuwa, kuna changamoto nyingi zinazowakumba wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika shule mbili lengwa. Hata hivyo, kuna changamoto zinazotofautiana katika shule hizi. Matokeo yalithibitisha kuwa, kuna tofauti tano za kimazingira kati ya shule zilizolengwa. Aidha, athari hasi na chanya zilitambulika kutokana na tofauti za kimazingira kwa wanafunzi wenye ulemavu wa macho katika ujifunzaji wa stadi za lugha ya Kiswahili. Matokeo ya utafiti huu yatawapa walimu wa lugha wanaofunza katika shule jumuishi na wakati mwingine shule maalum uelewa wa mbinu bora za kufunzia wanafunzi wenye ulemavu wa macho stadi za lugha ya Kiswahili. Aidha, matokeo ya utafiti huu pia yatasaidia washikadau katika elimu kama vile; Wizara ya Elimu, Taasisi ya kukuza mitalaa na watafiti wa masuala ya lugha na ulemavu wa macho.
Description
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Juni, 2022
Keywords
Ulinganishaji, Ujifunzaji Stadi, Kiswahili, Wanafunzi, Ulemavu wa Macho, Shule Jumuishi, Kaunti za Nakuru, Kisumu, Kenya
Citation