Uchanganuzi Linganishi wa Matini ya Hotuba za Kisiasa Kuhusu Ufisadi Kuanzia Mwaka 2015 Hadi 2020
Loading...
Date
2025-06
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Hotuba ni chombo muhimu kinachotumiwa na wanasiasa kuwasilisha sera zao, itikadi na hata kukemea maovu yanayotendeka katika jamii. Nchini Kenya, suala la ufisadi ni mojawapo ya maovu yanayotekelezwa na baadhi ya viongozi na wananchi. Kwa sababu hii, wanasiasa wengi huliangazia suala hili katika hotuba zao kwa umma kama mojawapo ya mikakati ya kuupiga vita ufisadi. Wao hutumia lugha kwa njia ya kipekee wanapoangazia suala hili hususan vita dhidi yake. Hii basi ndiyo sababu utafiti huu ulilenga kuchanganua na kulinganisha matini ya hotuba za kisiasa zinazoangazia suala la ufisadi nchini Kenya. Utafiti uliongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Usemi Hakiki (UUH) iliyoasisiwa na Fairclough katika kuchanganua hotuba sita za viongozi wawili wa kisiasa wa nchi ya Kenya kuhusu ufisadi ili kuchanganua na kulinganisha namna matini ya hotuba za kisiasa yanavyoshughulikia suala la ufisadi, kubainisha athari za hotuba hizi kwa wananchi na kisha kubaini mielekeo ya wananchi kuhusu hotuba hizi. Usampulishaji wa kimakusudi ulitumiwa kuwachagua wasailiwa na pia viongozi wa kisiasa ambao matini za hotuba zao zilichanganuliwa na kulinganishwa. Wanasiasa teule ni wale ambao wameliangazia suala hili la ufisadi kwa kina, hivyo basi hotuba zao ni faafu katika utafiti huu. Ili kupata matini za hotuba za kisiasa ambazo zilitumiwa kama data katika utafiti huu, mtafiti alikusanya video kutoka mtandao wa “YouTube”. Data nyingine pia ilikusanywa nyanjani kupitia hojaji funge ya likati na hojaji wazi ili kubaini athari na mielekeo ya wananchi wa Kenya kuhusu hotuba za kisiasa zinazoangazia suala la ufisadi. Mtafiti alizisikiliza na kuzinukuu hotuba teule kisha kuchanganua na kulinganisha matini zake. Aidha, data ilichanganuliwa na kulinganishwa kwa kutumia majedwali, takwimu na maelezo na kisha matokeo yake kuwasilishwa vilevile kwa kutumia maelezo, majedwali na takwimu. Matokeo ya utafiti huu yatawapa wananchi ama matumaini kuwa hotuba za kisiasa zinatekeleza dhima kuu katika vita dhidi ya ufisadi au ni gumzo tupu. Utafiti huu pia utachangia katika taaluma ya uchanganuzi matini ya hotuba za kisiasa zinazolenga maudhui teule kwa kutumia nadharia ya Uchanganuzi Usemi Hakiki.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa katika Idara ya Kiswahili ili Kutimiza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Juni, 2025
Supervisor:
1.Bonface Ngugi