Changamoto za Kimofosintaksia Miongoni Mwa Wanafunzi wa Kiswahili wa Shule za Upili Wilayani Muhanga, Nchini Rwanda

Loading...
Thumbnail Image
Date
2014-07-31
Authors
Ntawiyanga, Sylvain
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Pendekezo hili la utafiti linatarajia kuchunguza "Changamoto za kimofosintaksia miongoni mwa wanafunzi wa Kiswahili wa shule za upili wilayani Muhanga, nchini Rwanda". Katika utafiti huu, makosa ya kimofosintaksia yanayofanywa na wanafunzi hawa yatachunguzwa kwani kipengele hiki huchukuliwa kama kiini cha lugha yoyote ile. Vipengele vingine vya sarufi huingiliana nacho na kukitegemea kwa kiwango kikubwa. Kwa hivyo, utafiti huu unalenga kubainisha makosa ya kimofosintaksia yanayofanywa na wanafunzi wa Kiswahili wa shule za upili wilayani Muhanga, kuainisha makosa hayo; kuyaeleza na kutathmini mikakati inayozingatiwa kupunguza makosa hayo. Utafiti huu utaongozwa na nadharia za Uchanganuzi Makosa (UM) na ile ya Lugha Kadirifu (LK). UM unatilia mkazo mbinu za kuichunguza lugha ya mwanafunzi kwa kubainisha makosa anayoyafanya, aina za makosa hayo, kuyaeleza na kuyatathmini. Nayo LK inachunguza lugha ya mwanafunzi kwa kuzingatia mikakati ya isaikoljia katika mchakato unaoendelea wa ujifunzaji wa L2. Katika LK, vyanzo vya makosa yanayofanywa na mwanafunzi huchunguzwa kutegemea mikakati hiyo ya kisaikolojia ambayo mwanafunzi anatumia katika jitihada zake za kujifunza L2. Kwa hivyo, kupitia uzingatifu wa nadharia hizi, matokeo ya utafiti huu yatasaidia kutoa mapendekezo mwafaka kwa washikadau wa ufundishaji wa Kiswahili wa shule za upili nchini Rwanda ili kupunguza makosa ya kisarufi yanayofanywa na wanafunzi hawa. Utafiti huu utakuwa wa kimaelezo na data zitakusanywa nyanjani kwa kuzihusisha shule tatu wilayani Muhanga ambazo ni Groupe Scolaire de Kirwa, Groupe Scolaire de Nyarusange na shule ya Groupe Scolaire de Shyogwe. Mbinu ya kimakusudi itazingatiwa katika usampulishaji na watafitiwa watapatikana kwa kutumia mbinu nasibu ambapo wanafunzi kumi watachaguliwa katika madarasa ya tano na sita kutoka kila shule iliyoteuliwa. Hojaji na mahojiano ndiyo yatakayozingatiwa na mtafiti kukusanya data kutoka kwa wanafunzi hao na walimu wao. Uwasilishaji wa data utafanywa kwa njia ya kimaelezo ambapo majedwali na vielelezo vitatumika ili kufafanua zaidi matokeo ya utafiti huu.
Description
Keywords
Citation