Uhamishaji wa maana katika sajili ya mchezo wa Kandanda

Loading...
Thumbnail Image
Date
2015
Authors
Anjejo, Mark Odawo
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulinuia kubainisha jinsi maana inavyohamishwa katika sajili ya mchezo wa kandanda nchini Kenya. Lugha ya mchezo wa kandanda huonyesha namna ya utegemezi wa maneno na kauli za sajili tofauti na istilahi za taaluma nyingine kufuma na kuibua maana. Utafiti huu ulilenga kutimiza malengo matatu yafuatayo: Kutambua mbinu za mawasiliano zinazotumiwa na watangazaji wa mchezo wa kandanda, kubainisha msimbo wa maana inayoibuliwa kutokana na matumizi ya lugha katika sajili ya mchezo wa kandanda na kubainisha taaluma na sajili zinazotumiwa na sajili ya mchezo wa kandanda ili kujitosheleza. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Sarufi Amilifu Mfumo iliyoasisiwa na Halliday (1985). Nadharia hii inaeleza kuwa kama tukio la kijamii, lugha iliundwa kwa minajili ya kuwezesha mawasiliano kulingana na miktadha mbalimbali. Inaangalia lugha sawa na mtandao wa maana unaowakilishwa kwa maumbo ya kisarufi. Data ya utafiti huu ilikusanywa maktabani na nyanjani. Maandishi yanayohusu mchezo huu kutoka vitabu, makala, tasnifu, magazeti na majarida yalidurusiwa ili kujenga usuli wa utafiti huu na kung'amua yaliyoandikwa kuhusu mada. Matangazo ya moja kwa moja ya mchezo huu na taarifa za mchezo huu katika redio na runinga yalisikilizwa ili kupata data iliyochanganuliwa. Data iliyokusanywa ni msamiati, istilahi, virai, vishazi na sentensi. Data iliainishwa na kuchanganuliwa kwa uzingativu wa maswali na malengo ya utafiti na mihimili ya nadharia ya Sarufi Amilifu Mfumo. Matokeo ya utafiti yaliwasilishwa kwa njia ya maelezo yaliyojumuisha matumizi ya majedwali. Ripoti ya utafiti huu imepangwa katika sura tano. Sura ya kwanza ni utangulizi uliojumuisha usuli wa mada, suala la utafiti, maswali na malengo ya utafiti, sababu za kuchagua mada, upeo na mipaka, mapitio ya maandishi, misingi ya kinadharia na mbinu za utafiti. Sura ya pili imeangalia mbinu za mawasiliano zinazotumiwa na watangazaji wa mchezo wa kandanda. Mbinu zilizobainika ni utohozi, uchanganyaji msimbo, ubadilishaji msimbo, takriri, tashbihi, tashihisi, semi, methali, maswali ya balagha na tafsiri sisisi. Sura ya tatu imebainisha msimbo wa maana inayoibuliwa kutokana na matumizi ya lugha katika sajili ya mchezo wa kandanda. uchanganuzi wa data umebainisha kuwa lugha huwa na maana dhanishi, maana tagusani na maana matinishi. Sura ya nne iliangazia taaluma na sajili zinazotumiwa na sajili ya mchezo wa kandanda ili kujitosheleza. Imejitokeza kuwa sajili ya mchezo wa kandanda hutegemea istilahi na vipashio vya sajili ya hoteli, ulinzi, hospitali, biashara na mapenzi. Sura ya tano ni muhtasari wa matokeo ya utafiti, mahitimisho na mapendekezo. mependekezwa kuwa Maandihi na malurnbano baina ya mashabiki wa sajili hii yachunguzwe kwa kuwa utafiti huu ulijikita katika lugha ya uneni inayotumiwa na watangazaji wa mchezo huu. Mbali na kutafiti namna lugha inavyotumiwa katika aina tofauti ya michezo, pana hitaji la kuchunguza lakabu zinazohusu wachezaji, wakufunzi na viwanja mbalimbali ili kubainisha maana zinazotokana nazo. Hivyo basi, matokeo ya utafiti huu yanatazamiwa kuwa ya manufaaa kwa wanafunzi, walimu, watafiti na wataalam wengine wa isimu watakaozamia matagaa ya semantiki na pragmatiki, hasa kuhusu maana inavyoibuliwa katika miktadha mbalimbali. Waaidha, yatatoa mchango mkubwa kwa waitifaki wa isimujamii wanaodhamiria kukuza sajili changa.
Description
Tasnifu hii imetolewa ill kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya shahada ya uzamili katlka chuo kikuu cha Kenyatta
Keywords
Citation