Muundo wa Njeo Katika Lugha ya Kingoni
Loading...
Date
2013-12-17
Authors
Haule, Festo Christantus
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Utafiti huu umehusika kuchunguza muundo wa njeo na halinjeo katika lugha ya
Kingoni. Mofimu ya njeo na halinjeo katika vitenzi vya lugha ya Kingoni
inaundwa kupitia viambishi (mofimu) na toni. Kwa hivyo, masuala matatu ya
msingi yameshughulikiwa ili kuweza kubaini muundo wa mofimu hizo. Kwanza,
utafiti huu umechunguza viambishi katika vitenzi ili kuvibaini na kuona jinsi
vinavyohusika katika kuunda njeo na halinjeo. Pili, umechunguza toni ili kuweza
kubaini mwenendo wake katika kuunda njeo na halinjeo katika vitenzi vya lugha
hii. Hatimaye, uhusiano wa viambishi na toni katika kuunda njeo na halinjeo za
Kingoni umechunguzwa na kubainishwa. Misingi ya Nadharia ya Fonolojia
Vipambasauti ambayo inahusika katika uchanganuzi wa toni hususan katika
vitenzi na Nadharia ya Fonolojia ya Konsonanti Vokali ambayo inahusika katika
uchunguzi wa silabi zimetumiwa. Nadharia hizo zimetumiwa ili kufanikisha
malengo ya utafiti huu. Data ya utafiti huu hasa ilipatikana nyanjani ambako
vitenzi vya njeo (pia virai tenzi na sentensi kwa ajili ya kubaini halinjeo) viliweza
kukusanywa. Data hiyo ilipatikana katika vijiji vitano vya wilaya ya Songea
Vijijini ambako lugha ya Kingoni inatumiwa zaidi. Vijiji hivyo ni Mpitimbi,
Namatuhi, Matimila, Magagula na Peramiho (mji mdogo). Utafiti huu
umegawanywa katika sura tano; Sura ya kwanza inahusu utangulizi wa kazi
nzima. Katika kufanya hivyo kiini cha utafiti huu kimeelezwa. Aidha
kumejadiliwa yaliyoandikwa kuhusu njeo na halinjeo katika lugha za Kibantu na
lugha ya Kingoni. Vilevile, mbinu za utafiti zimebainishwa. Sura ya pili
imechunguza vipengele vya fonolojia na mofolojia hususani katika vitenzi vya
Kingoni kwa kuzingatia vipengele ambavyo vinahusiana na muundo wa njeo na
halinjeo. Sura ya tatu imechanganua mofimu ya njeo katika vitenzi vya Kingoni.
Uchanganuzi huo umehusisha viambishi awali, fuatishi, tamati na toni katika
kubainisha mofimu hiyo. Sura ya nne imechanganua namna mofimu ya halinjeo
inavyoundwa ambapo viambishi na toni pamoja na mazingira ya matukio katika
kuundwa kwa halinjeo yameweza kubainishwa. Sura ya tano imehitimisha utafiti
huu kwa kutoa muhtasari, matokeo, mapendekezo na changamato za utafiti huu.
Matokeo ya utafiti huu yamedhihirisha kuwa kuna viambishi awali, fuatishi na
tamati vya njeo katika vitenzi vya Kingoni. Aidha viambishi hasa viambishi awali
vya wakati ndivyo vinavyohusika kubainisha halinjeo kwa kushirikiana na
viambishi vya matukio. Matokeo hayo pia yamedhihirisha kuwa torn inahusika
kubainisha njeo na halinjeo kwa kushirikiana na viambishi vya mofimu hizo.
Utafiti huu licha ya kuwezesha kufahamu njeo na halinjeo katika lugha ya
Kingoni, pia unaongeza ujuzi wa kiisimu kuhusu njeo na halinjeo katika lugha za
Kibantu ikizingatiwa kuwa lugha hii ni miongoni mwa familia ya lugha hizo.
Description
PL 8701 .H31