Dhima ya utawala wa nabongo mumia katika maenezi ya lugha ya kiswahili ubukusuni, Mkoani Magharibi (Kenya)
Loading...
Date
2009
Authors
Nakhisa, Andrew W.
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umeeleza na kuchanganua dhima ya utawala wa Nabongo Mumia katika
maenezi ya lugha ya Kiswahili Ubukusuni, Magharibi mwa Kenya. Utafiti huu ulijikita
katika kipindi cha utawala wa Nabongo Mumia tangu kutawazwa kwake kama Chifu
Mkuu, mnamo mwaka wa 1910 hadi kifo chake katika mwaka wa 1949.
Katika utafiti huu, tutalenga kuainisha, kueleza kuchunguza na kuchanganua mikakati
iliyotumiwa na Nabongo Mumia kuchangia maenezi ya lugha ya Kiswahili. Katika
kulifafanua swala la utawala, misingi iliyowekwa ili kufanikisha maenezi ya lugha ya
Kiswahili iliangaliwa. Maendeleo na mabadiliko yaliyojikita katika asasi muhimu kama
dini ,biashara, ndoa na maingiliano ya kijamii kwa kuitumia mizani ya mifanyiko ya
kijamii yalichangia maenezi ya lugha ya Kiswahili Ubukusuni. Lugha ya Kiswahili
ilipata hadhi kubwa katika kipindi hiki kwa sababu iliendesha shughuli nyingi za
Nabongo Mumia ambaye alikuwa mshiriki wa karibu wa mkoloni. Utafiti huu basi
umebainisha nafasi muhimu ya utawala wa Nabongo Mumia katika kuwekea lugha ya
Kiswahili msingi thabiti wa kuenea Ubukusuni.
Tasnifu hii imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza ambayo ni utangulizi
imeshughulikia swala la utafiti, sababu zakuichagua mada, upeo wa utafiti, madhumuni
ya utafiti, msingi wa nadharia, yaliyoandikwa kuhusu mada na mbinu za mtafiti. Sura ya
pili imechunguza historia ya jamii mbili - Ababukusu na Abawanga - hasa jinsi
walivyoingiliana na kuathiriana. Sura ya tatu inaangalia dhima ya utawala wa Nabongo
Mumia katika maenezi ya Kiswahili. Sura ya nne imeangazia asasi nyinginezo kama dini,
mahakama, ndoa miongoni mwa nyingine. Mwisho, sura ya tano ni hitimisho. Mtafiti
arnetoa muhtasari, matokeo kuhusu utafiti, mapendekezo ya utafiti zaidi na matatizo
yaliyokumba utafiti huu.
Kutokana na utafiti huu imedhihirika kwamba utawala ulichukua nafasi muhimu zaidi
katika maenezi ya lugha ya Kiswahili Ubukusuni. Pili, utafiti huu umeonyesha kwamba
Babukusu walikuwa wategemezi kwa kuwa katika kuitumia lugha ya Kiswahili, walianza
kuunga mkono utamaduni wa kigeni. Mwisho, asasi kama ndoa, dini, biashara,
mahakama za Kiafrika, elimu, muziki, michezo na miundo misingi ilifanikiwa Ubukusuni
kwa sababu ya kutumia lugha ya Kiswahili. Kwa kiasi kikubwa asasi hizi zilifanikishwa
na utawala wa Nabongo Mumia.
Description
Imetolewa kwa madhumuni ya kutosheleza baadhi ya mahitaji ya shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu Cha Kenyatta