Nafasi ya Wahusika Wendawazimu Katika Riwaya Teule: Kidagaa Kimemwozea na Mkamandume
Loading...
Date
2022
Authors
Karimi, Kibui Sarabina
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu unalenga kuchunguza nafasi ya wahusika wendawazimu. Wahusika hawa ni Matuko Weye na Bilal katika riwaya za Kidagaa Kimemwozea (Walibora:2012) na Mkamandume (Mohamed:2013).Malengo ya utafiti huu lilikamilishwa ambayo ni matatu ni pamoja na: kuchunguza mchango wa wahusika wendawazimu katika kufanikisha maudhui ya riwaya teule, kubainisha mchango wa wahusika hawa katika kuendeleza mbinu za uandishi na kuthibitisha jinsi wahusika wendawazimu wanafaulisha dhamira ya waandishi. Nadharia ya Uchanganuzi Nafsia ilitumika katika kuchambua data ya utafiti.Kwa mujibu wa Freud (1913), Uchanganuzi Nafsia hufananisha kazi ya fasihi na ndoto. Riwaya, tamthilia na Ushairi ni kazi zinazofananishwa na ndoto kwani ni kazi bunifu. Usanii ni ndoto zinazoashiria matumaini na matamanio ya mwandishi. Aidha, wahusika katika fasihi ni viumbe au binadamu wanaoishi katika ndoto za mwandishi. Wao hushirikiana na mwandishi katika matarajio na matatizo yake. Ukusanyaji wa data ulifanyika maktabani. Riwaya teule za Kidagaa Kimemwozea na Mkamandume zilisomwa pamoja na majarida, tasnifu, vitabu na matini husika kutoka mtandaoni. Tulipitia nyaraka na kusoma kwa umakinifu ili kudondoa data iliyotakikana. Utafiti huu si linganishi . Tulitumia sampuli ya kimaksudi ili kupata data ambayo tulishughulikia kuuendeleza utafiti. Data ilichanganuliwa kwa kuzingatia maswali ya utafiti, malengo ya utafiti na mihimili ya nadharia ya uchanganuzi-nafsia. Uwasilishaji wa matokeo ulifanyika kwa kuzingatia mbinu ya maelezo. Matokeo ya utafiti yamebaini kuwa waandishi wa riwaya za Kidagaa Kimemwozea na Mkamandume waliwashirikisha wahusika wendawazimu ambao ni Matuko Weye na Bilal. Wahusika hawa wamechangia kukuza maudhui ambayo ni pamoja na vita dhidi ya udhalimu, uongozi mbaya, elimu na ukombozi. Utafiti huu pia umefaulu kubainisha mchango wa wahusika hawa katika kuendeleza mbinu za uandishi.Wahusika wendawazimu wamechangia kukuza mbinu za uandishi kama vile taswira, kejeli, mbinu rejeshi, kinaya, balagha, dayalojia na ucheshi. Utafiti pia umebainisha dhamira ya waandishi ya kueleza masaibu yanayowakumba wanyonge katika jamii, kuangazia na kutahadharisha kuhusu athari za uongozi mbaya unaosababisha kugawanywa kwa raia katika misingi ya kitabaka. Changamoto tulizozipitia zimeangaziwa na hatimaye tumetoa mapendekezo kwa watakaofanya tafiti za baadaye kuhusiana na riwaya hizi.Utafiti huu utasaidia jamii kwa jumla. Utawafaa wanajamii, wanafunzi, wahadhiri na wahakiki wa fasihi.
Description
Tasnifu Hii Imewasilishwa Katika Idara ya Kiswahili, Shule ya Fani na Sayansi ya Jamii ya Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa Ajili ya Kutimiza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili
Keywords
Nafasi, Wahusika, Wendawazimu, Riwaya Teule, Kidagaa, Kimemwozea, Mkamandume, Riwaya