Usawiri wa Mhusika Mkinzani katika Tamthilia Teule za Ebrahim Hussein: Kinjeketile (1969), Jogoo Kijijini (1976) na Arusi (1980)
No Thumbnail Available
Date
2024-11
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umechunguza usawiri wa mhusika mkinzani katika tamthilia teule za
Ebrahim Hussein; Kinjeketile (1969), Jogoo Kijijini (1976) na Arusi (1980). Mhusika
mkinzani ni mhusika ambaye huenda kinyume cha maadili ya jamii yake au kukinzana
na mhusika nguli katika kazi ya fasihi. Katika kufanya hili, mkinzani hukuza
kutoelewana au mgogoro katika utungo wa kifasihi. Malengo yaliyonuiwa kutekelezwa
ni; kubainisha mbinu mbalimbali za usawiri wa mhusika mkinzani katika tamthilia
teule, kuchunguza namna mhusika mkinzani anavyokuza mgogoro katika tamthilia
teule na kutathmini maudhui yanayoibuliwa na mhusika mkinzani katika tamthilia teule.
Nadharia mbili ndizo zilizoongoza utafiti huu; Naratolojia na nadharia ya Drama.
Naratolojia iliasisiwa na Plato (1930) na kukuzwa na Rimmon-Kennan (1983), Stanzel
(1984), Phelan (1987) na Keen (2003). Inahusika na vipengele vya usimulizi vikiwemo
wakati, nafsi, nafasi, wahusika na maudhui. Vipengele vya wahusika na namna
wanavyokuza maudhui ndivyo vilivyotufaa katika utekelezaji wa lengo la kwanza na la
tatu. Naratolojia inafafanua kuhusu njia za kuwasawiri wahusika na vilevile kueleza
kuhusu wahusika kama vyombo vya kuwasilishia ujumbe (maudhui). Hata hivyo, swala
la ukuzaji wa mgogoro na mhusika mkinzani halielezeki vyema na nadharia ya
Naratolojia. Hivyo, nadharia ya Drama iliyoasisiwa na Carl Jung (1964) ndiyo
iliyotuongoza katika kutekeleza lengo la pili. Nadharia hii ya Drama inahusu matendo
ya wahusika katika drama na namna yanavyopelekea kuzuka kwa migogoro. Sampuli
iliteuliwa kwa mbinu ya kimaksudi ambapo tamthilia mbili; Kinjeketile na Jogoo
Kijijini ziliteuliwa kimaksudi ili kuchunguza usawiri wa mhusika mkinzani kama
mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa. Kwa upande mwingine, tamthilia ya Arusi
iliteuliwa ili kuchunguza usawiri wa mhusika mkinzani kama mhusika aliyepo kwenye
jukwaa. Data ilikusanywa maktabani ambapo tasnifu, majarida na makala mbalimbali
yanayohusiana na mada hii yalisomwa kwa kina. Aidha data ya kimsingi ilitoka katika
tamthilia teule ambazo zilisomwa na kuchanganuliwa kwa umakini na uzingativu
mwingi. Hoja zinazohusiana na mkinzani zilitengwa katika mada ndogondogo,
zikachanganuliwa kisha kufafanuliwa kwa maelezo yaliyoambatanishwa na dondoo
mwafaka kutoka katika tamthilia teule. Jumla ya ripoti ya utafiti huu imesukwa katika
sura tano. Matokeo ya kazi hii yanatarajiwa kuwafahamisha wasomi kuhusu mbinu
mbalimbali za kumsawiri mhusika mkinzani katika tamthilia pamoja na nafasi yake
katika ukuzaji wa mgogoro na maudhui. Utafiti uligundua kwamba, mhusika mkinzani
katika tamthilia anaweza kuwasilishwa kama mhusika aliyepo kwenye jukwaa au kama
mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa. Mhusika mkinzani anapowasilishwa kama
mhusika asiyekuwepo kwenye jukwaa, huzua ukinzani kutokana na wanachokisema
wahusika wengine au msimulizi kuhusu matendo yake. Haya yalibainishwa katika
tamthilia za Kinjeketile na Jogoo Kijijini. Aidha, iligundulika kuwa mhusika mkinzani
anapowasilishwa kama mhusika aliyepo kwenye jukwaa, huzua ukinzani kutokana na
mazungumzo na matendo yake ya moja kwa moja kama ilivyobainika katika Arusi.
Mbinu ambazo mhusika mkinzani amesawiriwa nazo katika tamthilia teule ni pamoja
na ya kuwatumia wahusika wengine, ya kinatiki, ya kimaelezo na ya ulinganuzi na
usambamba. Pia, mkinzani amebainika kuwa nguzo muhimu katika ploti ya tamthilia
kwani huchochea migogoro mikuu katika drama. Mbali na hayo, utafiti umeonyesha
kwamba, katika tamthilia teule, mhusika mkinzani ametumiwa na mtunzi kama chombo
cha kuwasilishia maudhui makuu, kama vile udhalimu, ukatili, usaliti, siasa na utawala
kwa ujumla.
Description
Tasnifu Hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitajiya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Nov, 2024
supervisor
Richard. M. Wafula