Uhusiano wa Mbinu za Kufundisha Sarufi na Umilisi wa Mazungumzo ya Wanafunzi wa Sekondari Wilayani Thika Magharibi, Kenya.
Abstract
Lugha ya Kiswahili ina dhima kubwa ulimwenguni katika kukidhi mahitaji ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kielimu. Nchini Kenya, Kiswahili ni lugha ya taifa na rasmi. Isitoshe, Kiswahili ni somo la lazima linalofundishwa na kutahiniwa katika viwango vya shule za msingi na sekondari. Msingi wa lugha hii ni sarufi ambayo hutawala stadi zote za lugha. Licha ya dhima ya sarufi katika kufanikisha mawasiliano tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wanafunzi wengi hawawezi kujieleza kwa usahihi na kwa ufasaha hata baada ya kuhitimu masomo ya sekondari. Hali hii ilimchochea mtafiti wa kazi hii kuchunguza uhusiano uliopo kati ya mbinu za kufundisha sarufi na umilisi wa mazungumzo ya wanafunzi.Utafiti huu ulidhamiria kutimiza malengo yafuatayo: Kuchunguza mbinu zinazotumiwa na walimu kufunza sarufi ya Kiswahili, kuchunguza vifaa vinavyotumika katika ufundishaji wa sarufi, kutambua mazoezi yanayotumiwa ili kuimarisha umilisi wa mazungumzo, na hatimaye kuchunguza uhusiano uliopo kati ya mbinu za kufundisha sarufi na umilisi wa mazungumzo ya wanafunzi. Utafiti huu ulifanyika katika Kaunti ndogo ya Thika Magharibi katika Kaunti ya Kiambu. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya mfumo katika utaratibu wa ufunzaji na ujifunzaji wa lugha ya pili. Muundo wa kimaelezo ulitumika. Mtafiti alitumia uteuzi sampuli kinasibu kuteua shule katika viwango vya kitaifa, kaunti na kaunti ndogo. Uteuzi makusudi ulitumika kuteua kidato cha tatu na walimu wao. Sampuli lengwa ya wanafunzi iliteuliwa kinasibu. Data ilikusanywa kutumia hojaji, mahojiano na utaratibu wa utazamaji darasani ili kuimarisha uaminifu na uthabiti wa data. Data iliyokusanywa ilichanganuliwa kwa muundo wa kimaelezo, kithamani na kiidadi. Data hii iliwasilishwa kwa kutumia majedwali na grafu. Matokeo yalionyesha kuwa walimu wengi walitumia mbinu ya mhadhara katika kufundisha sarufi huku mbinu za kisasa zinazowashirikisha wanafunzi zaidi zikipuuzwa.Utafiti pia ulidhihirisha kuwa wanafunzi hawashirikishwi ipasavyo katika mazoezi yanayoweza kuimarisha umilisi wa sarufi na mazungumzo. Isitoshe, matumizi ya chaki na ubao ulitawala utaratibu wa kufundisha sarufi huku vifaa vingi vikikosa kutumika. Hatimaye utafiti huu ulibainisha kuwa kuna uhusiano kati ya mbinu za kufundisha sarufi na umilisi wa mazungumzo ya wanafunzi. Utafiti huu ulipendekeza kuwepo na mafunzo kwa walimu kuhusu mbinu, mazoezi na vifaa mwafaka katika ufundishaji wa sarufi ili kuimarisha umilisi wa lugha ya Kiswahili.