Mitindo katika nyimbo za tohara za jamii ya wakamba wa masaku tarafa ya kati
Abstract
Utafiti huu ulifanywa ili kushughulikia mabadiliko ya kimtindo katika nyimbo za tohara za jamii ya Wakamba wa Masaku tarafa ya kati. Tasnifu hii imegawanywa katika sura tano. Sura ya kwanza imetanguliza mada ya utafiti. Miongoni mwa mambo yaliyoshughulikiwa ni swala la utafiti, malengo ya utafiti, upeo na mipaka, misingi ya nadharia na mbinu za utafiti. Sura ya pili imezungumzia historia ya Wakamba na kuonyesha ya kwamba tohara zao zimetokana na mazingira yao. Katika sura ya tatu, utafiti umeinisha -na kuchanganua nyimbo za tohara za kimapokeo katika jainii ya Wakamba. Sura ya nne nayo imezingatia nyimbo zinazoimbwa wakati wa sasa vijana wanapotahiriwa. Hatimaye sura ya tano ni muhtasari, matokeo na changmoto ya nadharia za Ethnografia ya mawasiliano ya Hymes (1974) na ile ya kimtindo ya Leech (1969) ambazo zilitumiwa katika utafiti huu zimeonyesha kuwa muktadha na matumizi ya tamathali za usemi huchangia pakubwa katika kueleza, kuelewa na kufahamu umuhimu wa nyiso katika jamii. Wakati wa kushughulikia utafiti huu iligunduliwa kuwa kuna mabadiliko makubwa katika mitindo ya nyimbo za tohara ya Wakamba hasa wa eneo lililofanyiwa utafiti. Mabadiliko haya yanatokana na mapisi ya kiwakati, mfumo wa kisasa wa elimu, dini za Kimagharibi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, na utamanduni wa kigeni. Utafiti huu uligundua kuwa mambo haya yameuathiri sana utamaduni wa jamii hii. Fikra na mawazo ya wanajamii kuhusu nyiso pamoja na tohara za kijamii zinaendelea kudidimia. Sababu ni kwamba watahiriwa hawapelekwi "kitutoni", yaani mahali pa kutahiriwa pamoja kama zamani. Hawaimbi nyimbo za tohara wao wenyewe bali wanapelekwa hospitalim kutahiriwa na madaktari wa kisasa wala sio ngariba tena. Nyiso zilizopo zina mawazo kuhusu Mungu na mitindo ya kisasa ya kuchanganya ndimi. Nyimbo hizi huimbwa na familia ya mtahiriwa kama vile babu na nyanya yake. Kwingine wazazi wa mtahiriwa na ndugu zake ndio humwimbia usiku wa kuamkia kutahiriwa au usiku wa baada ya tohara. Inasemekana kuwa hakuna unyago tena katika jamii hii. Ni watoto wa kiume to ndio wanaofanyiwa tohara. Mwisho, kupitia uchanganuzi wa nyiso za zamani na kisasa, utafiti huu uligundua kuwa utamaduni wa jamii za Kiafi-ika hasa jamii iliyofanyiwa utafiti unaendelea kudidimia na kuundika au kuumbika upya katika nyanja zote za kimaisha. Hii ndio sababu ya haya mabadiliko.