Ukengeushi wa wasomi katika riwaya ya Euphrase Kezilahabi
Abstract
Utafiti wetu unahusu swala la ukengeushi wa wahusika wasomi katika riwaya nne za Euphrase Kezilahabi. Riwaya zenyewe ni Rosa Mistika, Kichwa Maji, Dunia Uwanja wa Fujo na Gamba la Nyoka. Tunachambua usawiri wa wahusika kwa lengo la kuainisha hali zinazosababisha huo ukengeushi. Juu ya kumulika ukengeushi ni daraja zake mbalimbali, tumeonyesha vile mwandishi amechora wahusika waliokengeuka na mapendekezo anayoyatoa kuhusu suluhisho la hali hiyo. Sura ya kwanza ni utangulizi wa utafiti. Katika sura hii tunajadili misingi ya nadharia ya utafiti wetu kwa ujumla. Licha ya hayo, tunaangalia mada ya utafiti. Ingawa wataalam kama vile Marx na Engels, Goldthorpe, Bottomore, Ollman, Boyd na Wanjala wameliangalia swala la ukengeushi, hawajaainisha daraja zake. Kuongezea, tunaitazama nadharia tunayoitumia katika utafiti wetu ambayo ni uhalisia wa kijamaa. Nadharia hii ndiyo imetuwezesha kuliangalia swala zilizofanywa ambazo kwa hali moja au nyingine zinahusiana na kazi yetu. Tunazijadili kazi hizi kwa ufupi. Mwisho tunaelexa njia tuanazozitumia katika utafiti wetu. Sababu kuu ya kuwepo kwa sehemu hii ni kututayarisha kinadharia kuzishughulikia sehemu zinazofuata. Katika sura ya pili, tunachunguza kwa ufupi maisha ya mwandishi wa kazi za utafiti wetu ili pengine tuelewe ni kwa nini anaandika vile anavyofanya. Tunaelewa kuwa maisha ya mwandishi humwathiri katika kazi yake. Fauka ya hayo, tunatazama dhana ya ukengeushi na athari zake kwa msomi. Sura hii ndiyo msingi wa utafiti wetu. Upeo wa utafiti wetu unabainika katika sura za tatu na nne. Katika sura hizi, tunadhihirisha daraja mbalimbali za ukengeushi zinazoonyeshwa na wasomi katika uhusiano wao na wanajamii wengine. Daraja hizo ni, ukengeushi wa kukosa mamlaka, kukosa adabu, kutengwa pamoja na kujitenga na jamii na kujitenga na nafsi. Katika srua ya tatu tunamchunguza msomi kwa upande wa uhusiano wake na jamii pamoja na mamlaka au uwezo anaopatiwa na hiyo jamii. Sura ya nne inaendeleza mawazo ambayo yamejadiliwa katika sura inayotangulia. Tunamchambua msomi akiwa kama kiongozi, kwa upande wa uadilifu na mfano wa nidhamu anaotoa pamoja na maana ya maisha kwa msomi. Kwa ujumla , mwandishi Euphrase Kezilahabi amemsawiri msomi kama asiyeleta matumaini yoyote katika jamii. Amemwonyesha kama mwanajamii aliyejitenga na kutengwa na wanajamii wengine, aliyekisa adabu na aliyetengana na hata nafsi yake. Mfano anaoutoa msomi unaangamiza badala ya kuongoza.