Uhakiki wa maudhui ya utetezi katika utunzi wa Remmy Onyala
Abstract
Tasnifu hii inahakiki maudhui ya utetezi katika utunzi wa Remmy Ongala. Tunachunguza vile Remmy Kama msanii amefinyanga na kusawiri maudhui hayo katika baadhi ya nyimbo zake tulizochagua. Uchunguzi wetu unajaribu kudhiririsha mambo mawili ya kimsingi; kwanza, kwamba wimbo ni utanzu wa fasihi unaohakiki maisha ya jamii husika. Pili, fasihi huathiriwa sana na nguvu na nyenzo za uzalishaji mali katika jamii.
Sura ya kwanza ni utangulizi wa utafiti ambapo tunazingatia somo, maudhumuni na upeo wa utafiti huu. Vile vile tunataja machache kuhusu nadharia inayotuongoza katika uchunguzi wetu pamoja na yale yaliyoandikwa na wengi kuhusu somo hili letu. Hatimaye tunatoa sababu za kulichagua somo letu pamoja na njia zetu za utafiti.
Sura ya pili inajadili mapisi ya wimbo katika mifumo mbali mbali ya kisiasa. Inadhihirisha kwamba wimbo kama ilivyho na tanzu nyengine za fasihi unaathiriwa sana na nyenzo na nguvu za uzalishaji mali zinazodhihir katika jamii husika. Aidha imeonyeshwa kwamba watunzi kwa pupa yao ya kujulimbikia mali wameedelea kutunga nyimbo kwa ajili ya kutunga tu. Hata hivyo si wote waliochukua mkondo huu, na tumeonyesha nafasi ya aina ya utunzi inayowakilishwa na Remmy katika Jamii.
Sura ya tatu tumeigawa katika sehemu tatu hata ingawa sehemu zote hizi zinazingatia jambo lile lile la utetezi. Sehemu ya kwanza inajadili jinsi Remmy anavyotetea wanyonge wa kitabaka ambao kwa kukosa nguvu za kiuchumi wanajikuta wakidhulumiwa na tabaka la juu ambalo ndilo linalohimili nguvu za kiuchumi. Sehemu ya pili inajadili jinsi Remmy anavyomtetea mwanamke ambaye kwa sababu ya kuwa mwanamke anadhulumiwa na mwanaume. Sehemu ya tatu inajadili jinsi Remmy anavyowatetea walemavu ambao kwa kasoro za kimaumbile wanajikuta wakibaguliwa na kudhulumiwa na jamii iliyogawika katika matabaka. Katika sura hii vile vile tumeonyesha vile Remmy anavyotumia lugha kisanaa ili kuyasawiri maudhui yake ya utetezi.
Sura ya nne ndilo hitimisho la uchunguzi wetu. Katika sura hii tumetoa muhtasari wa kazi yetu kwa jumla na kuonyesha kuwa mazingira yanayozunguka utunzi wa wimbo wowote ni muhimu sana kama nguzo ya kuuelewa wimbo huo. Tumetoa mapendekezo yetu kuhusu uchunguzi zaidi wa wimbo wa kisasa. Hatimaye tumeorodhesha nyimbo tulisozipitia katika uchunguzi wetu.