Ufungamano wa Itikadi na Propaganda Katika Tamthilia za Kithaka wa Mberia: Kifo Kisimani (2001) na Maua Kwenye Jua La Asubuhi (2004)
Loading...
Date
2023
Authors
Minyade, Sheril Mugaduka
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
kenyatta university
Abstract
Utafiti huu umeonyesha ufungamano wa itikadi na propaganda katika tamthilia za
Kithaka Wa Mberia: Kifo Kisimani (2001) na Maua kwenye Jua la Asubuhi (2004).
Baadhi ya sababu ambazo zimechochea kufanywa kwa utafiti huu ni kuwa; suala la
itikadi ni la muhimu sana kwa vile ndilo ambalo huongoza matendo ya binadamu. Pia,
propaganda ina uhusiano wa karibu sana na kazi za kifasihi ambazo huwa ni chombo cha
kiitikadi. Kwa hivyo, malengo ya utafiti yalikuwa kubainisha aina za itikadi katika
tamthilia teule, kuonyesha aina za propaganda katika tamthilia teule na kuonyesha
uhusiano kati ya itikadi na propaganda. Kwa mujibu wa Marx na Engels (1977), itikadi ni
fikra zote za maoni ya wanadamu kuhusu wanayoyasema na wanayoyafikiria kuhusu
dini, sheria, siasa, maadili na falsafa. Propaganda hushawishi fikra za mtu kutenda jambo
kwa namna fulani. Ni ushawishi unaoratibiwa kwa malengo fiche, (Ellul, 1965).
Tamthilia za Kifo Kisimani na Maua kwenye Jua la Asubuhi ziliteuliwa kimaksudi kwa
sababu zina data ambayo imetumika katika kutimiza malengo ya utafiti. Utafiti huu
umeongozwa na nadharia ya Uchanganuzi Tahakiki Usemi (UTU) iliyoasisiwa na
Fairclough (1989). Ni nadharia ambayo hueleza uhusiano uliopo kati ya matukio ya
kiusemi, kisiasa, kijamii na kiutamaduni na jinsi yanavyoathiriwa na itikadi.Nadharia
teule inaangazia jinsi usemi huo huathiri matukio katika jamii. Utafiti huu ni wa
kimaelezo kwa sababu uchanganuzi wa data umetekelezwa na kuwasilishwa katika
maelezo ya kina. Kutokana na maelezo ya kina, itikadi ya dini, ukombozi, utawala,
utamaduni, umwinyi na ubepari imebainishwa kutoka katika tamthilia teule. Data
ilikusanywa kutokana na muktadha wa mazungumzo ya wahusika, usemi na matumizi
yao ya lugha. Mtafiti ameonyesha aina za propaganda kama vile propaganda ya kisiasa na
kijamii, wazi, siri na propaganda ya kati. Pia, utafiti umethibitisha kuwa itikadi na
propaganda ni dhana mbili tofauti lakini zina uhusiano wa karibu. Diskozi zote
zinaongozwa na itikadi ambapo maudhui, usemi, matumizi ya lugha na muktadha wa
mazungumzo huashiria itikadi ya mhusika. Propaganda na itikadi ni masuala muhimu
katika kazi za kifasihi. Hata hivyo, imebainika kuwa ili propaganda iweze kufaulu,
inajiegemeza katika itikadi fulani. Pia, hakuna itikadi ambayo inaweza kufaulu bila
kuwashawishi watu. Ushawishi huu ndio propaganda, na hivyo kufanya dhana hizi kuwa
na uhusiano wa karibu sana. Tafiti zaidi zinaweza kufanywa katika kitengo cha itikadi ili
kuchunguza wahusika wanaharakati katika tamthilia hizi. Uanaharakati unaendana moja
kwa moja na itikadi ambayo huhalalisha seti za matendo zinazojitokeza katika vitendo.
Utafiti huu unawawezesha wasomi na wahakiki wa kazi za kifasihi kutumia dhana ya
itikadi na propaganda kama dhana mbili tofauti ambazo zina ufungamano.
Description
Tasnifu hii Imewasilishwa ili Kutosheleza Baadhi ya
Mahitaji ya Shahada ya Uzamili Katika Chuo Kikuu cha
Kenyatta
Keywords
Itikadi na Propaganda, Kithaka wa Mberia, Kifo Kisimani, Maua Kwenye Jua La Asubuhi