Makosa ya kileksia katika insha na chanzo chake uchunguzi wa shule tano za upili wilayani Kiambu
Abstract
Lengo la kazi hii ni kuchunguza na kuanisha makosa ya kileksia yanayofanywa na wanafunzi wa kidato cha pili katika insha zao. Aidha, chanzo cha makosa hayo na umuhimu wake katika kujifunza lugha ni jambo linalotiliwa maanani. Wanafunzi wanaoshiriki katika utafiti huu ni wa wilaya ya Kiambu (Kenya) na wanazungumza Kikikuyu LI yao. Kwa kurejerelea nadharia ya Lugha Kadirifu, mikondo ambayo makosa haya yanafuata imejadiliwa.
Kuna sehemu tano katika kazi hii. Sura ya kwanza inatanguliza kazi yote. Hapa, mada ya utafiti, madhumuni na malengo ya utafiti, sababu za kuchagua mada, misingi ya nadharia, upeo na mipaka, yale yaliyoandikwa kuhusiana na utafiti huu na mbinu za utafiti, zimeshughulikiwa.
Katika sura ya pili, umuhimu wa insha katika kujifunza lugha umeshughulikiwa. Uandashi wa insha umejitokeza kama kipengele cha utendaji wa lugha kwani mtu huwasilisha ujumbe kupitia maandishi. Aidha, sifa muhimu za insha bora zimejadiliwa katika sura hii. Imejitokeza kuwa insha bora yapaswa kutumia sarufi inayofaa, msamiati mpana ulioendelezwa vizuri na pia iwe na mtindo na maudhui mahsusi.
Ni katika sura ya tatu ambapo data inawasilishwa na hoja muhimu kujadiliwa. Hapa, makosa yaliyojitokeza kwenye insha za wanafunzi yamefafanuliwa na kuchanganuliwa kwa kufuata misingi ya Lugha Kdirifu. Makosa yamewekwa katika mikondo mbalimbali kama vile tahajia, uhamishaji, ujumlishaji wa sheria, athari ya LI. mbinu za ufundishaji, matumizi ya methali, misemo na tashbihi, tafsiri isiyofaa, visawe na manenno tangamano.
Kwenye sura ya nne, chanzo cha makosa yaliyojadiliwa katika sura ya tatu yameshughulikiwa. Kadhalika, maoni ya wanafunzi na walimu kuhusu makosa ya kileksia yamejadiliwa. Chanzo cha makosas haya kimejitokeza kama vile athari ya LI kutojua mipaka ya sheria, tafsiri na utohozi usiofaa, upungufu wa msamiati na mbinu dhaifu za ufundishaji.
Hatimaye, sura ya tano ni muhtasari wa kazi hii yote. Aidha, matokeo ya utafiti huu pamoja na mapendekezo yameshughulikwa. Imedhihirika kuwa insha za wanafunzi huwa na makosa mbalimbali ya kileksia na hatua zifaazo zinahitaji kuchukuliwa na walimu pamoja na wakuza mitaala ili kukabiliana na tatizo hili.