Ukiukaji wa Kanuni ya Kufuta Mabano katika Uundaji wa Nomino Ambatani za Kiswahili: Mtazamo wa Mofolojia Leksia
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuchunguza ukiukaji wa Kanuni ya Kufuta Mabano katika
uundaji wa nomino ambatani za Kiswahili. Nomino ambatani ni mofu changamano
(Mgullu; 1999). Kanuni ya Kufuta Mabano huonyesha hatua zinazotumiwa kuunda
neno sahihi kwa kutumia viambajengo. Mabano katika kanuni hii hudhihirisha mipaka
na hufutwa kuashiria kuwa sheria za uundaji wa maneno hazina ufikiaji wa umbo la
neno linalotokana na ngazi za awali. Uchunguzi huu ulifanywa baada ya kubaini kuwa
baadhi ya nomino ambatani za Kiswahili hukiuka Kanuni ya Kufuta Mabano hasa
pale ambapo mabadiliko hutokea katikati mwa neno baada ya vipashio mbalimbali
kuunganishwa. Data ya uchunguzi huu ilikusanywa kutoka kwenye Kamusi Kuu ya
Kiswahili (2015) ambapo nomino ambatani thelathini zinazoghairi thelathini
zisizoghairi Kanuni ya Kufuta Mabano mtawalia zilitumika. Nomino hizi
zilichaguliwa kwa kuzingatia uwepo wa sifa za ukiukaji wa Kanuni ya Kufuta Mabano
(KKM). Malengo ya uchunguzi huu yalikuwa ni: kudhihirisha nomino ambatani za
Kiswahili zinazoghairi KKM ya Mofolojia Leksia (ML). Kudhihirisha maumbo ya
nomino ambatani za Kiswahili yanayokiuka KKM ya Mofolojia Leksia, kubainisha
sababu za baadhi za nomino ambatani za Kiswahili kukiuka KKM ilhali zingine
hazikiuki, na kueleza mchango wa ukiukaji wa KKM ya Mofolojia Leksia kwa
wanaleksikografia wa Kiswahili. Ili kufanikisha utafiti huu, nadharia ya Mofolojia
Leksia iliyoanzishwa na Kiparsky (1982) na kufafanuliwa zaidi na Katamba &
Stonham (2019): Kanuni ya Kufuta Mabano na Kanuni ya Mzunguko Kamili
iliongoza uchunguzi huu. Data ya uchunguzi huu ilikusanywa maktabani. Baadhi ya
makala zilizotumika katika uchunguzi huu ni tasnifu, makala yaliyosakurwa
mtandaoni na majarida. Usampulishaji kimakusudi uliongoza uchunguzi huu ili
kufikia maneno husika ya nomino ambatani yaliyodhihirisha ukiukaji wa KKM.
Matokeo ya uchunguzi huu yamedhihirisha kuwa ukiukaj wa Kanuni ya Kufuta
Mabano husababishwa na mofu ya pili ya nomino ambatani kuonekana na mofu ya
kwanza, na muktadha wa matumizi ya nomino ambatani katika mawasiliano ya kila
siku. Utafiti huu ni nafasi bora ya kuchangia isimu hasa kupitia kufahamu na
kufafanua mwambatano katika Kiswahili, kuwahami waundakamusi za Kiswahili na
maarifa, kukuza mofolojia ya Kiswahili na kuchochea uchunguzi zaidi.