Makosa ya Kisarufi Yanayofanywa na Wanafunzi Wataita wa Shule za Msingi Wanaojifunza Kiswahili Sanifu katika Kaunti ya Taita / Taveta Nchini Kenya

Loading...
Thumbnail Image
Date
2021
Authors
Zighe, Martina
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulilenga kuchunguza makosa ya kisarufi miongoni mwa wanafunzi Wataita wanaojifunza Kiswahili Sanifu. Utafiti uliongozwa na nadharia za Uchanganuzi Linganuzi (UL) na Uchanganuzi Makosa (UM). UL ni nadharia ya uchanganuzi wa kiisimu unaohusisha ulinganishaji wa lugha mbili. Nadharia hii ilituwezesha kuchunguza athari za lugha ya Kitaita kwa wanafunzi Wataita wanapojifunza Kiswahili Sanifu. UM ulituwezesha kubainisha aina mbalimbali za makosa ya kisarufi ya wanafunzi na jinsi ya kuyakabili. Malengo ya utafiti huu yalikuwa: Kubainisha makosa ya kisarufi yanayofanywa na wanafunzi Wataita wa shule za msingi katika kujifunza Kiswahili Sanifu, kuainisha makosa ya kisarufi yanayofanywa na wanafunzi Wataita wa shule za msingi, kuchunguza uhusiano uliopo kati ya makosa yanayofanywa na wanafunzi Wataita na ubashiri wa UL na kubainisha mbinu mwafaka za kuyakabili makosa ya kisarufi yanayofanywa na wanafunzi Wataita katika utendaji wao wa Kiswahili Sanifu. Utafiti ulihusisha ukusanyaji data kupitia kwa maongezi na maandishi. Utafiti ulihusisha shule sita za msingi kutoka tarafa ya Wundanyi katika kaunti ya Taita/Taveta zilizoteuliwa kuzingatia usampulishaji. Wanafunzi walioshirikishwa ni wale wanaoongea Kitaita kama L1 waliokuwa darasa la saba. Wanafunzi watano waliteuliwa kutoka kila shule kutumia njia ya sampuli nasibu, kwa jumla wakiwa wanafunzi thelathini. Mbinu zilizotumika kukusanya data ni hojaji, mahojiano yaliyochochewa na usimulizi wa hadithi na ukaguzi wa insha zilizowahi kuandikwa na wanafunzi na kusahihishwa na walimu wao. Hojaji ilihusisha jaribio lililojumuisha sehemu mbili za maswali. Sehemu ya kwanza ilishirikisha maswali ya kutafsiri kauli kutoka kwa Kitaita hadi Kiswahili Sanifu na ya pili ilikuwa na maswali ya kujaza mapengo yaliyoachwa wazi katika sentensi. Maswali ya kutafsiri yalituwezesha kuchunguza ikiwa Kitaita kiliathiri wanafunzi katika utendaji wao wa Kiswahili Sanifu na yale ya kujaza mapengo yalitusaidia kubainisha vipengele vya kisarufi vilivyowatatiza wanafunzi. Katika kukusanya data ya maongezi iliyohusisha masimulizi ya hadithi, mtafiti alizinasa kwa kanda kisha baadaye akazinakili na kuzichunguza. Utafiti ulijikita kwa makosa yaliyohusu nomino, vivumishi na virejeshi. Data iliwasilishwa kwa njia ya kimaelezo ambapo majedwali yalitumika. Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwepo kwa makosa ya kisarufi yaliyotokana na athari za lugha ya Kitaita. Makosa hayo yalijumuisha uhamishaji wa dhana na mifumo ya kiisimu kutoka L1 hadi L2 na tafsiri potofu. Makosa mengine yalikuwa ujumuishaji mno, uhamishaji wa ufundishaji na kutomakinika kwa wanafunzi katika maandishi yao ya Kiswahili Sanifu. Mikakati ya kuyashughulikia makosa haya tuliyoibainisha ni: utangamano wa mwalimu na wanafunzi, wanafunzi kushirikiana katika kukosoana, mwalimu kutambua chanzo cha kosa la mwanafunzi na kumwelekeza, mwalimu kujitayarisha vilivyo kabla ya somo, matumizi ya vitabu vilivyoidhinishwa, ufundishaji wa Kiswahili kwa kuzingatia mwelekeo wa UL na kutahadharisha wanafunzi dhidi ya tafsiri sisisi. Ilipendekezwa utafiti zaidi ufanywe kuhusu makosa ya wanafunzi Wataita kuhusiana na vipengele kama fonolojia, semantiki na msamiati.
Description
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza Baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Kenyatta, Septemba, 2021
Keywords
Makosa ya Kisarufi, Yanayofanywa, Wanafunzi Wataita, Shule za Msingi, Wanaojifunza Kiswahili Sanifu, Kaunti ya Taita / Taveta, Nchini Kenya
Citation