Mshabaha na Tofauti Kati ya Hadithi Fupi ya Kisasa na Ngano

Loading...
Thumbnail Image
Date
2021
Authors
Mwanzu, Misigo Daniel
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu umeshughulikia mshabaha na tofauti kati ya hadithi fupi ya kisasa na ngano. Diwani zilizoshughulikiwa ni: Mwavyaji wa Roho na Hadithi Nyingine (Sanja, 2011), Kurudi Nyumbani na Hadithi Nyingine (Mbatiah, 2007) na Mimba Ingali Mimba na Hadithi Nyingine (Mc Onyango, 2006). Hali kadhalika, ngano zilizoshughulikiwa zimo katika vitabu vya Swahili Tales as Told by the Natives of Zanzibar (Steere, 1870) na Myths and Legends of the Swahili (Knappert, 1970). Utafiti ulilenga kuchanganua muundo, mtindo, maudhui na wahusika katika hadithi fupi ya kisasa na ngano. Nadharia iliyoongoza utafiti huu ni nadharia ya vikale iliyoasisiwa na Jung ama Frazer na kuimarishwa katika fasihi na Northrop Frye (1957) na baadaye ikaendelezwa na Campbell (2004), Guerin (2005) na Larsen (2018). Kulingana na Frye, kikale ni ishara ambayo huzua taswira inayojirudiarudia katika kazi ya sanaa kiasi kwamba inatambuliwa kama kiungo cha ujuzi wa mtunzi wa kazi fulani. Nadharia hii imeteuliwa kwa msingi kuwa ilituwezesha kuonyesha ikiwa taswira zinazojitokeza katika hadithi fupi zinasheheni picha kongwe zinazojirudiarudia mara kwa mara kama ilivyo katika ngano. Kwa msingi huu tumebaini kuwa kuna vigezo tofauti vya kupimia kazi za hadithi fupi na ngano. Aidha, utafiti huu umefanyika katika maktaba za vyuo vikuu nchini Kenya. Data ya kimsingi imepatikana kutokana na kusoma diwani ya hadithi fupi, ngano zilizomo katika vitabu vya Steere na Knappert, tasnifu, majarida na vitabu vinavyohusiana na mada ya utafiti. Data imechanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo na lugha ya nathari kuambatana na malengo ya utafiti. Utafiti huu umeonyesha kuwa kuna tofauti nyingi kati ya hadithi fupi ya kisasa na ngano kuliko mshabaha. Hii inathibitisha kuwa hakuna hadithi fupi iliyotokana na ngano.
Description
Tasnifu hii Imetolewa ili Kutosheleza baadhi ya Mahitaji ya Shahada ya Uzamili katika Shule ya Fani na Sayansi za Kijamii, Chuo Kikuu cha Kenyatta, Machi, 2021
Keywords
Mshabaha, Tofauti Kati, Hadithi Fupi, Kisasa, Ngano
Citation