Ufundishaji na ujifunzaji wa ushairi katika shule za upili
Résumé
Utafiti huu unahusu misingi ya ugumu wa ushairi wa Kiswahili katika shule za upili. Misingi hii imeelezwa na kujadiliwa kulingana na maelezo ya walimu, wanafunzi, wakuza mitaala kutoka Taasisi ya Elimu Kenya, pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Nadharia changamano iliyoongoza na kuelekeza utafiti huu ilikita misingi yake katika nadharia ya umaumbo na ya ushirikiano. Kwa kuzingatia misingi ya nadharia hizi, misingi ya ugumu wa mashairi imetathminiwa. Kadhalika, lugha ya kishairi imechanganuliwa, na kuonyeshwa namna inavyokiuka na kupotosha lugha ya kawaida. Imeelezewa namna lugha ya kishairi inavyokiuka lugha ya kawaida katika viwango tofauti. Kwa mfano, ina ukiushi wa kilahaja, kitahajia, awamu ya kihistoria, kisajili na kisemantiki. Pia mna maelezo kuhusu uchanganuzi wa lugha ya kishairi katika viwango vitatu; kiwango cha tamathali za usemi, cha mikakati ya kujielezea na cha kisauti.
Tasnifu hii imegawika katika sura tano. Sura ya kwanza ina utangulizi wa tasnifu. Katika sehemu hii, mna mada ya utafiti, sababu za utafiti na madhumuni ya utafiti. Upeo wa utafiti pia umeshughulikiwa katika sehemu hii. Pia, ina maelezo kuhusu yale yaliyoandikwa kuhusiana na mada hii, mbinu za utafiti pamoja na nadharia iliyoongoza utafiti huu.
Sura ya pili ina maelezo juu ya fasili za dhana ya ushairi na namna zinavyoweza kuathiri ujifunzaji na ufundishaji wa ushairi. Vile vile sura hii ina maelezo kuhusu malengo ya kielimu ya kufundisha ushairi katika shule za upili pamoja na umuhimu wake.
Sura ya tatu ina maelezo na mjadala kuhusu misingi ya ugumu wa mashairi kama ilivyoelezwa na wanafunzi. Lugha, umbo, uhaba wa vifaa, mielekeo hasi na uhaba wa wakati, ndiyo msingi iliyotajwa na wanafunzi.
Sura ya nne inahusu maelezo ya walimu na maafisa wa elimu kuhusu ufundishaji wa ushairi wa Kiswahili na matatizo yake. Matatizo yanayoukumba ufundishaji wa ushairi ni Lugha ya kishairi, uhaba wa vifaa na wakati, mielekeo hasi pamoja na mbinu zisizofaa.
Sura ya tano inahusu uchanganuzi wa viwango mbalimbali vya Lugha ya Kiswahili. Kura ya sita ina muhtasari wa tasnifu, mahitimisho, pamoja na mapendekezo kutokana na utafiti.