Lugha ya kimafumbo katika riwaya za katama mkangi
Abstract
Utafiti huu utashughulikia matumizi ya lugha ya kimafumbo katika riwaya za Mkangi Mafuta
(1984) na Walenisi (1995). Kutokana na udurusu wa maandishi ya wahakiki na watafiti
mbalimbali wa riwaya za Mafuta (1984) na Walenisi (1995) imebainika kwamba kuna pengo
linalohitaji utafiti zaidi. Matumizi ya lugha ya kimafumbo inayojumuisha istiari, tashbihi,
jazanda, majazi, methali na nahau haijashughulikiwa kama mada mahususi ya utafiti katika
riwaya hizi mbili. Malengo ya utafiti huu ni; kubainisha mifano ya matumizi ya lugha ya
kimafumbo katika riwaya teule, kukadiria mchango wa lugha ya kimafumbo katika kuibulia na
kuendeleza maudhui, mwisho ni kutathmini jinsi lugha ya kimafumbo inavyotumiwa katika
usawiri na uainishaji wa wahusika katika riwaya hizi.
Mada hii ya "lugha ya kimafumbo" katika riwaya za Mafuta (1984) na Walenisi (1995)
iliteuliwa kwa kuzingatia sababu kadhaa. Kwanza, lugha ya kimafumbo ni miongoni mwa
vipengele muhimu vya lugha katika kazi za fasihi. Pili, riwaya za Mkangi hufunzwa vyuoni na
shuleni. Katika kuwasaidia wasomaji wa riwaya hizi kuelewa zaidi, haina budi kutathmini na
kubainisha lugha ya kimafumbo iliyotumiwa na mwandishi katika riwaya teule. Mwisho ni
kwamba, utanzu wa riwaya unaendelea kukua, hivyo basi utafiti unafaa kufanywa ili kutathmini
mitindo ya lugha aliyotumia mwandishi. Utafiti huu utaongozwa na nadharia nadharia ya
kimafumbo ya kisasa ambayo waasisi wake ni Lakoffna Johnson (1992). Data itakayokusanywa
itachanganuliwa kwa kuzingatia lugha ya kimafumbo kwa usaidizi wa mihimili ya nadharia ya
kimafumbo ya kisasa. Utafiti huu utasaidia katika uhakiki wa fasihi kwa upande wa riwaya.