Browsing by Author "Masika, Mark Elphas"
Now showing 1 - 2 of 2
Results Per Page
Sort Options
Item Mchango wa Sitiari na Metonimu Katika Uzuaji wa Polisemia Katika Kiswahili(Kenyatta University, 2024-04) Masika, Mark Elphas; King'ei, Kitula Osore, MiriamUtafiti huu ulilenga kuangazia mchango wa sitiari na metonimu katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili ambapo uliweza kupambanua namna metonimu na sitiari zinavyoweza kuzua maana mpya ya maneno ya Kiswahili. Pia ulitusaidia kufahamu athari ya metonimu na sitiari katika uzuaji wa polisemia katika Kiswahili. Kimsingi polisemi ni leksimu moja yenye maana nyingi ambazo zinahusiana kwa njia moja au nyingine (Chacha na Pendo, 2019). Pia kuna njia zingine za uzuaji wa polisemi kwa mfano ukopaji, mabadiliko katika matumizi ya neno, na ufasiri mpya wa homonimu. Kuna baadhi ya wataalamu ambao wamezungumzia polisemia kama vile Mwendamseke (2016) aliyeandika makala kuhusu uelekeo wa maana za kipolisemia katika msamiati wa Kiswahili. Naye Gaichu (2013) alishughulikia uchunguzi wa sitiari dhanifu katika methali za Kiswahili. Utafiti huu wa sitiari na metonimu ndio usiodhihirika moja kwa moja. Utafiti huu uliongozwa na malengo yafuatayo: Kubainisha polisemi ambazo zimeundwa kutokana na sitiari na metonimu katika Kiswahili, kuainisha polisemi katika lugha ya Kiswahili, kudhihirisha mchakato ambao sitiari na metonimu hupitia kuunda polisemi katika Kiswahili. Nadharia ya semantiki tambuzi iliongoza utafiti huu. Nadharia hii ni sehemu ya nadharia ya Isimu Tambuzi ambayo ina misingi katika saikolojia tambuzi (Vyvyan & Greens, 2006). Data husika ilikusanywa maktabani. Maktabani, maneno ambayo ni polisemi na yameundwa kwa sitiari na metonimu kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2018) yalikusanywa. Mbinu ya usampulishaji wa kimaksudi ilitumika katika uteuzi wa sampuli. Data ilichanganuliwa na kuwasilishwa kwa njia ya kimaelezo na majedwali ili iweze kueleweka. Kutokana na data ya utafiti huu, imebainika kuwa kuna baadhi ya polisemi zilizojitokeza ndani ya homonimu. Kwa mfano, tata2 na chuo1. Pia, imebainika kuwa data hiyo ilikuwa na polisemi za majina ya wanyama, wadudu na ndege. Hata hivyo, imebainika kuwa sitiari huwa na maeneo mawili ya ufahamu: moja ni ile inayotokana na maumbo tunayoyaona na nyingine ni ile ya kidhahania. Hiyo ya kwanza inaitwa eneo chasili na ya pili eneo lengwa. Kwa mfano, sitiari “Maria ni chui” maumbo tunayoyaona (eneo chasili) ni Maria na chui na maumbo ya kidhahania (eneo lengwa) ni ukali. Kwa upande mwingine, imebainika kuwa metonimu huwa na eneo moja. Kwa mfano, leksimu kiti eneo lake ni uongozi. Tafiti zingine zinaweza kufanywa kuhusu mchango wa mbinu zingine za lugha kama vile tashibihi, lakabu na jazanda yaani; namna ambavyo mbinu hizo zinaweza kuchangia pia katika kuunda polisemia katika Kiswahili.Item Polisemi ambazo Zimeundwa Kutokana na Sitiari na Metonimu katika Kiswahili(EANSO, 2024-02) Masika, Mark Elphas; Mwita, Leonard ChachaMakala haya imechunguza polisemi ambazo zimeundwa kutokana na sitiari na metonimu katika Kiswahili. Kimsingi, polisemi ni leksimu moja yenye maana nyingi ambazo zinahusiana kwa njia moja au nyingine. Pia polisemi huundwa kwa njia zingine kwa mfano, ukopaji, mabadiliko katika matumizi ya neno, na ufasiri mpya wa homonimu. Nadharia ya semantiki tambuzi ilitumiwa katika uchambuzi wa data ya utafiti huu. Nadharia hii ni sehemu ya nadharia ya Isimu Tambuzi ambayo ina misingi yake katika saikolojia tambuzi . Data ya makala haya ilikusanywa maktabani. Maneno ambayo ni polisemi na yameundwa kwa sitiari na metonimu kwenye Kamusi ya Kiswahili Sanifu (2018) yalikusanywa. Mbinu ya usampulishaji wa kimaksudi ilitumika katika uteuzi wa sampuli. Kutokana na data ya utafiti huu, imebainika kuwa kuna baadhi ya polisemi zilizojitokeza ndani ya homonimu. Kwa mfano, tata1 na chuo1. Pia, utafiti huu umebaini kuwa polisemi nyingi huundwa kisitiari ikilinganishwa na metonimu. Makala haya inapendekeza kwamba tafiti zingine zaidi zinaweza kufanywa kuhusu namna mbinu zingine za lugha kama vile chuku, methali, nahau na tashibihi zinaweza kuchangia katika Isimu.