Ushairi wa Kiswahili: maendeleo na mabadiliko ya maudhui

Loading...
Thumbnail Image
Date
2012-01-03
Authors
Masinde, E. W.
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Abstract
Tasnifu hii imejishughulisha na uchanganuzi wa maendeleo na mabadiliko ya maudhui katika ushairi wa Kiswahili. Mazingira ya msanii pamoja na tajriba zake katika maisha huathiri kwa kiasi kikubwa namna anavyouona na kuusawiri ulimwengu. Mtazamo wake humwelekeza kuhusu mapendekezo anayoyatoa kwa jamii. Hivyo, kadiri mazingira yake ya kibinafsi na ya kijamii yanavyoendelea kubadilika ndivyo tajriba ya mtunzi pia inavyobadilika kwa sababu ya kuathiriwa kwa njia tofauti. Mabadiliko haya yanaweza kuelezwa kwa kuzingatia muktadha maalum kihistoria. Kubadilika kwa maudhui ya watunzi kwa mujibu wa wakati ndilo lengo la tasnifu hii. Udurusu wa utafiti na kauli ambazo zimezingatia maendeleo ya historia ya ushairi wa Kiswahili ulionyesha kwamba kazi nyingi hazikuzingatia vilivyo uhusiano kati ya utunzi na mazingira halisi yaliyo chimbuko la kazi hizo. Kwa hivyo, utafiti huu umechunguza kwa uketo mifumo iliyokuwepo wakati wa utunzi na kuonyesha namna mifumo hiyo ilivyoathiri na kuchangia usawiri wa maudhui katika nyakati mbalimbali. Utafiti umehusisha maendeleo ya jamii kihistoria na mabadiliko ya maudhui ili kudhihirisha kwamba mazingira ya kihistoria na kijamii huathiri utunzi kufani na kimaudhui. Hivyo, utafiti umebainisha kuwa ushairi wa Kiswahili una uyakini ulifungamana na wakati, mazingira na mifumo ya jamii. Madhumuni ya kazi hii yalikuwa kuchunguza sababu za maudhui ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kusawiriwa jinsi, yalivyosawiriwa katika vipindi tofauti vya historia. Aidha, kazi hii ilitathmini iwapo uchambuzi wa kihistoria unaweza kusaidia kufafanua uelewaji wa ushairi wa Kiswahili. Hivyo, utafiti huu umechangia kuhusu nadharia ya uchambuzi wa fasihi ya Kiswahili kwa kuzingatia mkabala wa kihistoria. Illhamu ya kazi hii ilitokana na sababu kwamba ushairi wa Kiswahili una historia ndefu. Kupitia ushairi, watunzi wameweza kuyasawiri na kuyahifadhi matukio mbalimbali katika historia na mazingira ya jamii. Pia, wameweza kuonyesha namna walivyoathiriwa katika mazingira ya nyakati tofauti. Vile vile, ushairi wa Kiswahili unaweza kuyakinishwa vyema zaidi kwa kuzingatia vipengele vya mipaka ya historia. Lakini jambo hili halikuwa limezingatiwa katika kazi nyingi ambazo tayari zimefanywa. Hivyo, utafiti huu ulikusudia kuonyesha uwiano kati ya maendeleo na mabadiliko ya maudhui, pamoja na kueleza chanzo cha mabadiliko hayo. Aidha, wageni kama vile Harries na Allen walidanganywa na baadhi ya vipengele vya muundo na maudhui na kudai kwamba ushairi wa Kiswahili ni wa kigeni. Kwa kuonyesha kwamba ushairi wa Kiswahili unaakisi matukio maalum katika historia ya jamii, utafiti huu umesahihisha baadhi ya kauli potoshi ambazo zimewahi kutolewa kuhusu taaluma hii. Utafiti umeonyesha kwamba misingi na mikondo ya historia ya jamii huipa fasihi umbo lake kifani na kimaudhui pamoja na mwelekeo. Hii ina maana kwamba ushairi wa Kiswahili unaweza kueleweka na kutathminiwa vyema zaidi kwa kuwekwa katika muktadha maalum kihistoria. Mbali na wageni, washairi wa Kiswahili waligawanyika katika makundi ya wanajadi na wanausasa kuhusu ufafanuzi wa maana na umbo la shairi la Kiswahili. haya yalizusha mgogoro katika ushairi wa Kiswahili. Maadam matapo haya hayakuzingatia ipasavyo historia ya ushairi, utafiti huu umeonyesha kwamba ushairi wa Kiswahili umekua, kupanuka na kuibua aina 'mpya' za utunzi kwa mujibu wa maendeleo ya jamii. Uchanganuzi uliongozwa na nadharia ya Uhistoria-Mpya. Kwa mujibu wa vipengele vya nadharia hii: (a) Kila kipindi cha historia kinawekwa katika awamu. Kila awamu inaongozwa na kutawaliw na mwelekeo au mkabala maalum wa maarifa yanayowiana na awamu hiyo. Katika maendeleo ya historia, awamu moja hupisha nyingine kuashiria enzi mpya katika historia ya maarifa. Mabadiliko ya awamu huathiri kwa kiasi kikubwa maana iliyopo ya kuwa binadamu. (b) Kuna kutambua nafasi muhimu na kubwa inayochukuliwa na muktadha wa kihistoria katika usomaji na uhakiki wa kazi za kifasihi. (c) Kuna kudahili kuwa kazi za kifasihi ni matokeo ya uhusiano changamano wa mwigiliano matini. (d) Kuchukua matukio au matendo ya kihistoria na kuyafanya sehemu ya msuko, hadithi au kazi ya kifasihi (umatini katika historia). (e) Kazi ya fasihi kuangaliwa sambamba na utamaduni wa historia ya jamii. (f) Mamlaka, uwezo au nguvu huathiri maana, utoaji na usomaji wa kazi wa kifasihi. (g) Kusisitiza mabadiliko kwa mujibu wa wakati. Utafiti huu unaipa tajriba ya msanii umuhimu kwa sababu huathiri namna anavyouona ulimwengu na kuusawiri. Hivyo, vipindi maalum vya maendeleo ya ushairi wa Kiswahili vimewakilishwa na utenzi wa Inkishafi, mashairi ya Shaaban Robert na ya Eurphrase Kezilahabi. Kazi hizi zimeonyesha kwamba kadri jamii inavyoendelea, utunzi pia huendelea na kubadilika. Uhakiki nao hauna budi kwenda sambamba na maendeleo hayo ili kuwa razini na mahitaji na matarajio ya wakati unaohusika. Maswala kama vile ubinafsi wa msanii, matatizo ya uainishaji mpya uliopendekezwa, dhana ya 'uhuru' katika mashairi-huru, na athari ya mazingira mapya kwa wasanii yalikuwa nje ya upeo wa utafiti huu. Hivyo, yanafaa kufanyiwa utafiti zaidi.
Description
The PL 8701.M37
Keywords
Swahili poetry--Kenya
Citation