Mapokeo na upya katika utenzi wa mwana kupona na vimelea vyake
Loading...
Date
2025-10
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
Kenyatta University
Abstract
Utafiti huu ulichunguza mapokeo na upya katika Utenzi wa Mwana Kupona na vimelea vyake. Utafiti huu ulichochewa na hoja kuwa Utenzi wa Mwana Kupona ni maarufu na umeshughulikiwa na wataalam mbalimbali kufikia sasa. Hata hivyo, tangu utenzi huo kutungwa mwaka wa 1858 kumekuwa na washairi mbalimbali ambao wametunga tenzi zinazoelekea kuwa mwangwi wa utenzi huo na yaelekea kuwa utafiti wa aina hiyo haujatiliwa maanani. Ili kuziba pengo hilo, uchanganuzi ulifanywa kwa kuzingatia tungo zikiwemo Utenzi wa Mwana Kupona uliotungwa 1858 na kuchapishwa 1971 na Allen, J. W. T., ‘Utenzi wa Hati’ na ‘Utenzi wa Adili’ katika tawasifu ya Shaaban Robert ya; Maisha Yangu na Baada ya Miaka Hamsini (1967). Utenzi wa Howani Mwana Howani uliotungwa na Zaynab Himid Mohammed mwaka wa 1983 na utenzi wa Jawabu la Mwana Kupona uliotungwa na EL-Maawy mwaka wa 2011. Utafiti huu ulilenga kuchunguza vipengele vya mapokeo katika Utenzi wa Mwana Kupona, kubainisha muumano katika Utenzi wa Mwana Kupona na vimelea vyake na kujadili upya katika vimelea vya Utenzi wa Mwana Kupona. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya Ki-Bakhtin kuhusu lugha. Nadharia hii ilibuniwa na Mikhail Bakhtin na kuendelezwa na Clark na Holquist (1984), Farmer (1998), Hirschkop (2001), Holquist (2002), Brandist (2002) kati ya wengine. Kwa mujibu wa nadharia hii, lugha au usemi wowote una nguvu za aina mbili: nguvu za kani kitovu na nguvu za kani pewa. Nguvu za kani kitovu ni sehemu ya lugha inayoelekezwa kwenye kitovu au katika mhimili mkuu wa mzunguko. Nguvu za kani pewa nazo ni sehemu ya lugha inayovuta kwenda nje ya kitovu. Nguvu kati ya kani kitovu na kani pewa ziliwasilisha mabadiliko ya lugha na zilihakikisha kuwa daima mabadiliko hayo yalibakia kushindana. Mhimili wa kani kitovu ulitumiwa kuchunguza mapokeo katika Utenzi wa Mwana Kuponana muumano uliopo kati ya Utenzi wa Mwana Kupona na vimelea vyake. Nao mhimili wa kani pewa ulitumiwa kuchunguza upya katika vimelea vya Utenzi wa Mwana Kupona. Utafiti huu ulikuwa wa kimaelezo. Utafiti ulijikita maktabani na nyanjani. Mtafiti alizuru maktaba mbalimbali zikiwemo za vyuo, kitaifa na dafina mbalimbali kama Research Institute of Swahili Studies of Eastern Africa (RISSEA) kwa lengo la kupata data faafu ya utafiti huu. Maktabani, vitabu, makala, majarida na wavuti zilisomwa kwa kina ili kupata data iliyosaidia katika kuweka msingi wa utafiti huu. Nyanjani, mtafiti alizuru eneo la Lamu kwa lengo la kupata mawazo ya wahojiwa kuhusu Utenzi wa Mwana Kupona. Mawazo hayo yalitumiwa kushadidia utafiti husika. Mtafiti alitumia maswali ya mwongozo wa mahojiano na mjadala ili kupata maoni ya wahojiwa yaliyochangia ufanisi wa utafiti huu. Sampuli iliteuliwa kimaksudi. Vitabu vilisomwa kwa kina ili kupata data faafu ya utafiti huu. Uchanganuzi ulifanywa kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya ki-Bakhtin kuhusu lugha pamoja na malengo ya utafiti. Data iliwasilishwa kwa njia ya maelezo katika sura mbalimbali. Ilibainika kwamba; tenzi hizi kwa kiasi kikubwa ziliazima kutoka katika Utenzi wa Mwana Kupona kifani na kimaudhui. Mambo waliyoazima yalikuwa mapokeo ambayo yalirithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine. Hata hivyo, japo warithi wa Mwana Kupona waliazima kutoka katika Utenzi wa Mwana Kupona, waliongeza upya katika tenzi zao ili kukidhi mahitaji ya wakati wao na hivyo kuzifanya tenzi hizi kuwa mwangwi wa Utenzi wa Mwana Kupona. Utafiti huu utachangia wasomi wa masuala ya fasihi ya Kiswahili katika kuonyesha uwezo wa vimelea vya Utenzi wa Mwana Kupona kama vifaa muhimu katika kuangazia mageuzi yaliyotokea katika jamii katika mpito wa wakati
Description
Tasnifu hii imewasilishwa kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya shahada ya uzamifu (ph. D) katika idara ya kiswahili, Shule ya Sheria, Fani na Sayansi za Jamii, Chuo Kikuu cha Kenyatta. Oktoba 2024
Supervisors:
Dkt. Richard Wafula
Prof. Ireri Mbaabu
Dkt. Pamela Ngugi